JUMATATU JUMA 11 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 2Kor.6:1–10
Nasi tukitenda kazi pamoja naye twawasihi, msiipokee neema ya Mungu bure. Kwa maana asema, Wakati
uliokubalika nalikusikia, Siku ya wokovu nalikusaidia; tazama, wakati uliokubalika ndio sasa.
Tusiwe kwazo la namna yoyote katika jambo lolote, ili utumishi wetu usilaumiwe; bali katika kila
neno tujipatie sifa njema, kama watumishi wa Mungu; katika saburi nyingi, katika dhiki, katika
misiba, katika shida; katika mapigo, katika vifungo, katika fitina, katika taabu, katika kukesha,
katika kufunga; katika kuwa safi, katika elimu, katika uvumilivu, katika utu wema, katika Roho
Mtakatifu, katika upendo usio unafiki; katika neno la kweli, katika nguvu ya Mungu; kwa silaha
za haki za mkono wa kuume na za mkono wa kushoto; kwa utukufu na aisbu; kwa kunenwa vibaya na
kunenwa vema; kama wadanganyao, bali tu watu wa kweli; kama wasiojulikana, bali wajulikanao sana;
kama wanaokufa, kumbe tu hai; kama wanaorudiwa, bali wasiouawa; kama wenye huzuni, bali sikuzote
tu wenye furaha; kama maskini, bali tukitajirisha wengi; kama wasio na kitu, bali tu wenye vitu
vyote.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:1-4. (K)2
1. Mwimbieni Bwana wimbo mpya,
Kwa maana ametenda mambo ya ajabu.
Mkono wa kuume wake mwenyewe,
Mkono wake mtakatifu umemtendea wokovu.
(K) Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
2. Machoni pa mataifa ameidhihirisha haki yake.
Amezikumbuka rehema zake,
Na uaminifu wake kwa nyumba ya Israeli. (K)
3. Miisho yote ya dunia imeuona
Wokovu wa Mungu wetu.
Mshangilieni Bwana, nchi yote,
Inueni sauti, imbeni kwa furaha, imbeni zaburi. (K)
SHANGILIO: Efe.1:17,18
Aleluya, aleluya!
Mungu wa Bwana wetu Yesu Kristu,
awape roho ya hekima mjue tumaini la mwito wake.
Aleluya!
INJILI: Mt.5:38-42
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Mmesikia kwamba imenenwa Jicho kwa jicho, na jino kwa jino;
lakini mimi nawaambia, Msishindane na mtu mwovu; lakini mtu akupigaye shavu la kuume, mgeuzie
na la pili. Na mtu atakaye kukushitaki na kuitwaa kanzu yako, mwachie na joho pia. Na mtu
atakayekulazimisha mwendo wa maili moja, nenda naye mbili. Akuombaye, mpe; naye atakaye kukopa
kwako, usimpe kisogo.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu unayeendelea kutufumbulia fumbo lako la
ajabu, kwa kutuletea ulimwenguni Neno wako wa
kweli na Roho Mtakatifu, twakuomba.
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Ili Baba Mtakatifu wetu F., na viongozi wote wa
Kanisa wawe daima kielelezo cha maadili mema kwa
waamini wako. Ee Bwana.
2. Ili Raisi wetu F., na watawala wote wa
dunia washinde vishawishi vyote dhidi ya yule mwovu, ili watu
wako wafaidi matunda ya kazi zao njema. Ee Bwana.
3. Ili wote wenye mamlaka watumie madaraka yao
vizuri, hasa kuwatetea wanyonge wanaodhulumiwa
sababu ya kutetea haki zao. Ee Bwana.
4. Ili katika utumishi wetu asiwepo wa kulaumiwa bali,
katika kila neno, kila mmoja wetu ajipatie sifa njema
na kulijua tumaini la wito wake. Ee Bwana.
5. Ili marehemu wetu wasamehewe dhambi zao na
kuvikwa taji la uzima wa milele. Ee Bwana.
Ee Mungu unayewapa watu roho ya hekima isiyo na kisasi,
uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.