JUMATANO JUMA LA 7 PASAKA
MASIFU YA JIONI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI chagua 1-5(32-36)
1 (32)
Roho Muumbaji njoo kwetu
Ushuke toka juu uliko,
Njoo uzitwae roho zetu,
Zote uzifanye mali yako.
Wewe unaitwa Mfariji,
Thawabu isiyo na kifani,
Ni chemchemi na moto hai,
Ndiwe manukato na upendo.
Mtoaji wa vipaji saba,
Kidole cha kuume cha Mola;
Sisi wadogo watufundisha
Kusema na pia kuelewa.
Uziangaze akili zetu,
Washa upendo mioyo yetu;
Na kwa zako za daima nguvu
Iimarishe miili yetu.
Mfukuzie mbali mwuaji,
Amani ya kweli tuipate;
Na kila janga utuepushe
Kwa zako mbawa utulinde.
Kumjua Baba tujalie
Na huyo wa milele Mwanae,
Wewe Roho pia tukujue,
Watatu nyie Mungu Mmoja.
Baba utukufu wote kwako,
Na kwa Mwanao mlio sawa,
Pia kwa Mfariji Mkuu:
Ninyi mtukuzwe bila mwisho.
2 (33)
Njoo, Ewe Muumbaji,
Njoo, Roho mtukufu,
Uje ujipumzishe
Rohoni mwetu karibu;
Uje na neema zako
Na misaada ya mbingu,
Ili tele kuijaza
Mioyo uloiumba.
E Mfariji Mkuu,
Tunakulilia Bwana,
Ewe karama kamambe
'Toka kwa Mungu Mkuu,
Chemchemi ya Uzima,
Ewe Moto wa Upendo,
Na mafuta ya kupaka -
Mazuri kutoka juu!
Wewe unajulikana
Kwa mapaji yako saba;
U kidole, tunakiri,
Cha mkono wake Mungu;
Wewe pia ni ahadi
Ya Baba Mwenyezi Mungu,
Ulimi waujalia
Uwezo wa kuongea.
Viwashe vyetu vionjo
Kutoka juu uliko,
Na zifanye zetu nyoyo
Zifurike kwa upendo;
Twondolee udhaifu
Wa hii miili yetu,
Saburi utugawie
Nazo fadhila kamambe.
Fukuzia mbali nasi
Adui tumwogopaye,
Na badala yake tupe
Amani yako ya kweli;
Wewe ukituongoza
Nasi tukikufuata,
Basi hatutaiacha
Njia ile ya uzima.
Twaomba yako neema
Itujalie, twaomba,
Kumjua yeye Baba,
Mwanae na Wewe pia,
Ambaye kila wakati
Bila mwisho tunakiri
U Roho wa Baba, Mwana,
Roho wao wa milele.
Utukufu wote wote,
Tena kwa nyakati zote,
Kwake yeye Mungu Baba
Na pia kwa wake Mwana,
Mfufuka 'toka wafu;
Pia kwako utukufu,
E Roho Mtakatifu,
Kwa milele mtukufu.
3 (34)
Ewe Roho wa Mungu Mwenyezi,
Juu ya nchi tupu gizani
Kwa uwezo mwingi uliruka
Ulimwengu ulipoumbika;
Mambo mazuri ukatengeza
Kwa ule udongo na vurugu,
Uzima wa Mungu livuvia
Katika pua yake adamu;
Njoo ili upande uhai
Katika nafsi zetu duni,
Sali ndani yetu, utuunde
Tuwe wana ndani yake Mwana.
Ee Roho uliye muweza,
Nyoyo zetu kwako elekeza,
Utuingize katika uzima
Ndani ya Utatu, Mungu 'Moja.
Stanbrook Abbey Hymnal
4 (35)
Shuka chini, Upendo wa Kimungu,
Uitafute hii roho yangu,
Na itembelee kwa ari yako,
Kwa ari yako hiyo iwakayo;
E Mfariji sogea karibu,
Jitokeze ndani ya moyo wangu,
Na uuwashe na kuupatia
Mwako wako mtakatifu sana.
Uuache uwake peke yake,
Mpaka tamaa za kidunia
Zitapoungua kwa joto lake
Na kuwa vumbi na majivu hasa;
Nayo hiyo nuru yako tukufu
Na iniangazie macho yangu,
Na inifunike mimi kabisa
Wakati yanimulikia njia.
Unipe upendo mtakatifu
Ili uwe vazi langu la nje,
Unipatie na unyenyekevu
Ili uwe vazi langu la ndani:
Unyenyekevu halisi wa moyo,
Ambao hutwaa yaliyo duni,
Na ambao hulia kwa uchungu
Juu ya kasoro zake wenyewe.
Na hivi ile tamaa ya roho,
Hamu kubwa isiyo na kipimo,
Wanadamu watashindwa kabisa
Kuieleza na kusimulia;
Maana hakuna anayeweza,
Kukisia hasa yake neema
Mpaka mwenyewe awe makao,
Makao ya Mtakatifu Roho.
Bianco da Siena +1434
5 (36)
Pendo la Baba na la Mungu Mwana,
Pendo ulo chanzo cha vitu vyote,
Ulotengeza uzuri wa mbingu,
Lengo na uhai wa ulimwengu.
Ewe Mwenyezi na Mtakatifu,
Amani na haki watuletea,
Viumbe kwa wema wavitendea,
Na waviepusha na kila ovu.
Usafi, cheo, hekima, haki,
Ukweli: vyote unavyo kamili;
Kwa njia ya Kristo mwenyewe,
Watutenga na mambo ya dunia.
Watu wote wakuabudu wewe,
Uliye mtukufu kwa milele
Tufariji sisi viumbe wako,
Jalia tufaidi mwanga wako.
Robert Bridges 1844-1930
ANT. I: Huzuni yenu itageuka kuwa furaha, aleluya.
Zab.126 Kuomba nguvu mpya
Mkishiriki mateso yetu, mtashiriki pia faraja yetu (2Kor.1:7)
Mungu alipoturudisha tena Sion,*
tulikuwa kama wanaoota ndoto!
Hapo tuliangua kicheko;*
tulishangilia kwa furaha.
Nao watu wa mataifa mengine walisema:*
“Mungu amewatendea mambo makubwa!“
Kweli Mungu alitutendea maajabu,*
tulifurahi kweli kweli!
Ee Mungu, urekebishe tena hali yetu,/
kama mvua inavyotiririsha maji*
katika mabonde makavu.
Wanaopanda kwa machozi*
watavuna kwa shangwe.
Wanaokwenda kupanda mbegu huku wakilia,*
watarudi kwa furaha huku wakichukua mavuno.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Huzuni yenu itageuka kuwa furaha, aleluya.
ANT. II: Tuwe tunaishi au tuwe tunakufa, tu mali ya Bwana, aleluya.
Zab.127 Bila Mungu kazi ya binadamu haifai
Ninyi ni jengo lake Mungu (1Kor.3:9)
Mungu asipoijenga nyumba,*
waijengao wanajisumbua bure.
Mungu asipoulinda mji,*
waulindao wanakesha bure.
Mnaamka mapema asubuhi na kuchelewa kulala usiku,/
mkihangaika na kutoka jasho kupata chakula chenu*
Kwa nini mnajihangaisha hivyo?
Kama mnampenda Mungu*
atawajalieni yote mngali usingizini!
Watoto ni zawadi itokayo kwa Mungu;*
watoto ni tuzo lake kwetu sisi.
Watoto unaowapata ukiwa kijana,*
ni kama mishale mikononi mwa askari.
Heri mtu aliye na mishale hiyo kwa wingi.*
Hatashindwa akutanapo na adui mahakamani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Tuwe tunaishi au tuwe tunakufa, tu mali ya Bwana, aleluya.
ANT. III: Vyote vilivyopo vimetoka kwake na kwa njia yake, na vimo
ndani yake: utukufu uwe kwake milele, aleluya.
WIMBO: Kol.1:12-20 Kristo ni mzaliwa wa kwanza wa viumbevyote,
ni mzaliwa wa kwanza kutoka wafu.
Mshukuruni Baba*
aliyewawezesha ninyi kuwa na sehemu yenu
katika mambo yale/
Mungu aliyowawekea watu wake*
katika Utawala wa mwanga.
Yeye alituokoa kutoka katika nguvu ya giza,/
akatuleta salama*
katika Utawala wa Mwanae mpenzi,
ambaye kwa njia yake tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.
Kristo ni mfano kamili unaoonekana*
wa Mungu asiyeonekana.
Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza,*
mkuu kuliko viumbe vyote.
Maana kwa njia yake/
Mungu aliumba kila kitu*
duniani na mbinguni,
vitu vinavyoonekana na visivyoonekana:/
wenye enzi, watawala,*
wakuu na wenye mamlaka.
Vyote viliumbwa kwa njia yake*
na kwa ajili yake.
Kristo alikuwako kabla ya viumbe vyote/
na kwa kuungana naye,*
kila kitu hudumu mahali pake.
Yeye ni kichwa cha mwili wake,/
yaani kanisa;*
yeye nichanzo cha uhai wa huo mwili.
Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza*
aliyefufuliwa katika wafu,
ili yeye peke yake/
awe na nafasi ya kwanza*
katika vitu vyote.
Maana Mungu mwenyewe aliamua
kwamba Mwana anao ukamilifu wote*
wa kimungu ndani yake.
Basi, kwa njia yake,/
Mungu aliamua*
kuupatanisha ulimwengu wote naye.
Kwa damu ya Kristo msalabani*
Mungu alifanya amani,
na hivyo akavipatanisha naye*
vitu vyote duniani na mbinguni.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. III: Vyote vilivyopo vimetoka kwake na kwa njia yake, na vimo
ndani yake: utukufu uwe kwake milele, aleluya.
SOMO: 1Kor.2:9-10
Mambo ambayo jicho halijapata kuyaona wala sikio kuyasikia, mambo ambayo binadamu hajapata
kuyafikiria moyoni, hayo ndiyo Mungu aliyowatayarishia wale wampendao. Hayo ndiyo mambo Mungu
aliyotufunulia kwa njia ya Roho wake. Maana Roho huchunguza kila kitu hata mambo ya ndani
kabisa ya Mungu.
KIITIKIZANO
K. Roho Mtakatifu ni Msaidizi, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Atawafundisheni kila kitu.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Roho Mtakatifu ni Msaidizi, aleluya, aleluya.
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Kristo atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto, aleluya.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Kristo atawabatizeni kwa Roho Mtakatifu na kwa moto, aleluya.
MAOMBI
Pamoja na mitume na wale wote waliopokea ahadi ya Roho Mtakatifu, tunamsifu na kumwomba Mungu.
W. Bwana, utusikie.
Mungu mwenye nguvu na uwezo, umempaliza juu Kristo, na kumwingiza katika utukufu wa mbinguni;
- uwasaidie watu wote, waone kuwa yeye anaishi katika Kanisa lake. (W.)
Baba, kuhusu Kristo ulisema, 'Huyu ndiye Mwanangu mpenzi, msikilizeni yeye.'
- Uifanye sauti ya Mwanao isikike katika mioyo ya watu, na iwafikishe kwenye wokovu. (W.)
Tunaomba Roho wako Mtakatifu aje kukaa katika mioyo ya waamini wako;
- na aufanye upya uso wa dunia. (W.)
Katika mikono yako twawaweka ndugu zetu marehemu;
- yaimarishe matumaini yetu katika ufufuo ujao. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tuseme kwa pamoja yale maneno aliyotupatia Bwana
yawe kielelezo cha sala zote: Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Mungu mwenye huruma, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, umewakusanya pamoja
waamini wako. Utudumishe katika utumishi wako, na katika umoja wetu. Tunaomba hayo kwa njia
ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima
na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye
uzima wa milele.
(W.) Amina.