JUMATATU JUMA 16 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kut.14:5-18
Mfalme wa Misri aliambiwa ya kuwa wale watu wamekwisha kimbia; na moyo wa Farao, na mioyo ya watumishi
wake, iligeuzwa iwe kinyume cha hao watu, nao wakasema, Ni nini jambo hili tulilotenda, kwa kuwaacha
Waisraeli waende zao wasitutumikie tena? Akaandalia gari lake, akawachukua watu wake pamoja naye; tena
akatwaa magari mia sita yaliyochaguliwa, na magari vote ya Misri, na maakida juu ya magari hayo vote.
Na Bwana akaufanya moyo wake Farao mfalme wa Misri kuwa mgumu, naye akawafuata wana wa Israeli; kwa
sababu wana wa Israeli walitoka kwa ujeuri. Wamisri wakafuata nyuma yao, farasi zote na magari yote
ya Farao, na askari zake wenye kupanda farasi, na jeshi lake, nao wakawapata hali wamepanga pale karibu
na bahari, karibu na Pi-hahirothi, kukabili Baal-sefoni. Hata Farao alipokaribia, wana wa Israeli
wakainua macho yao, na tazama, Wamisri wanakuja nyuma yao; wakaogopa sana; wana wa Israeli wakamlilia
Bwana. Wakamwambia Musa, Je! kwa sababu hapakuwa na makaburi katika Misri umetutoa huko ili tufe
jangwani? Mbona umetutendea haya, kututoa katika nchi ya Misri? Neno hili silo tulilokuambia huko
Misri, tukisema, Tuache tuwatumikie Wamisri? Maana ni afadhali kuwatumikia Wamisri kuliko kufa
jangwani. Musa akawaambia watu, Msiogope, simameni tu, mkauone wokovu wa Bwana atakaowafanyia leo;
kwa maana hao Wamisri mliowaona leo hamtawaona tena milele. Bwana atawapigania ninyi, nanyi mtanyamaza
kimya. Bwana akamwambia Musa, Mbona unanililia mimi? Waambie wana wa Israeli waendelee mbele. Nawe
inua fimbo yako, ukanyoshe mkono wako juu ya bahari, na kuigawanya; nao wana wa Israeli watapita kati
ya bahari katika nchi kavu. Nami, tazama, nitaifanya mioyo ya Wamisri kuwa migumu, nao wataingia na
kuwafuatia, nami nitajipatia utukufu kwa Farao, na kwa jeshi lake lote, kwa magari yake na kwa wapanda
farasi wake. Na Wamisri watajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, nitakapokwisha kujipatia utukufu kwa Farao,
na magari yake, na farasi zake.
WIMBO WA KATIKATI: Kut.15:1-6 (K)1
1. Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana;
Farasi na mpanda farasi amewatupa baharini.
Bwana ni nguvu zangu, na wimbo wangu;
Naye amekuwa wokovu wangu.
Yeye ni Mungu wangu, nami nitamsifu;
Ni Mungu wa baba yangu, nami nitamtukuza.
(K) Nitamwimbia Bwana, kwa maana ametukuka sana.
2. Bwana ni mtu wa vita,
Bwana ndilo jina lake.
Magari ya Farao na jeshi lake amewatupa baharini,
Maakida yake wateule wamezama katika bahari ya Shamu. (K)
3. Vilindi vimewafunikiza,
Walizama vilindini kama jiwe.
Bwana, mkono wako wa kuume
umepata fahari ya uwezo,
Bwana, mkono wako wa kuume wawasetaseta adui. (K)
Shangilio: Yn.15:15
Aleluya, aleluya,
Bwana anasema: Siwaiti tena watumwa,
lakini ninyi nimewaita rafiki,
kwa kuwa yote niliyoyasikia kwa Baba yangu nimewaarifu.
Aleluya.
INJILI: Mt.12:38–42
Baadhi ya waandishi wa Mafarisayo walimjibu Yesu wakasema, Mwalimu, twataka kuona ishara kwako.
Akajibu, akawaambia, Kizazi kibaya na cha zinaa chatafuta ishara, wala hakitapewa ishara, ila
ishara ya nabii Yona. Kwani kama vile Yona alivyokuwa siku tatu mchana na usiku katika tumbo la
nyangumi, hivyo ndivyo Mwana wa Adamu atakavyokuwa siku tatu mchana na usiku moyo wa nchi. Watu
wa Ninawi watasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, nao watawahukumu kuwa wamekosa;
kwa sababu wao walitubu kwa mahubiri ya Yona; na hapa yupo aliye mkuu kuliko Yona. Malkia wa kusini
atasimama siku ya hukumu pamoja na watu wa kizazi hiki, naye atawahukumu kuwa wamekosa; kwa sababu
yeye alikuja kutoka pande za mwisho za dunia ili asikie hekima ya Sulemani, na hapa yupo aliye
mkuu kuliko Sulemani.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Bwana wetu Yesu Krsito ni Mkuu kuliko Sulemani.
Kwa vile wapo wengi wasiomkiri bado hata katika
kizazi hiki chetu, tumwombe Mungu tukisema:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Kwa nguvu ya Utatu Mtakatifu, uwaongezee Askofu
wetu F. na viongozi wote wa Kanisa bidii ya kuhubiri
toba katika kizazi hiki kinachotaka ishara. Ee Bwana.
2. Wote wenye mapenzi mema washirikiane na viongozi
wa serikali, katika kupambana na wahalifu wanaokosesha
amani na utulivu hapa nchini. Ee Bwana.
3. Sisi sote tutumie vema neema ya ukombozi tulioupata
kwa Fumbo Kuu la Pasaka, ili tuishi kitakatifu na hivi
kushinda hukumu siku ya mwisho. Ee Bwana.
4. Utujalie kutenda haki, kupenda rehema, na kwenda
kwa unyenyekevu mbele yako; kwani ndiyo sadaka
bora kabisa kwako. Ee Bwana.
5. Uwahurumie marehemu wetu na kuwashirikisha
uzima mpya pamoja na watakatifu wako huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyewapigania wana wa Israeli dhidi ya
maadui, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.