JUMATATU JUMA 10 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 2Kor.1:1-7
Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo ndugu yetu; kwa kanisa la Mungu
lililoko Korintho, pamoja na watakatifu wote walioko katika nchi yote ya Akaya. Neema na iwe
kwenu na Amani zitokazo kwa Mungu Baba yetu na kwa Bwana Yesu Kristo. Na ahimidiwe Mungu, Baba
wa Bwana wetu Yesu Kristo, Baba wa rehema, Mungu wa faraja yote; atufarijiye katika dhiki zetu
zote ili nasi tupate kuwafariji wale walio katika dhiki za namna zote, kwa faraja hizo,
tunazofarijiwa na Mungu. Kwa kuwa kama vile mateso ya Kristo yanavyozidi kwetu, vivyo hivyo
faraja yetu inazidi kwa njia ya Kristo. Lakini ikiwa sisi tu katika dhiki, ni kwa ajili ya
faraja yenu na wokovu wenu; au ikiwa twafarijiwa, ni kwa ajili ya faraja yenu; ambayo hutenda
kazi yake kwa kustahimili mateso yale tuteswayo na sisi. Na tumaini letu kwa ajili yenu ni imara,
tukijua ya kuwa kama vile mlivyo washiriki wa yale mateso, vivyo hivyo mmekuwa washiriki wa zile
faraja.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.34:1–8 (K)8
1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.
(K) Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema.
2. Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote. (K)
3. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote. (K)
4. Malaika wa Bwana hufanya kituo,
Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema;
Heri mtu yule anayemtumaini. (K)
SHANGILIO: Zab.119:18
Aleluya, aleluya!
Unifumbue macho yangu niyatazame,
maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya!
INJILI: Mt.5:1-12
Naye Yesu alipowaona makutano, alipanda mlimani; na alipokwisha kuketi, wanafunzi wake walimjia;
akafumbua kinywa chake, akawafundisha, akisema, Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni
ni wao. Heri wenye huzuni; Maana hao watafarijika. Heri wenye upole; Maana hao watairithi nchi. Heri
wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa. Heri wenye rehema; Maana hao watapata rehema.
Heri wenye moyo safi; Maana hao watamwona Mungu. Heri wapatanishi; Maana hao wataitwa wana wa Mungu.
Heri wenye kuudhiwa kwa ajili ya haki; Maana ufalme wa mbinguni ni wao. Heri ninyi watakapowashutumu
na kuwaudhi na kuwanenea kila neno baya kwa uongo, kwa ajili yangu. Furahini, na kushangilia; kwa kuwa
thawabu yenu ni kubwa mbinguni; kwa maana ndivyo walivyowaudhi manabii waliokuwa kabla yenu.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, huku tukiungama Umoja wa Mungu katika
Utatu Mtakatifu wa milele, tumpelekee Mungu maombi
yetu:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwape neema ya uthabiti na kuwafariji viongozi wetu
wa Kanisa katika huzuni na mateso wayapatayo katika
utume wao. Ee Bwana.
2. Watawala wa dunia walisikilize neno lako na
kuzitii sauti za manabii wako; wapate kuwaongoza
watu kadiri ya mapenzi yako. Ee Bwana.
3. Wote wenye wajibu wa kuzitoa huduma za jamii
wawe tayari kuyakabili mateso; na faraja yao iwe katika
kuwatendea wenzao yale ambayo wao wenyewe wangependa
kutendewa. Ee Bwana.
4. Sisi sote tujaliwe kuziishi heri zote tulizofunuliwa
na Bwana wetu Yesu Kristo, kwa ajili ya ufalme wa
mbinguni. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wapewe msamaha wa dhambi na
furaha isiyo na mwisho huko mbinguni. Ee Bwana.
Tunaomba hayo yote kwako, Ee Mungu, kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.