Generic placeholder image

JUMATANO JUMA LA 6 PASAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Bwana amefufuka kweli, aleluya.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI chagua 1-7
1 (25)
Kristo Bwana amefufuka!
Kila mnyororo Bwana kakata,
Sikilizeni, hao malaika
Makelele kwa shangwe wanapiga,
Milele mbinguni juu waimba,
Aleluya!

Aliyekufa kwa ajili yetu,
Na mateso mengi kuvumilia -
Kuvumilia kwa ajili yetu,
Ni Kondoo wetu wa Paska leo!
Nasi pia kwa shangwe tunaimba.
Aleluya!

Yeye aliyepata maumivu
Na hasara yote msalabani,
Sasa yupo katika utukufu,
Akitwombea, huko mbinguni,
Na anasikia kilio chetu.
Aleluya!

Sasa atuagiza tutangaze
Pote pote ulimwenguni jinsi
Ya kuokoka waliopotea,
Na ya kusamehewa wenye toba,
Na tuwezavyo ingia mbinguni.
Aleluya!
Mikaeli Weisse yapata 1480-1534

2 (26)
Aleluya! Aleluya!
Angani inatanda Pasaka!
Yesu ni mzima, hafi tena!
Giza limetokomezwa lote,
Na Bwana wa nuru Mfufuka!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Mama Maria mwone Mwanao,
Anavyofurahi kwa ushindi!
Mateso mlishiriki nyote,
Milele mtatawala nyote!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Watafuta waliopotea!
Naye Petro anakulilia!
Mwimarishe awe mwamba,
Kundi lako alichunge!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Mzima haishi kaburini,
Kristo yupo ghorofani!
Utukufu wake kauficha,
Mwili wake hai aonesha!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Japo uso wake hatuoni,
Yupo na sisi kama mwanzoni!
Ni padre wetu mtukufu,
Twashangilia mtu mzima!
Aleluya! Aleluya!
Yakobo Quinn SJ

3 (27)
Aleluya, mwimbieni Yesu,
Enzi na ufalme ni vyake.
Aleluya, fanaka ni yake,
Ushindi ni wake peke yake.
Sikizeni, nyimbo za Sion
Zinanguruma kama tufani,
Zinasikika kama gharika:
Kwa damu yake ilo azizi,
Yesu ametukomboa sisi,
Watu kutoka kila taifa.

Aleluya, katika huzuni
Kama yatima hatujaachwa;
Aleluya, yu karibu nasi,
Imani yasadiki kabisa,
Haiulizi kwa jinsi gani
Ingawa Bwana alitoweka,
Akafunikwa nayo mawingu
Siku ile ya arobaini,
Tutasahau ahadi yake:
'Nipo nanyi daima milele'?
S. S. Wesley 1810-1876

4 (28)
Kwenye Karamu ya Mwana-Kondoo
Mfalme mshindi twamwimbia,
Alotuosha kwa wingi wa maji
Kutoka penye tobo ubavuni.

Yeye analo pendo la kimungu
Waalikwa wanyweshwa damu yake,
Na awapa waule mwili wake
Pendo ndilo kafara na kuhani.

Panapomwagwa damu ya Pasaka
Mwuaji upanga aufutika;
Jeshi la Israeli lapita
Askari adui wafa maji.

Kristo kondoo aliyechinjwa,
Kafara na mkate wa Pasaka;
Tuile manna itokayo juu
Kwa unyofu na upendo halisi.

Kafara shujaa kutoka juu,
Nguvu za kuzimu ni chini yako;
Vitani mauti umeyashinda,
Uzima na mwanga kutuletea.

Bendera sasa waipeperusha,
Shetani na kaburi watiisha;
Malaika waungana kusifu
Kupinduliwa kwa bwana shetani.

Ushindi na furaha ya Pasaka
Dhambi tu ndo yaweza viharibu;
Tukinge na kifo cha dhambi Bwana,
Tulozaliwa upya ndani yako.

Tenzi za fahari, nyimbo za sifa
Tunakuimbia mpenzi Baba;
Na sifa zote milele mpate,
Bwana Mfufuka na wewe Roho.
Karne ya 7

5 (29)
Utangazeni ushindi wake,
Ewe mbingu na wewe dunia,
Maana Kristo amefufuka
Kama mwenyewe alivyosema:
Ndie yule alosulibiwa,
Ni Mungu kweli aliye hai,
Aliyekaa kwa siku tatu
Kati ya wafu huko kuzimu.

Kristo alikufa kwa aibu
Kwa ajili yetu sisi watu,
Lakini sasa aishi tena
Akiwa na nguvu na uweza;
Moto wake na haujazimwa,
Mwali wake unaoangaza
Ulimwengu wote waujaza
Kwa furaha tele na mwangaza.

Sifa na heshima kwake Baba
Ambaye hakika Hakuumbwa,
Na kwa Mwanae aliye hai
Ambaye hakika hakushindwa,
Bali anatawala kwa enzi
Pamoja na Roho wake Mungu,
Utatu ulio Mtukufu,
Katika yeye Mungu Mmoja.
Stanbrook Abbey Hymnal

6 (30)
Njoni, enyi waamini, njoni,
Mkashangilie kwa furaha;
Mungu kawapa Israeli
Furaha baada ya huzuni;
Wana na binti zake Yakobo
Si watumwa tena wa Farao;
Kawavusha miguu mikavu
Katikati ya Bahari ya Shamu.

Leo ndio roho zachipua;
Kristo jela kabomoa,
Japo siku tatu kawa mfu
Leo kachomoza kama jua;
Kipupwe chote cha dhambi zetu,
Cha muda mrefu na cha kiza,
Metokomezwa kwa yako nuru
Wewe tukusifuye daima.

Milango imara ya mauti,
Wala kaburi pana la giza,
Wala walinzi, wala muhuri,
Havikushiki uwe maiti
Maana leo ulisimama.
Kati yao Kumi na Wawili,
Amani yako ukawapatia
Ipitayo ufahamu wetu.
Mt. Yohane wa Damasko yapata 750

7 (31)
Hakika vita sasa vimekwisha,
Majeshi ya motoni yakimbia;
Tupige ukelele wa ushindi
Kwa furaha na shangwe, aleluya.

Kristo aliyeuvumilia
Ule mti utiao aibu,
Twamkaribisha tukimsifu
Aloshinda mauti, aleluya.

Asubuhi ya tatu kafufuka,
Amevishwa nuru ya utukufu.
Ambayo wenye imani thabiti
Mbinguni watavishwa, aleluya.

Ile milango duni ya kuzimu
Ufunguo wao yaachilia,
Mlango wa Paradisi u wazi;
Tusichoke kuimba, aleluya.

Bwana, kwa mapigo tulokupiga,
Tujalie tuwe mbali na kifo,
Ili tuendelee kukariri
Salamu yetu hii, aleluya.
Simphonia Sirenum 1695

ANT. I: Yale maji yalikuona, Ee Mungu; uliwavusha watu wako baharini, aleluya.

Zab.77 Faraja wakati wa shida
Daima twapata taabu, lakini hatugandamizwi; twapata mashaka, lakini hatukati tamaa (2Kor.4:8)

Kwa sauti namlilia Mungu,*
namlilia naye ananisikiliza.

Wakati wa taabu namwomba Bwana;/
nanyosha mikono yangu usiku kucha kuomba,*
lakini sipati kitulizo chochote.

Ninapomfikiria Mungu, nasononeka;*
ninapotafakari, nafa moyo.

Ananizuia hata kupata lepe la usingizi,*
nina mahangaiko hata kusema siwezi.

Nafikiria siku za zamani;*
nakumbuka miaka iliyopita.

Usiku kucha nafikirifikiri;*
nawaza na kujiuliza hivi:

“Je, Bwana ametuacha kabisa?*
Je, hatanifanyia tena hisani yake?

Na upendo wake mkuu je, umekwisha?*
Hatatimiza tena ahadi zake?

Je, Mungu amesahau kuwa na huruma?*
Je, hasira yake imeuondoa upole wake?“

Halafu nikasema: “Kinachonichoma zaidi,*
ni kwamba Mungu hana nguvu tena!"

Lakini, Ee Mungu, nitayakumbuka matendo yako;*
nitayafikiria maajabu yako ya hapo kale.

Nitatafakari juu ya kazi zako,*
na kuwazia matendo yako makuu.

Ee Mungu, kila ufanyacho ni kitakatifu.*
Hakuna mungu aliye mkuu kama wewe.

Wewe ni Mungu unayetenda maajabu;*
umeyaonesha mataifa enzi yako.

Kwa mkono wako uliwakomboa watu wako;*
naam, wazaliwa wa Yakobo na Yosefu.

Maji yalipokuona, Ee Mungu, yaliogopa mno;*
bahari ilitetemeka hata vilindini.

Mawingu yalichuruzika maji, ngurumo zikavuma,*
na mishale ya umeme ikaangaza kila upande.

Kishindo cha ngurumo yako kilitokea,/
umeme wake ukaangaza ulimwengu;*
dunia ikatikisika na kutetemeka.

Wewe ulitembea juu ya mawimbi;/
ulivuka bahari ile kuu,*
lakini nyayo zako hazikuonekana.

Uliwaongoza watu wako kama kondoo,*
chini ya uongozi wa Musa na Aroni.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Yale maji yalikuona, Ee Mungu; uliwavusha watu wako baharini, aleluya.

ANT. II: Bwana huua, naye hufanya kuwa hai, aleluya.

WIMBO: 1Sam.2:1-10 Maskini hufurahi katika Bwana
Amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi, akawakweza wanyenyekevu. Wenye njaa amewashibisha mema (Lk.1:52-53)

Moyo wangu wamshangilia BWANA,*
Pembe yangu imetukuka katika BWANA,

Kinywa changu kimepanuka juu ya adui zangu;*
Kwa kuwa naufurahia wokovu wako;

Hakuna aliye mtakatifu kama BWANA;/
Kwa maana hakuna ye yote ila wewe,*
Wala hakuna mwamba kama Mungu wetu.

Msizidi kunena kwa kutakabari hivyo;*
Majivuno yasitoke vinywani mwenu;

Kwa kuwa BWANA ni Mungu wa maarifa,*
Na matendo hupimwa na yeye kwa mizani.

Pinde zao mashujaa zimevunjika,*
Na hao waliojikwaa wamefungiwa nguvu.

Walioshiba wamejikodisha ili kupata chakula,*
Na hao waliokuwa na njaa wamepata raha.

Naam, huyo aliyekuwa tasa amezaa watoto saba,*
Na yeye aliye na wana wengi amedhoofika.

BWANA huua, naye hufanya kuwa hai;*
Hushusha hata kuzimu, tena huleta juu.

BWANA hufukarisha mtu, naye hutajirisha;*
Hushusha chini, tena huinua juu.

Humwinua mnyonge kutoka mavumbini,*
Humpandisha mhitaji kutoka jaani,

Ili awaketishe pamoja na wakuu,*
Wakakirithi kiti cha enzi cha utukufu;

Kwa maana nguzo za dunia zina BWANA,*
Naye ameuweka ulimwengu juu yake.

Yeye atailinda miguu ya watakatifu wake;*
Bali waovu watanyamazishwa gizani,

Maana kwa nguvu hakuna atakayeshinda;*
Washindanao na BWANA watapondwa kabisa.

Toka mbinguni yeye atawapigia radi;*
BWANA ataihukumu miisho ya dunia;

Naye atampa mfalme wake nguvu,*
Na kuitukuza pembe ya masihi wake.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana huua, naye hufanya kuwa hai, aleluya.

ANT. III: Nuru imewaangazia waadilifu, na heri imewajia wanyofu wa moyo, aleluya.

Zab.97 Mungu mtawala mkuu
Zaburi hii yaeleza ukombozi wa dunia na imani ambayo watu wote wangekuwanayo katika Kristo (Mt. Athanasius)

Mungu anatawala!/
Furahi, ee dunia*
Furahini, enyi visiwa!

Mawingu na giza nene vya mzunguka;*
anatawala kwa adili na haki.

Moto watangulia mbele yake,*
na kuwateketeza adui zake pande zote.

Umeme wake wauangaza ulimwengu;*
dunia yauona na kutetemeka.

Vilima vyayeyuka kama nta mbele ya Mungu;*
naam, mbele ya Bwana wa dunia yote.

Mbingu zatangaza uadilifu wake;*
na mataifa yote yauona utukufu wake.

Wote wanaoabudu sanamu wanaaibishwa,/
naam, wote wanaojisifia miungu duni;*
miungu yote husujudu mbele yako.

Watu wa Sion wanafurahi;/
miji ya Yuda inashangilia,*
kwa sababu ya hukumu zako, Ee Mungu.

Wewe Mungu watukuka juu ya dunia yote;*
wewe ni mkuu mno kuliko miungu yote.

Mungu huwapenda wenye kuchukia uovu,/
huyalinda maisha ya waaminifu wake;*
huwaokoa katika makucha ya waovu.

Mwanga humwangazia mtu mwadilifu,*
na furaha kwa watu wema.

Enyi waadilifu furahieni aliyotenda Mungu!*
Kumbukeni utukufu wake na kumshukuru!

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Nuru imewaangazia waadilifu, na heri imewajia wanyofu wa moyo, aleluya.

SOMO: Rom.6:8-11
Basi, ikiwa tumekufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba tutaishi pia pamoja naye. Maana, tunajua kwamba Kristo amekwisha fufuliwa katika wafu; hafi tena, kifo hakimtawali tena. Hivyo kwa kuwa alikufa mara moja tu dhambi haina tena nguvu juu yake; na sasa anaishi maisha yake katika umoja na Mungu. Hali kadhalika, nanyi lazima mjione kuwa mmekufa kuhusu dhambi, lakini kama mnaoishi katika umoja na Mungu kwa njia ya Kristo Yesu.

KIITIKIZANO
K. Bwana amefufuka kutoka wafu, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Kwa ajili yetu alikufa msalabani.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili. Lakini atakapokuja huyo Roho wa kweli, atawaongozeni kwenye ukweli wote, aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote *
na milele. Amina

Ant. Ninayo bado mengi ya kuwaambieni, ila kwa sasa hamwezi kuyastahimili. Lakini atakapokuja huyo Roho wa kweli, atawaongozeni kwenye ukweli wote, aleluya.

MAOMBI
Tumwombe Mungu, aliyewadhihirishia mitume utukufu wa Kristo Mfufuka.
W. Ututukuze, Bwana, kwa utukufu wa Kristo.

Baba, tunakutukuza leo kwa mioyo yenye shukrani, kwa sababu umetuingiza katika mwanga wako wa ajabu;
- utusaidie daima tuweze kuona wema na upendo wako. (W.)

Kwa njia ya Roho Mtakatifu, uwaimarishe na kuwatakasa, watu;
- uwapatie moyo mpya katika harakati zao za kuinua hali ya maisha. (W.)

Na tuyatumie maisha yetu katika kuwahudumia watu:
- uzibariki juhudi zetu, ili ubinadamu wote upate kuwa sadaka inayokubalika kwako. (W.)

Asubuhi hii uijaze mioyo yetu upendo wako;
- ujalie, kusifu utukufu wako kuwe furaha ya maisha yetu. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu na Baba, tunaiheshimu sikukuu ya kila mwaka ya ufufuko wa Mwanao kwa kuiadhimisha katika fumbo. Utupatie pia neema ya kufurahi pamoja na watakatifu wote hapo Mwanao atakapokuja katika utukufu. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.