JUMATANO JUMA LA 7 PASAKA
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Bwana Mungu na wa vyote Muumba,
Ulimwengu nawe wategemezwa.
Vyote hubadilika na kuoza,
Wewe hapana, wabaki ni Mpуа.
Ndiwe faraja na ya mtu kinga,
U Mwamba juu yake wa kujenga,
Ndiwe makao tulivu ya roho,
Yote hutimilika ndani yako.
Asifiwe Baba na Mwana Mungu,
Asifiwe Roho Mtakatifu;.
Na utukuzwe Utatu milele,
Nguvu yetu maisha yetu yote.
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya
Zab.119:105-112 XIV Sheria ya Mungu ni mwanga
Neno lako ni taa ya kuniongoza,*
na mwanga katika njia yangu.
Nimeapa na kuthibitisha kiapo changu,*
kwamba nitashika maagizo yako maadilifu.
Ee Mungu, ninateseka mno;*
unipe uhai kama ulivyoahidi.
Ee Mungu, upokee sala yangu ya shukrani;*
na unifundishe maagizo yako.
Maisha yangu yamo hatarini daima,*
lakini siisahau sheria yako.
Waovu wamenitegea mitego kuninasa,*
lakini sikiuki amri zako.
Maagizo yako ni rasilmali yangu daima;*
naam, ni furaha ya moyo wangu.
Nimekusudia kwa moyo wote*
kutimiza kanuni zako milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.70 Kuomba msaada
Bwana, utuokoe, tunaangamia (Mt.8:25)
Upende, Ee Mungu, upende kuniokoa;*
Ee Mungu, uje hima kunisaidia!
Waaibike na kufedheheka,*
hao wanaotaka kuniangamiza!
Warudishwe nyuma na kupata aibu,*
hao wanaofurahia maafa yangu!
Wapumbazike kwa aibu,*
hao wanaofurahia kunidhihaki!
Lakini wote wale wanaokutafuta,*
Wafurahi na kushangilia kwa sababu yako.
Wote wale wapendao nguvu yako ya kuokoa,*
waseme daima: “Mungu ni mkuu mno!"
Mimi niliye mnyonge na fukara,*
unijie hima, Ee Mungu!
Wewe ni msaada wangu, na mkombozi wangu;*
Ee Mungu, usikawie kunisaidia.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.75 Mungu hakimu
Amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao. vya enzi, akawakweza wanyenyekevu (Lk.1:52)
Tunakushukuru, Ee Mungu, tunakushukuru!/
Tunatangaza ukuu wako,*
na kusimulia juu ya matendo yako makuu.
"Mimi," asema Mungu, "nimeweka wakati maalum!*
Wakati huo nitatoa hukumu iliyo sawa.
Nchi ikitetemeka na vyote vilivyomo,*
mimi ndiye ninayeitegemeza misingi yake.
Nawaambia wenye kiburi: 'Acheni kujigamba!'*
na waovu: 'Msioteshe pembe za majivuno!
Msijione kuwa watu wa maana sana,*
hata kusema maneno ya kiburi.' "
Hukumu haiji kutoka mashariki au magharibi;*
wala haitoki nyikani au mlimani.
Mungu mwenyewe ndiye hakimu;*.
humshusha mmoja na kumkweza mwingine.
Mungu anashika kikombe mkononi,*
kimejaa divai kali ya hasira yake;
anaimimina, na waovu wote wanainywa;*
naam, wanainywa mpaka tone la mwisho.
Lakini mimi nitafurahi milele,*
nitamwimbia sifa Mungu wa Yakobo.
Atavunja nguvu zote za watu waovu;*
lakini nguvu za waadilifu ataziimarisha.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Rom.4:24-25
Sisi tunamwamini Mungu aliyemfufua Yesu, Bwana wetu, katika wafu. Yeye alitolewa auawe kwa
ajili ya dhambi zetu, akafufuliwa ili tupate uhusiano mwema na Mungu.
K. Bwana amefufuka kweli, aleluya.
W. Amemtokea Simoni, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: 1Yoh.5:5-6
Nani, basi, awezaye kuushinda ulimwengu? Ni yule anayeamini kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.
Yesu Kristo ndiye aliyekuja kwa maji ya ubatizo wake na kwa damu ya kifo chake. Hakuja kwa
maji tu, bali kwa maji na kwa damu. Naye Roho anashuhudia kwamba ni kweli, kwani Roho ni
ukweli.
K. Wanafunzi walifurahi, aleluya.
W. Walipomwona Bwana, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: Ef.4:23-24
Jirekebisheni upya rohoni na katika fikra zenu. Vaeni hali mpya ya utu ambayo imeumbwa kwa
mfano wa Mungu, na ambayo hujionesha katika maisha ya kweli ya uadilifu na utakatifu.
K. Kaa nasi, Bwana, aleluya.
W. Maana usiku unakaribia, aleluya.
SALA:
Tuombe: Mungu mwenye huruma, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, umewakusanya pamoja waamini wako.
Utudumishe katika utumishi wako, na katika umoja wetu. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo
Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.