JUMATATU JUMA 18 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Hes.11:4-15
Wana wa Israeli walilia wakasema, N’nani atakayetupa nyama tule? Twakumbuka samaki tuliokula huko Misri bure; na yale matango, na matikiti, na mboga, na vitunguu, na vitunguu saumu; lakini sasa roho zetu zimekauka; hapana kitu cho chote; hatuna kitu cha kutumaini isipokuwa hi; mana tu. Na hiyo mana ilikuwa mfano wa chembe za mtarna, na kuonekana kwake kulikuwa kama kuonekana kwake bedola. Watu wakazunguka-zunguka na kuikusanya, kisha wakaisaga kwa mawe ya kusagia, au kuitwanga katika vinu, kisha wakaitokosa nyunguni, na kuandaa mikate; na tamaa yake ilikuwa kama tamu ya mafuta mapya. Umande ulipoyaangukia marago wakati wa usiku, hiyo mana ilianguka pamoja nao. Basi Musa akawasikia watu wakilia katika jamaa zao zote, kila mtu mlangoni pa hema yake; na hasira za Bwana zikawaka sana; Musa naye akakasirika. Musa akamwambia Bwana, Mbona umenitenda uovu mimi mtumishi wako? kwa nini sikupata neema machoni pako, hata ukanitwika mzigo wa watu hawa wote juu yangu? Je! ni mimi niliyewatungisha mimba watu hawa wote? je! ni mimi nilivewazaa, hata ikawa wewe kuniambia, Haya, wachukue kifuani mwako, mfano wa baba mwenye kulea achukuavyo mtoto aamwaye, wende nao mpaka nchi uliyowaapia baba zao? Nipate wapi nyama ya kuwapa watu hawa wote? kwani wanililia, wakisema, Tupe nyama, tupate kula. Mimi siwezi kuwachukua watu hawa wote peke yangu, kwa kuwa ni mzigo mzito sana wa kunishinda. Na kama ukinitenda hivi, nakuomba uniulie mbali, kwamba nimepata fadhili mbele ya macho yako; nami nisiyaone haya mashaka yangu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.81:11-16 (K)1
1. Watu wangu hawakuisikiliza sauti yangu, Wala Israeli hawakunitaka. Nikawaacha wakaenda kwa ukaidi wa mioyo yao, Waenende katika mashauri yao.

(K) Mwimbieni Mungu, nguvu zetu, nyimbo za furaha.

2. Laiti watu wangu wangenisikiliza, Na Israeli angeenenda katika njia zangu; Ningewadhili adui zao kwa upesi, Na juu ya watesi wao ningegeuza mkono wangu. (K)

3. Wamchukiao Bwana wangenyenyekea mbele zake, Bali wakati wao ungedumu milele. Naam, ningewalisha kwa unono wa ngano, Ningewashibisha kwa asali itokayo mwambani. (K)

SHANGILIO: Zab.119:34
Aleluya, aleluya!
Unifahamishe nami nitaishika sheria yako,
nitaitii kwa moyo wangu wote.
Aleluya!

INJILI: Mt.14:13-21
Yesu aliposikia; hayo, aliondoka huko katika chombo, akaenda mahali pasipo watu, faraghani. Na makutano waliposikia, walimfuata kwa miguu kutoka mijini mwao. Yesu akatoka, akaona mkutano mkuu, akawahurumia, akawaponya wagonjwa wao. Hata kulipokuwa jioni, wanafunzi wake walimwendea, wakasema, Mahali hapa ni nyika tupu, na saa imekwisha pita; uwaage makutano, waende zao vijijini, wakajinunulie vyakula. Yesu akawaambia, Hawana haja kwenda zao, wapeni ninyi vyakula. Wakamwambia, Hamna kitu hapa ila mikate mitano na samaki wawili. Akasema, Nileteeni hapa. Akawaagiza makutano waketi katika majani; akaitwaa ile mikate mitano na wale samaki wawili, akatazama juu mbinguni, akabariki, akaimega ile mikate, akawapa wanafunzi, wanafunzi wakawapa makutano. Wakala wote wakashiba; wakayaokota masazo ya vipande vya mikate, vikapu kumi na viwili, vimejaa. Nao waliokula walikuwa wanaume wapata elfu tano, bila wanawake na watoto.

--------------

--------------
MAOMBI
Ndugu, kazi ya kuwachunga kondoo wenye vionjo na matatizo mbalimbali ni ngumu. Inahitaji moyo na msaada wa Mungu mwenyewe. Ee Mungu twakuomba:-

Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Uwajalie Maaskofu wetu na Wachungaji wote wa Kanisa lako neema ya kuchukuliana na kondoo wanaowachunga kwa niaba yako. Ee Bwana.

2. Viongozi wetu wa serikali na wa taasisi mbalimbali watoe kwa watu wao huduma bora, kadiri wawezavyo, kulingana na haki za walengwa. Ee Bwana.

3. Utujalie sisi sote kukutegemea Wewe katika shida zetu, bila manung'uniko au malalamiko yasiyo na msingi. Ee Bwana.

4. Roho wako Mtakatifu awaimarishe wahubiri wa neno lako ili, kwa ujasiri wa kinabii, wapate kuutangaza ujumbe wako, kuusisitiza na, ikibidi, kukaripia, kuonya na kuhimiza watu kwa uvumilivu wote na wakati wote. Ee Bwana.

5. Ndugu zetu walioaga dunia wapokelewe katika ufalme wako huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu uliyewapa watu mkate kwa muujiza, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.