JUMATATU JUMA 14 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Mwa.28:10-22
Yakobo alitoka Beer-sheba, kwenda Harani. Akafika mahali fulanl akakaa huko usiku kucha, maana jua
lilikuwa limekuchwa; akatwaa jiwe moja la mahali pale akaliweka chini ya kichwa chake, akalala
usingizi pale pale. Akaota ndoto; na tazama, ngazi imesimamisha juu ya nchi, na ncha yake yafika
mbinguni. Tena, tazama. malaika wa Mungu wanapanda, na kushuka juu yake. Na tazama, Bwana amesimama
juu yake, akasema, Mimi ni Bwana, Mungu wa Ibrahimu baba yako, na Mungu wa Isaka; nchi hii uilalayo
nitakupa wewe na uzao wako. Na uzao wako utakuwa kama mavumbi ya nchi, nawe utaenea upande wa
magharibi, na mashariki, na kaskazini, na kusini; na katika wewe, na katika uzao wako, jamaa zote
za dunia watabarikiwa. Na tazama, mimi nipo pamoja nawe, nitakulinda kila uendako, nami nitakuleta
tena mpaka nchi hii, kwa maana sitakuacha, hata nitakapokufanyia hayo niliyokuambia. Yakobo akaamka
katika usingizi wake, akasema, Kweli, Bwana yupo mahali hapa, wala mimi sikujua. Naye akaogopa
akasema, Mahali hapa panatisha kama nini! Bila shaka, hapa ni nyumba ya Mungu, napo ndipo lango
la mbinguni. Yakobo akaondoka asubuhi na mapema, akalitwaa lile jiwe aliloliweka chini ya kichwa
chake, akalisimamisha kama nguzo, na kumimina mafuta juu yake. Akaita jina la mahali pale Betheli;
lakini jina la mji ule hapo kwanza uliitwa Luzu. Yakobo akaweka nadhiri akisema, Mungu akiwa pamoja
nami, akinilinda katika njia niiendeayo, na kunipa chakula nile, na nguo nivae; nami nikirudi kwa
amani nyumbani kwa baba yangu, ndipo Bwana atakuwa Mungu wangu. Na jiwe hili nililosimamisha kama
nguzo litakuwa nyumba ya Mungu; na katika kila utakalonipa hakika nitakutolea wewe sehemu ya kumi.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.91:1-4,14-15 (K)2
1. Aketiye mahali pa siri pake Aliye juu
Atakaa katika uvuli wake Mwenyezi.
Nitasema, Bwana ndiye kimbilio langu na ngome yangu,
Mungu wangu nitakayemtumaini.
(K) Mungu wangu nitakayemtumaini.
2. Maana Yeye atakuokoa na mtego wa mwindaji,
Na katika tauni iharibuyo.
Kwa manyoya yake atakufunika,
Chini ya mbawa zake utapata kimbilio;
Uaminifu wake ni ngao na kigao. (K)
3. Kwa kuwa amekaza kunipenda
Nitamwokoa; na kumweka palipo juu,
Kwa kuwa amenijua jina langu.
Ataniita nami nilamwitikia;
NitaKuwa pamoja naye taabuni,
Nitamwokoa na kumtukuza. (K)
SHANGILIO: Lk.8:15
Aleluya, aleluya!
Wanabarikiwa wale ambao kwa unyofu na wema wa mioyo yao,
hulisikia neno la Mungu na kulishika.
Aleluya!
INJILI: Mk1:14-20
Yesu alipokuwa akiwaambia hayo, tazama, akaja jumbe mmoja, akamsujudia, akisema, Binti yangu
sasa hivi amekufa; lakini njoo, uweke mkono wako juu yake, naye ataishi. Akaondoka Yesu, akamfuata,
pamoja na wanafunzi wake. Na tazama, mwanamke aliyekuwa na ugonjwa wa kutoka damu muda wa miaka
kumi na miwili, alikuja kwa nyuma, akaugusa upindo wa vazi lake. Kwa maana alisema moyoni mwake,
Nikigusa tu upindo wa vazi lake nitapona. Yesu akageuka, akamwona, akamwambia, Jipe moyo mkuu,
binti yangu, Imani yako imekuponya. Yule mwanamke akapona tangu saa ile. Yesu alipofika nyumbani
kwa yule jumbe, aliona wapiga filimbi, na makutano wakifanya maombolezo, akawaambia, Ondokeni; kwa
maana kijana hakufa, amelala tu. Wakamcheka sana. Lakini makutano walipoondoshwa, aliingia, akamshika
mkono; yule kijana akasimama. Zikaenea habari hizi katika nchi ile yote.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, Wewe ni mwaminifu katika ahadi zako; na akuombaye
kwa imani hakosi kupata thawabu yake. Kwa hiyo twakuomba.
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Baba Mtakatifu wetu F., na
Wakleri wote wadumu kiaminifu katika kuwafundisha waamini
uliowaposa wawe wako kwa milele; ili wakujue Wewe. Ee Bwana.
2. Kwa huruma yako, uendeleze miujiza yako katika
Kanisa na dunia nzima ya leo inayozidi kuonewa na
ibilisi. Ee Bwana.
3. Serikali yetu itoe kipaumbele katika huduma za afya;
na uzikinge jamii zetu na imani potofu dhidi ya vifo
na magonjwa. Ee Bwana.
4. Utumiminie baraka zako na kumjalia kila mmoja wetu
kukutegemea Wewe Mungu katika taabu na raha. Ee Bwana.
5. Wagonjwa wetu wapone na wafu wafufuliwe na
kushiriki uzima mpya. Ee Bwana.
Ee Mungu unayemjazi kila anayekujia kwa imani na
matumaini, uipokee sala yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana
wetu. Amina.