Generic placeholder image

JUMATANO JUMA LA 7 PASAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Kristo Bwana ametuahidia Roho Mtakatifu: njooni, tumwabudu, aleluya.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI chagua 1-5(32-36)
1 (32)
Roho Muumbaji njoo kwetu
Ushuke toka juu uliko,
Njoo uzitwae roho zetu,
Zote uzifanye mali yako.

Wewe unaitwa Mfariji,
Thawabu isiyo na kifani,
Ni chemchemi na moto hai,
Ndiwe manukato na upendo.

Mtoaji wa vipaji saba,
Kidole cha kuume cha Mola;
Sisi wadogo watufundisha
Kusema na pia kuelewa.

Uziangaze akili zetu,
Washa upendo mioyo yetu;
Na kwa zako za daima nguvu
Iimarishe miili yetu.

Mfukuzie mbali mwuaji,
Amani ya kweli tuipate;
Na kila janga utuepushe
Kwa zako mbawa utulinde.

Kumjua Baba tujalie
Na huyo wa milele Mwanae,
Wewe Roho pia tukujue,
Watatu nyie Mungu Mmoja.

Baba utukufu wote kwako,
Na kwa Mwanao mlio sawa,
Pia kwa Mfariji Mkuu:
Ninyi mtukuzwe bila mwisho.


2 (33) Njoo, Ewe Muumbaji,
Njoo, Roho mtukufu,
Uje ujipumzishe
Rohoni mwetu karibu;
Uje na neema zako
Na misaada ya mbingu,
Ili tele kuijaza
Mioyo uloiumba.

E Mfariji Mkuu,
Tunakulilia Bwana,
Ewe karama kamambe
'Toka kwa Mungu Mkuu,
Chemchemi ya Uzima,
Ewe Moto wa Upendo,
Na mafuta ya kupaka -
Mazuri kutoka juu!

Wewe unajulikana
Kwa mapaji yako saba;
U kidole, tunakiri,
Cha mkono wake Mungu;
Wewe pia ni ahadi
Ya Baba Mwenyezi Mungu,
Ulimi waujalia
Uwezo wa kuongea.

Viwashe vyetu vionjo
Kutoka juu uliko,
Na zifanye zetu nyoyo
Zifurike kwa upendo;
Twondolee udhaifu
Wa hii miili yetu,
Saburi utugawie
Nazo fadhila kamambe.

Fukuzia mbali nasi
Adui tumwogopaye,
Na badala yake tupe
Amani yako ya kweli;
Wewe ukituongoza
Nasi tukikufuata,
Basi hatutaiacha
Njia ile ya uzima.

Twaomba yako neema
Itujalie, twaomba,
Kumjua yeye Baba,
Mwanae na Wewe pia,
Ambaye kila wakati
Bila mwisho tunakiri
U Roho wa Baba, Mwana,
Roho wao wa milele.

Utukufu wote wote,
Tena kwa nyakati zote,
Kwake yeye Mungu Baba
Na pia kwa wake Mwana,
Mfufuka 'toka wafu;
Pia kwako utukufu,
E Roho Mtakatifu,
Kwa milele mtukufu.

3 (34)
Ewe Roho wa Mungu Mwenyezi,
Juu ya nchi tupu gizani
Kwa uwezo mwingi uliruka
Ulimwengu ulipoumbika;

Mambo mazuri ukatengeza
Kwa ule udongo na vurugu,
Uzima wa Mungu livuvia
Katika pua yake adamu;

Njoo ili upande uhai
Katika nafsi zetu duni,
Sali ndani yetu, utuunde
Tuwe wana ndani yake Mwana.

Ee Roho uliye muweza,
Nyoyo zetu kwako elekeza,
Utuingize katika uzima
Ndani ya Utatu, Mungu 'Moja.
Stanbrook Abbey Hymnal

4 (35)
Shuka chini, Upendo wa Kimungu,
Uitafute hii roho yangu,
Na itembelee kwa ari yako,
Kwa ari yako hiyo iwakayo;
E Mfariji sogea karibu,
Jitokeze ndani ya moyo wangu,
Na uuwashe na kuupatia
Mwako wako mtakatifu sana.

Uuache uwake peke yake,
Mpaka tamaa za kidunia
Zitapoungua kwa joto lake
Na kuwa vumbi na majivu hasa;
Nayo hiyo nuru yako tukufu
Na iniangazie macho yangu,
Na inifunike mimi kabisa
Wakati yanimulikia njia.

Unipe upendo mtakatifu
Ili uwe vazi langu la nje,
Unipatie na unyenyekevu
Ili uwe vazi langu la ndani:
Unyenyekevu halisi wa moyo,
Ambao hutwaa yaliyo duni,
Na ambao hulia kwa uchungu
Juu ya kasoro zake wenyewe.

Na hivi ile tamaa ya roho,
Hamu kubwa isiyo na kipimo,
Wanadamu watashindwa kabisa
Kuieleza na kusimulia;
Maana hakuna anayeweza,
Kukisia hasa yake neema
Mpaka mwenyewe awe makao,
Makao ya Mtakatifu Roho.
Bianco da Siena +1434

5 (36)
Pendo la Baba na la Mungu Mwana,
Pendo ulo chanzo cha vitu vyote,
Ulotengeza uzuri wa mbingu,
Lengo na uhai wa ulimwengu.

Ewe Mwenyezi na Mtakatifu,
Amani na haki watuletea,
Viumbe kwa wema wavitendea,
Na waviepusha na kila ovu.
Usafi, cheo, hekima, haki,
Ukweli: vyote unavyo kamili;
Kwa njia ya Kristo mwenyewe,
Watutenga na mambo ya dunia.

Watu wote wakuabudu wewe,
Uliye mtukufu kwa milele
Tufariji sisi viumbe wako,
Jalia tufaidi mwanga wako.
Robert Bridges 1844-1930

ANT. I: Mataifa yote yatakuja kukusujudia, Ee Bwana, aleluya.

Zab.86 Kuomba msaada
Atukuzwe Mungu... mwenye kuleta faraja yote. Yeye hutufariji sisi katika taabu zetu zote (2Kor.1:3-4)

Unisikilize, Ee Mungu, unitegee sikio,*
maana mimi ni fukara na mnyonge.

Uilinde roho yangu, maana mimi ni mchaji wako;*
uniokoe mimi mtumishi wako, ninayekutegemea.

Wewe ni Mungu wangu; basi, unionee huruma.*
Mimi ninakulilia mchana kutwa.

Unifurahishe mimi mtumishi wako, Ee Mungu,*
maana sala zangu nazielekeza kwako.

Wewe, Ee Bwana, u mwema na mwenye huruma;*
umejaa upendo mkuu kwa wote wanaokuomba.

Usikie, Ee Mungu, sala yangu;*
uangalie kilio cha ombi langu.

Siku za taabu nakuita,*
maana wewe wanisikiliza.

Ee Bwana, hakuna Mungu aliye kama wewe;*
hakuna awezaye kufanya unayofanya wewe.

Mataifa yote uliyoyaumba yatakuja na kukuabudu;*
yatatangaza ukuu wa jina lako.

Wewe ni mwenye enzi kuu, wafanya miujiza;*
wewe ndiwe Mungu peke yako.

Unifundishe, Ee Mungu, mwongozo wako,/
nami nitaufuata kwa uaminifu;*
uongoze moyo wangu nikuheshimu.

Nitakusifu, Ee Bwana, Mungu wangu, kwa moyo wote;*
nitatangaza ukuu wa jina lako hata milele.

Upendo wako ni mkuu mno!*
Umeniokoa kutoka chini kuzimu.

Ee Mungu, wenye kiburi wamenikabili;/
kundi la watu wakatili wanataka kuniua,*
watu ambao hawakujali wewe hata kidogo.

Lakini wewe Bwana, ni Mungu wa huruma na mapendo;*
wewe ni mvumilivu, mpole na mwaminifu.

Unigeukie, unihurumie;/
unijalie nguvu yako, unisalimishe,*
mimi niliye mtumishi wako kama mama yangu.

Unioneshe ishara ya wema wako, Ee Mungu,/
ili wale wanaonichukia waaibike,*
wakiona wewe umenisaidia na kunifariji.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Mataifa yote yatakuja kukusujudia, Ee Bwana, aleluya.

ANT. II: Macho yetu yatamwona mfalme katika utukufu wake, aleluya.

WIMBO: Isa.33:13-16 Mungu atatawala kwa haki
Ahadi ile ilikuwa kwa ajili yenu, kwa ajili ya watoto wenu, kwa ajili ya wote wanaokaa mbali, na kwa ajili ya wowote wale ambao Bwana Mungu wetu atawaita kwake. (Mate.2:39)

Sikieni ninyi mlio mbali, niliyoyatenda;/.
na ninyi mlio karibu,*
kirini uweza wangu.

Wenye dhambi walio katika Sion wanaogopa;*
tetemeko limewashika wasiomcha Mungu;

Ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto ulao;*
ni nani kwetu sisi awezaye kukaa na moto uteketezao milele?

Ni yeye aendaye kwa haki,*
anenaye maneno ya adili;

ni yeye anayedharau faida*
ipatikanayo kwa dhuluma;

akung'utaye mikono yake*
asipokee rushwa;

azibaye masikio yake*
asisikie habari za damu;

afumbaye macho yake*
asitazame uovu.

Huyu ndiye atakayekaa juu;*
majabali ni ngome yake;

atapewa chakula chake;*
maji yake hayatakoma.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Macho yetu yatamwona mfalme katika utukufu wake, aleluya.

ANT. III: Watu wote watauona wokovu wa Mungu wetu, aleluya.

Zab.98 Mungu mtawala dunia yote
Zaburi hii yaeleza ujio wa kwanza wa Bwana, na imani ya mataifa yote (Mt. Athanasius)

Mwimbieni Mungu, wimbo mpya,*
kwa maana ametenda mambo ya ajabu!

Kwa nguvu na enzi yake takatifu*
amejipatia ushindi.

Mungu ameonesha ushindi wake;*
ameyadhihirishia mataifa uwezo wake wa kuokoa.

Ameshika ahadi aliyowapa watu wa Israeli,*
kwa upendo mkuu na uaminifu kwao.

Pande zote za dunia*
zimeuona ushindi wa Mungu wetu.

Dunia yote imshangilie Mungu;*
imsifu kwa nyimbo na vigelegele.

Msifuni Mungu kwa shangwe,*
kwa sauti za kinubi na zeze.

Mpigieni vigelegele Mungu mfalme wetu,*
mshangilieni kwa tarumbeta na sauti ya baragumu.

Bahari ivume na vyote vilivyomo;*
dunia na wote waishio ndani yake.

Enyi mito, pigeni makofi;*
enyi vilima, imbeni pamoja kwa shangwe.

Shangilieni mbele ya Mungu,*
maana anakuja kutawala dunia.

Atauhukumu ulimwengu kwa haki,*
na watu atawatawala kwa uadilifu.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. III: Watu wote watauona wokovu wa Mungu wetu, aleluya.

SOMO: Rom.6:8-11
Basi, ikiwa tumekufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba tutaishi pia pamoja naye. Maana, tunajua kwamba Kristo amekwisha fufuliwa katika wafu; hafi tena, kifo hakimtawali tena. Hivyo kwa kuwa alikufa mara moja tu dhambi haina tena nguvu juu yake; na sasa anaishi maisha yake katika umoja na Mungu. Hali kadhalika, nanyi lazima mjione kuwa mmekufa kuhusu dhambi, lakini kama mnaoishi katika umoja na Mungu kwa njia ya Kristo Yesu.

KIITIKIZANO
K. Bwana amefufuka kutoka wafu, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Kwa ajili yetu alikufa msalabani.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Tumshukuru Mungu, aliyetupatia ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote *
na milele. Amina

Ant. Tumshukuru Mungu, aliyetupatia ushindi kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, aleluya.

MAOMBI
Roho Mtakatifu anaungana na roho zetu katika kushuhudia kuwa sisi ni watoto wa Mungu. Na tutoe shukrani kwa Baba yetu wa mbinguni.
W. Baba, uwasikie watoto wako.

Mungu mwenye uvumilivu na mwenye kutia moyo, utujalie tuweze kuafikiana wenyewe kwa wenyewe, kwa kufuata mfano wa Kristo;
- tukiwa tumeungana kwa nia na sauti, utuwezeshe kukutukuza. (W.)

Umjalie kila mmoja wetu aweze kufikiria mahitaji ya mwenzake, na ajitahidi kumridhisha;
- utuwezeshe kuimarisha imani za wenzetu. (W.)

Usiruhusu tupotoshwe na nguvu ya yule Mwovu,
- bali utujaze Roho atokaye kwako. (W.)

Bwana, wewe wajua kila kilicho ndani ya mioyo yetu;
- utuongoze katika njia za unyofu na ukweli. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu mwenye huruma, kwa nguvu ya Roho Mtakatifu, umewakusanya pamoja waamini wako. Utudumishe katika utumishi wako, na katika umoja wetu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe pamoja na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.