JUMATATU JUMA 13 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Mwa.18:16-33
Watu hao waliondoka huko wakaelekeza nyuso zao Sodoma. Ibrahimu akaenda pamoja nao awasindikize. Bwana akanena, Je! Nimfiche Ibrahimu jambo nilifanyalo, akiwa Ibrahimu atakuwa taifa kuu, hodari, na katika yeye mataifa yote ya dunia watabarikiwa? Kwa maana nimemjua ya kwamba atawaamuru wanawe, na nyumba yake baada yake waishike njia ya Bwana, wafanye haki na hukumu, ili kwamba Bwana naye akamtimizie Ibrahimu ahadi zake. Bwana akasema, Kwa kuwa kilio cha Sodoma na Gomora kimezidi, na dhambi zao zimeongezeka sana, basi, nitashuka sasa nione kama wanayotenda ni kiasi cha kilio kilichonijia; na kama sivyo, nitajua. Basi wale watu wakatoka huko wakaelekea Sodoma; lakini Ibrahimu alikuwa akali akisimama mbele za Bwana. Ibrahimu akakaribia, akasema, Je! Utaharibu mwenye haki pamoja na mwovu? Huenda wakawapo wenye haki hamsini katika mji, utaharibu, wala hutauacha mji kwa ajili ya hao hamsini wenye haki waliomo? Hasha usifanye hivyo, ukamwue mwenye haki pamoja na mwovu, mwenye haki awe kama mwovu. Hasha; Mhukumu ulimwengu wote asitende haki? Bwana akasema, Nikiona katika Sodoma wenye haki hamsini mjini, nitapaacha mahali pote kwa ajili yao. Ibrahimu akajibu, akasema, Basi, nimeshika kusema na Bwana, nami ni mavumbi na majivu tu. Huenda wakapunguka watano katika wale hamsini wenye haki, je! Utaharibu mji wote kwa kupungua watano? Akasema, Sitauharibu, nikiona humo arobaini na watano. Akazidi tena kusema naye, akinena, Huenda wakaonekana humo arobaini? Akasema, Sitafanya kwa ajili ya hao arobaini. Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema, Huenda wakaonekana huko thelathini? Akasema, Sitafanya, nikiona humo thelathini. Akasema, Tazama, nimeshika kusema na Bwana, huenda wakaonekana huko ishirini? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao ishirini. Akasema, Bwana asiwe na hasira, nami nitasema mara hii tu, Huenda wakaonekana huko kumi? Akasema, Sitaharibu kwa ajili ya hao kumi. Basi Bwana alipokwisha kuzungumza na Ibrahimu, akaenda zake; Ibrahimu naye akarudi mahali pake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.103:1-4,8-11 (K)8
1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana. Naam, vyote vilivyo ndani yangu Vilihimidi jina lake takatifu. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana, Wala usizisahau fadhili zake zote.

(K) Bwana amejaa huruma na neema.

2. Akusamehe maovu yako yote, Akuponya magonjwa yako yote, Aukomboa uhai wako na kaburi, Akutia taji ya fadhili na rehema, (K)

3. Bwana amejaa huruma na neema, Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili. Yeye hatateta sikuzote, Wala hatashika hasira yake milele. (K)

4. Hakututenda sawasawa na hatia zetu, Wala hakutulipa kwa kadiri ya maovu yetu. Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi, Kadiri ile ile rehema zake ni kuu kwa wamchao. (K)

SHANGILIO: Yn.10:27
Aleluya, aleluya!
Kondoo wangu huisikia sauti yangu;
mimi nawajua, nao hunifuata.
Aleluya!

INJILI: Mt.8:18-22
Yesu alipoona makutano mengi wakimzunguka, aliamuru kuvuka kwenda ng’ambo. Mwandishi mmoja akamwendea, akamwambia, Mwalimu, nitakufuata kokote uendako. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana vioto; lakini Mwana wa Adamu hana pa kulaza kichwa chake. Mwingine katika wanafunzi wake akamwambia, Bwana, nipe ruhusa kwanza, niende nikamzike baba yangu. Lakini Yesu akamwambia, Nifuate; waache wafu wazike wafu wao.

--------------

--------------
MAOMBI
Kwa vile tunautambua utukufu wa Utatu Mtakatifu wa milele katika kuungama imani ya kweli, hatuna budi kumwomba Mungu mwenyewe tukisema.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Pokea sala za Baba Mtakatifu, Maaskofu na Mapadre wanazokutolea kwa ajili ya Kanisa lako. Ee Bwana.

2. Uwaonye watu wa mataifa wasiotaka kukukiri Wewe Mungu, wala kuzitubu dhambi zao. Ee Bwana.

3. Utujalie kuitikia mwito wako wa kuitangaza Injili kokote unakotaka, bila kutoa udhuru wala masharti yoyote. Ee Bwana.

4. Kwa huruma yako, utuepushe na dhambi zinazoichafua miili yetu ambayo ni hekalu la Roho wako Mtakatifu. Ee Bwana.

5. Uwapokee ndugu zetu marehemu katika makao yako ya milele huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu uliyewafunulia watakatifu makusudio ya moyo wako, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.