JUMATANO JUMA LA 5 PASAKA
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
E Bwana Mbarikiwa,
Mungu Muumbaji wetu,
Vitu vyote hutakaswa
Katika Wewe, E Mungu,
Wewe waviimarisha
Hata milele vidumu.
Wenye heri, e mkono
Mtakatifu wa Mungu,
Ndiwe watakatifuza
Vitu vyote, vyote vitu,
Na upya unavitia
Wavipamba vyasitawi.
Ewe fahari tukufu,
Enzi yake Bwana Mungu,
Ndani mwako wachukua
Vyote unavyovijaza;
Na yote yanafanyika
Kadiri unavyotaka.
Usifiwe, utukuzwe
Utatu Mtakatifu,
Ujuaye kwa hakika
Na makini zako njia;
Wewe ndiwe nuru kuu
Milele inayodumu.
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya
Zab.119:9-16 II Uaminifu kwa Sheria ya Mungu
Kijana atatunzaje mwenendo wake uwe safi?*
Kwa kuyashika maagizo yako.
Najitahidi kukutii kwa moyo wote;*
unijalie kuzishika amri zako.
Nimeshika agizo lako moyoni mwangu,*
nisije nikakukosea.
Utukuzwe, Ee Mungu!*
Unifundishe kanuni zako.
Nitazirudia kwa sauti*
sheria zako zote ulizotoa.
Nafurahi kufuata amri zako,*
kuliko kuwa na utajiri mwingi.
Nazitafakari amri zako,*
na kuyazingatia maagizo yako.
Nazifurahia kanuni zako;*
sitazisahau amri zako.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.17 Sala ya mtu mwema
Yesu alipokuwa anaishi hapa duniani, kwa kilio kikuu na machozi, alisali na kumwomba
Mungu ambaye alikuwa na uwezo wa kumwokoa kutoka kifo; naye akasikilizwa (Ebr.5:7)
I
Ee Mungu, unisikilize niombapo haki zangu;/
usikilize kilio changu,*
upokee ombi langu la moyo mnyofu.
Utatoa hukumu ya kunifadhili,*
kwani wewe wajua jambo la haki.
Wewe waujua kabisa moyo wangu;/
umenijia usiku, umenichunguza;*
hukuona uovu wowote ndani yangu.
Sisemi maovu, kama wafanyavyo wengine;*
nimeitii amri yako, sikuishika njia ya wadhalimu.
Nimefuata daima njia yako;*
wala sikuiacha kamwe.
Nakuita, Ee Mungu, kwani wanisikiliza;*
unitegee sikio, uyasikilize maneno yangu.
Onyesha upendo wako mkuu,/
uwaokoe kutoka kwa adui zao,*
wale wanaokukimbilia.
Unilinde kama mboni ya jicho lako;/
unifiche kivulini mwa mabawa yako,*
mbali na mashambulio ya waovu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
II
Adui wa hatari wanizunguka,/
hawana huruma yoyote ile;*
wamejaa maneno ya kujigamba.
Sasa wamenizingira pande zote;*
wanavizia waniangushe chini.
Wako tayari kunirarua kama simba;*
kama aviziavyo mawindo mwana-simba.
Uje, Ee Mungu, kuwakabili na kuwaporomosha.*
Kwa upanga wako uniokoe na watu waovu;
kwa mkono wako, Ee Mungu, uniokoe na watu hao,*
watu ambao huthamini riziki ya dunia hii tu.
Waadhibu kwa mateso uliyowawekea,/
yawe ya kutosha kwa watoto wao,*
wawaachie na wajukuu wao.
Lakini mimi nitakuona, kwani sikutenda ubaya;*
niamkapo nitajaa furaha kwa kukuona.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: Rom.4:24-25
Sisi tunamwamini Mungu aliyemfufua Yesu, Bwana wetu, katika wafu. Yeye alitolewa auawe kwa
ajili ya dhambi zetu, akafufuliwa ili tupate uhusiano mwema na Mungu.
K. Bwana amefufuka kweli, aleluya.
W. Amemtokea Simoni, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: 1Yoh.5:5-6a
Nani basi, awezaye kuushinda ulimwengu? Ni yule anayeamini kwamba Yesu ni Mwana wa Mungu.
Yesu Kristo ndiye aliyekuja kwa maji ya ubatizo wake na kwa damu ya kifo chake.
K. Wanafunzi walifurahi, aleluya.
W. Walipomwona Bwana, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: Ef.4:23-24
Jirekebisheni upya rohoni na katika fikra zenu. Vaeni hali mpya ya utu ambayo imeumbwa kwa
mfano wa Mungu, na ambayo hujionesha katika maisha ya kweli ya uadilifu na utakatifu.
K. Kaa nasi, Bwana, aleluya.
W. Maana usiku unakaribia, aleluya.
SALA:
Tuombe: Bwana Mungu wetu, waupenda moyo usio na hatia, tunapotenda dhambi wewe wafuta makosa
yetu. Uiongoze kwako mioyo ya watu wakuchao, ili baada ya kuondolewa upofu wa utovu wa imani,
kamwe wasiachane na mwanga wa ukweli wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Yesu Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.