JUMATANO JUMA LA 5 PASAKA
MASIFU YA JIONI
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI chagua 1-7
1 (25)
Kristo Bwana amefufuka!
Kila mnyororo Bwana kakata,
Sikilizeni, hao malaika
Makelele kwa shangwe wanapiga,
Milele mbinguni juu waimba,
Aleluya!
Aliyekufa kwa ajili yetu,
Na mateso mengi kuvumilia -
Kuvumilia kwa ajili yetu,
Ni Kondoo wetu wa Paska leo!
Nasi pia kwa shangwe tunaimba.
Aleluya!
Yeye aliyepata maumivu
Na hasara yote msalabani,
Sasa yupo katika utukufu,
Akitwombea, huko mbinguni,
Na anasikia kilio chetu.
Aleluya!
Sasa atuagiza tutangaze
Pote pote ulimwenguni jinsi
Ya kuokoka waliopotea,
Na ya kusamehewa wenye toba,
Na tuwezavyo ingia mbinguni.
Aleluya!
Mikaeli Weisse yapata 1480-1534
2 (26)
Aleluya! Aleluya!
Angani inatanda Pasaka!
Yesu ni mzima, hafi tena!
Giza limetokomezwa lote,
Na Bwana wa nuru Mfufuka!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Mama Maria mwone Mwanao,
Anavyofurahi kwa ushindi!
Mateso mlishiriki nyote,
Milele mtatawala nyote!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Watafuta waliopotea!
Naye Petro anakulilia!
Mwimarishe awe mwamba,
Kundi lako alichunge!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Mzima haishi kaburini,
Kristo yupo ghorofani!
Utukufu wake kauficha,
Mwili wake hai aonesha!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Japo uso wake hatuoni,
Yupo na sisi kama mwanzoni!
Ni padre wetu mtukufu,
Twashangilia mtu mzima!
Aleluya! Aleluya!
Yakobo Quinn SJ
3 (27)
Aleluya, mwimbieni Yesu,
Enzi na ufalme ni vyake.
Aleluya, fanaka ni yake,
Ushindi ni wake peke yake.
Sikizeni, nyimbo za Sion
Zinanguruma kama tufani,
Zinasikika kama gharika:
Kwa damu yake ilo azizi,
Yesu ametukomboa sisi,
Watu kutoka kila taifa.
Aleluya, katika huzuni
Kama yatima hatujaachwa;
Aleluya, yu karibu nasi,
Imani yasadiki kabisa,
Haiulizi kwa jinsi gani
Ingawa Bwana alitoweka,
Akafunikwa nayo mawingu
Siku ile ya arobaini,
Tutasahau ahadi yake:
'Nipo nanyi daima milele'?
S. S. Wesley 1810-1876
4 (28)
Kwenye Karamu ya Mwana-Kondoo
Mfalme mshindi twamwimbia,
Alotuosha kwa wingi wa maji
Kutoka penye tobo ubavuni.
Yeye analo pendo la kimungu
Waalikwa wanyweshwa damu yake,
Na awapa waule mwili wake
Pendo ndilo kafara na kuhani.
Panapomwagwa damu ya Pasaka
Mwuaji upanga aufutika;
Jeshi la Israeli lapita
Askari adui wafa maji.
Kristo kondoo aliyechinjwa,
Kafara na mkate wa Pasaka;
Tuile manna itokayo juu
Kwa unyofu na upendo halisi.
Kafara shujaa kutoka juu,
Nguvu za kuzimu ni chini yako;
Vitani mauti umeyashinda,
Uzima na mwanga kutuletea.
Bendera sasa waipeperusha,
Shetani na kaburi watiisha;
Malaika waungana kusifu
Kupinduliwa kwa bwana shetani.
Ushindi na furaha ya Pasaka
Dhambi tu ndo yaweza viharibu;
Tukinge na kifo cha dhambi Bwana,
Tulozaliwa upya ndani yako.
Tenzi za fahari, nyimbo za sifa
Tunakuimbia mpenzi Baba;
Na sifa zote milele mpate,
Bwana Mfufuka na wewe Roho.
Karne ya 7
5 (29)
Utangazeni ushindi wake,
Ewe mbingu na wewe dunia,
Maana Kristo amefufuka
Kama mwenyewe alivyosema:
Ndie yule alosulibiwa,
Ni Mungu kweli aliye hai,
Aliyekaa kwa siku tatu
Kati ya wafu huko kuzimu.
Kristo alikufa kwa aibu
Kwa ajili yetu sisi watu,
Lakini sasa aishi tena
Akiwa na nguvu na uweza;
Moto wake na haujazimwa,
Mwali wake unaoangaza
Ulimwengu wote waujaza
Kwa furaha tele na mwangaza.
Sifa na heshima kwake Baba
Ambaye hakika Hakuumbwa,
Na kwa Mwanae aliye hai
Ambaye hakika hakushindwa,
Bali anatawala kwa enzi
Pamoja na Roho wake Mungu,
Utatu ulio Mtukufu,
Katika yeye Mungu Mmoja.
Stanbrook Abbey Hymnal
6 (30)
Njoni, enyi waamini, njoni,
Mkashangilie kwa furaha;
Mungu kawapa Israeli
Furaha baada ya huzuni;
Wana na binti zake Yakobo
Si watumwa tena wa Farao;
Kawavusha miguu mikavu
Katikati ya Bahari ya Shamu.
Leo ndio roho zachipua;
Kristo jela kabomoa,
Japo siku tatu kawa mfu
Leo kachomoza kama jua;
Kipupwe chote cha dhambi zetu,
Cha muda mrefu na cha kiza,
Metokomezwa kwa yako nuru
Wewe tukusifuye daima.
Milango imara ya mauti,
Wala kaburi pana la giza,
Wala walinzi, wala muhuri,
Havikushiki uwe maiti
Maana leo ulisimama.
Kati yao Kumi na Wawili,
Amani yako ukawapatia
Ipitayo ufahamu wetu.
Mt. Yohane wa Damasko yapata 750
7 (31)
Hakika vita sasa vimekwisha,
Majeshi ya motoni yakimbia;
Tupige ukelele wa ushindi
Kwa furaha na shangwe, aleluya.
Kristo aliyeuvumilia
Ule mti utiao aibu,
Twamkaribisha tukimsifu
Aloshinda mauti, aleluya.
Asubuhi ya tatu kafufuka,
Amevishwa nuru ya utukufu.
Ambayo wenye imani thabiti
Mbinguni watavishwa, aleluya.
Ile milango duni ya kuzimu
Ufunguo wao yaachilia,
Mlango wa Paradisi u wazi;
Tusichoke kuimba, aleluya.
Bwana, kwa mapigo tulokupiga,
Tujalie tuwe mbali na kifo,
Ili tuendelee kukariri
Salamu yetu hii, aleluya.
Simphonia Sirenum 1695
ANT. I: Mungu amemtukuza, akamweka mkono wake wa kuume awe kiongozi
na Mwokozi, aleluya.
Zab.27 Kwa Mungu kuna usalama
Tazama! Mungu amefanya makao yake kati ya watu (Ufu.21:3)
I
Mungu ndiye mwanga wangu, na mwokozi wangu,*
nimwogope nani?
Mungu ni mlinzi wa maisha yangu;*
nitamwogopa nani basi?
Watu wabaya wakinivamia na kutaka kuniua,*
wao wenyewe watajikwaa na kuanguka.
Hata kama nikizungukwa na jeshi, sitaogopa;*
hata nikikabiliwa na vita, sitakufa moyo.
Jambo moja nimemwomba Mungu;*
jambo moja tu natafuta:
Nikae nyumbani mwa Mungu,*
siku zote za maisha yangu;
niuone uzuri wake Mungu,*
na kutafuta maongozi yake Hekaluni mwake.
Siku ya taabu atanihifadhi bandani mwake;/
atanificha katika hema yake,*
na kunisalimisha juu ya mwamba.
Nami nitawashinda adui zangu wanaonizunguka;/
nitatolea sadaka kwa shangwe Hekaluni mwake,*
nitaimba na kumshangilia Mungu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. I: Mungu amemtukuza, akamweka mkono wake wa kuume awe kiongozi
na Mwokozi, aleluya.
ANT. II: Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana, katika nchi ya walio
hai, aleluya.
Msaada wapatikana kwa Mungu
Kisha wengine walisimama, wakatoa ushahidi wa uwongo dhidi ya Yesu (Mk.14:57)
II
Usikie, Ee Mungu, ninapokulilia;*
unionee huruma na kunisikiliza.
Nafikiria uliyosema: “Njoo kwangu!"/
Naam, naja kwako; Ee Mungu.*
Usiache kuniangalia kwa wema.
Usinikatae kwa hasira mimi mtumishi wako;/
wewe umekuwa daima msaada wangu.*
Usinitupe wala usiniache, Ee Mungu mwokozi wangu.
Hata kama wazazi wangu wangenitupa,*
Mungu hatakosa kamwe kunitunza.
Ee Mungu, unifundishe njia yako;/
uniongoze katika njia iliyo sawa,*
kwa sababu adui zangu ni wengi.
Usiniache adui wanitende wapendavyo;*
mashahidi wa uwongo wanikabili kwa vitisho.
Naamini nitauona wema wake Mungu,*
katika makao ya walio hai.
Jiaminishe kwake Mungu!/
Piga moyo konde, usikate tamaa!*
Jiaminishe kwake Mungu!
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. II: Naamini ya kuwa nitauona wema wa Bwana, katika nchi ya
walio hai, aleluya.
ANT. III: Vyote vilivyopo vimetoka kwake na kwa njia yake, na vimo
ndani yake: utukufu uwe kwake milele, aleluya.
WIMBO: Kol.1:12-20 Kristo ni mzaliwa wa kwanza wa viumbevyote,
ni mzaliwa wa kwanza kutoka wafu.
Mshukuruni Baba*
aliyewawezesha ninyi kuwa na sehemu yenu
katika mambo yale/
Mungu aliyowawekea watu wake*
katika Utawala wa mwanga.
Yeye alituokoa kutoka katika nguvu ya giza,/
akatuleta salama*
katika Utawala wa Mwanae mpenzi,
ambaye kwa njia yake tunakombolewa,*
yaani dhambi zetu zinaondolewa.
Kristo ni mfano kamili unaoonekana*
wa Mungu asiyeonekana.
Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza,*
mkuu kuliko viumbe vyote.
Maana kwa njia yake/
Mungu aliumba kila kitu*
duniani na mbinguni,
vitu vinavyoonekana na visivyoonekana:/
wenye enzi, watawala,*
wakuu na wenye mamlaka.
Vyote viliumbwa kwa njia yake*
na kwa ajili yake.
Kristo alikuwako kabla ya viumbe vyote/
na kwa kuungana naye,*
kila kitu hudumu mahali pake.
Yeye ni kichwa cha mwili wake,/
yaani kanisa;*
yeye nichanzo cha uhai wa huo mwili.
Yeye ni Mwana mzaliwa wa kwanza*
aliyefufuliwa katika wafu,
ili yeye peke yake/
awe na nafasi ya kwanza*
katika vitu vyote.
Maana Mungu mwenyewe aliamua
kwamba Mwana anao ukamilifu wote*
wa kimungu ndani yake.
Basi, kwa njia yake,/
Mungu aliamua*
kuupatanisha ulimwengu wote naye.
Kwa damu ya Kristo msalabani*
Mungu alifanya amani,
na hivyo akavipatanisha naye*
vitu vyote duniani na mbinguni.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. III: Vyote vilivyopo vimetoka kwake na kwa njia yake, na vimo
ndani yake: utukufu uwe kwake milele, aleluya.
SOMO: Ebr.7:24-27
Yesu si kama wao, yeye anaishi milele; ukuhani wake hauondoki kwake. Hivyo, yeye anaweza daima
kuwaokoa kabisa wote wanaomwendea Mungu kwa njia yake, maana yeye anaishi milele kuwaombea kwa
Mungu. Basi, Yesu ndiye Kuhani Mkuu ambaye anatufaa sana katika mahitaji yetu. Yeye ni
mtakatifu, hana hatia wala dhambi ndani yake; hayumo katika kundi la wenye dhambi, na ameinuliwa
mpaka juu mbinguni. Yeye si kama wale makuhani wengine; hana haja ya kutoa sadaka kila siku
kwanza kwa ajili ya dhambi zake mwenyewe, na kisha kwa ajili ya dhambi za watu. Yeye alitolea
sadaka moja, wakati alipojitoa yeye mwenyewe, na hiyo yatosha kwa nyakati zote.
KIITIKIZANO
K. Wanafunzi walifurahi, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Walipomwona Bwana.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Wanafunzi...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni cho chote mtakacho, nanyi
mtakipata, aleluya.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Mkikaa ndani yangu na maneno yangu yakikaa ndani yenu, ombeni
cho chote mtakacho, nanyi mtakipata, aleluya.
MAOMBI
Tumwombe Kristo, aliyefufuka kutoka wafu, na ambaye ameketi kuume kwa Baba.
W. Kristo unayeishi milele, utusikie.
Bwana, uwakumbuke wale waliowekwa wakfu kwa ajili ya utumishi wako;
- uwawezeshe kuwaonesha watu wako mfano mzuri kwa maisha yao. (W.)
Uwajalie wale wanaotutawala roho yako ya haki na amani;
- uwawezeshe watu kuungana, na kuwa na moyo mmoja na roho moja. (W.)
Uyafanye maisha yetu ya kila siku yawe safari ya wokovu;
- uitajirishe na kuineemesha dunia, ili fukara wajipatie mahitaji yao. (W.)
Kristo, Mwokozi wetu, nuru ya ulimwengu, umewaita wanadamu ambao wote hukabiliwa na kifo
waupate uzima usioharibika;
- uwajalie mwanga wa milele ndugu zetu marehemu. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tuseme kwa pamoja yale maneno aliyotupatia Bwana
yawe kielelezo cha sala zote: Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana Mungu wetu, waupenda moyo usio na hatia, tunapotenda dhambi wewe wafuta makosa yetu.
Uiongoze kwako mioyo ya watu wakuchao, ili baada ya kuondolewa upofu wa utovu wa imani, kamwe
wasiachane na mwanga wa ukweli wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao,
anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.