JUMATATU JUMA 17 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kut.32:15-24,30-34
Musa aligeuka akashuka katika mlima, na zile mbao nbili za mawe mikononi mwake; mbao zilizoaadikwa
pande zote mbili, upande huu na upande huu ziliandikwa. Na zile mbao zilikuwa kazi ya Mungu, nayo
maandiko yalikuwa maandiko ya Mungu, yaliyochorwa katika zile mbao. Na Yoshua aliposikia kelele za
watu walipokuwa wakipiga kelele, akamwambia Musa, Kuna kelele ya vita maragoni. Akasema, Hiyo si
sauti ya watu wapigao kelele kwa sababu ya kushinda vitani, wala si sauti ya watu wapigao kelele
kwa sababu ya kushindwa; bali kelele za watu waimbao ndizo ninazozisikia mimi. Hata alipoyakaribia
marago akaiona ila ndama, na ile michezo. Hasira ya Musa ikawaka, akazitupa zile mbao mikononi mwake,
akazivunja chini ya mlima. Akaitwaa ile ndama walioifanya, akaichoma moto, akaisaga hata ikawa mavumbi,
akainyunyiza juu ya maji, akawanywesha wana wa Israeli. Musa akamwambia Haruni; Watu hawa wamekufanyani
hata ukaleta dhambi hii kuu juu yao? Haruni akasema, Hasira ya bwana wangu isiwake; wewe unawajua
watu hawa, ya kuwa wamejielekeza kwa mabaya. Maana waliniambia, Katufanyie miungu, itakayokwenda
mbele yetu, kwa maana mtu huyo Musa, aliyetutoa katika nchi ya Misri, hatujui yaliyompata. Nikawaambia,
Mtu yeyote aliye na dhahabu na aivunje; basi wakanipa, nami nikaitupa ndani ya moto, akatoka ndama huyu.
Basi asubuhi yake Musa akawaambia watu, Mmetenda dhambi kuu; na sasa nitakwenda juu kwa Bwana, labda
nitafanya upatanisho kwa ajili ya dhambi yenu. Musa akarejea kwa Bwana, akasema, Aa! watu hawa
wametenda dhambi kuu, wamejifanyia miungu ya dhahabu. Walakini sasa, ikiwa utawasamehe dhambi yao
na kama sivyo, unifute, nakusihi, katika kitabu chako ulichokiandika. Bwana akamwambia Musa, Mtu
yeyote aliyenitenda dhambi, ndiye nitakayemfuta katika kitabu changu. Basi sasa uende ukawaongoze
watu hawa mpaka mahali pale ambapo nimekuambia habari zake; tazama, malaika wangu atakutangulia;
pamoja na hayo siku nitakavowajilia nitawapatiliza kwa ajili ya dhambi yao.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.106:19-23 (K)1
1. Walifanya ndama huko Horebu,
Wakaisujudia sanamu ya kuyeyuka.
Wakaubadili utukufu wao
Kuwa mfano wa ng’ombe mla majani.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema.
2. Wakamsahau Mungu, mwokozi wao,
Aliyetenda makuu katika Misri.
Matendo ya ajabu katika nchi ya Hamu,
Mambo ya kutisha penye bahari ya Shamu. (K)
3. Akasema ya kuwa atawaangamiza,
Kama Musa, mteule wakw, asingalisimama,
Mbele zake kama mahali paiipobomoka,
Ili aigeuze hasira yake asije akawaharibu. (K)
SHANGILIO: Efe.1:17,18
Aleluya, aleluya!
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristo,
awape roho ya hekima mjue
tumaini la mwito wake.
Aleluya!
INJILI: Yn.11:19-27
Watu wengi katika Wayahudi walikuwa wamekuja kwa Martha na Mariamu, ili kuwafariji kwa habari
ya ndugu yao. Basi Martha aliposikia kwamba Yesu anakuja, alikwenda kumlaki; na Mariamu alikuwa
akikaa nyumbani. Basi Martha akamwambia Yesu, Bwana, kama ungalikuwapo hapa, ndugu yangu
hangalikufa. Lakini hata sasa najua ya kuwa yoyote utakayomwomba Mungu, Mungu atakupa. Yesu
akamwambia, Ndugu yako atafufuka. Maratha akamwambia, Najua ya kuwa atafufuka katika ufufuo
siku ya mwisho. Yesu akamwambia, Mimi ndimi ufufuo, na uzima. Yeye aniaminiye mimi, ajapokufa,
atakuwa anaishi; naye kila aishiye na kuniamini hatakufa kabisa hata milele. Je! Unayasadiki
hayo? Akamwambia, Naam, Bwana, mimi nimesadiki ya kwamba wewe ndiwe Kristo, Mwana wa Mungu,
yule ajaye ulimwenguni.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu Baba, tunathubutu kulitaja jina lako na la
Mwanao wa pekee na la Roho Mtakatifu, tukitumaini
kupata msaada wako tunaposali.
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Uzipokee nia za Baba Mtakatifu wetu F., na
sala za Maaskofu na Mapadre wanazokutolea kwa ajili ya
wokovu wa watu wako wakosefu. Ee Bwana.
2. Uikinge nchi yetu na chachu ya sera mbaya za kigeni
zilizo kinyume si na amri zako tu, bali pia na mila,
desturi na tamaduni zetu nzuri. Ee Bwana.
3. Utujalie kuyathamini hata mambo madogomadogo
ambayo ni ya msingi katika kuukuza, kuulinda na
kuueneza ufalme wako hapa duniani. Ee Bwana.
4. Tunawaombea wenye kiburi, waovu, wakaidi na
wanaoabudu miungu mingine; waguswe mioyo yao
na kukuongokea Wewe. Ee Bwana.
5. Wakosefu wasamehewe dhambi zao; na marehemu
wetu wapokelewe mbinguni kunako uzima wa milele.
Ee Bwana.
Ee Mungu ambaye kwa mifano unayatamka yaliyositirika
tangu awali, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.