Generic placeholder image

JUMATANO JUMA LA 5 PASAKA
MASIFU YA ASUBUHI

K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.

ANTIFONA YA MWALIKO:
Bwana amefufuka kweli, aleluya.

(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)

Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuingie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)

Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)

Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)

Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)

Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)

Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)

UTENZI chagua 1-7
1 (25)
Kristo Bwana amefufuka!
Kila mnyororo Bwana kakata,
Sikilizeni, hao malaika
Makelele kwa shangwe wanapiga,
Milele mbinguni juu waimba,
Aleluya!

Aliyekufa kwa ajili yetu,
Na mateso mengi kuvumilia -
Kuvumilia kwa ajili yetu,
Ni Kondoo wetu wa Paska leo!
Nasi pia kwa shangwe tunaimba.
Aleluya!

Yeye aliyepata maumivu
Na hasara yote msalabani,
Sasa yupo katika utukufu,
Akitwombea, huko mbinguni,
Na anasikia kilio chetu.
Aleluya!

Sasa atuagiza tutangaze
Pote pote ulimwenguni jinsi
Ya kuokoka waliopotea,
Na ya kusamehewa wenye toba,
Na tuwezavyo ingia mbinguni.
Aleluya!
Mikaeli Weisse yapata 1480-1534

2 (26)
Aleluya! Aleluya!
Angani inatanda Pasaka!
Yesu ni mzima, hafi tena!
Giza limetokomezwa lote,
Na Bwana wa nuru Mfufuka!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Mama Maria mwone Mwanao,
Anavyofurahi kwa ushindi!
Mateso mlishiriki nyote,
Milele mtatawala nyote!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Watafuta waliopotea!
Naye Petro anakulilia!
Mwimarishe awe mwamba,
Kundi lako alichunge!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Mzima haishi kaburini,
Kristo yupo ghorofani!
Utukufu wake kauficha,
Mwili wake hai aonesha!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Japo uso wake hatuoni,
Yupo na sisi kama mwanzoni!
Ni padre wetu mtukufu,
Twashangilia mtu mzima!
Aleluya! Aleluya!
Yakobo Quinn SJ

3 (27)
Aleluya, mwimbieni Yesu,
Enzi na ufalme ni vyake.
Aleluya, fanaka ni yake,
Ushindi ni wake peke yake.
Sikizeni, nyimbo za Sion
Zinanguruma kama tufani,
Zinasikika kama gharika:
Kwa damu yake ilo azizi,
Yesu ametukomboa sisi,
Watu kutoka kila taifa.

Aleluya, katika huzuni
Kama yatima hatujaachwa;
Aleluya, yu karibu nasi,
Imani yasadiki kabisa,
Haiulizi kwa jinsi gani
Ingawa Bwana alitoweka,
Akafunikwa nayo mawingu
Siku ile ya arobaini,
Tutasahau ahadi yake:
'Nipo nanyi daima milele'?
S. S. Wesley 1810-1876

4 (28)
Kwenye Karamu ya Mwana-Kondoo
Mfalme mshindi twamwimbia,
Alotuosha kwa wingi wa maji
Kutoka penye tobo ubavuni.

Yeye analo pendo la kimungu
Waalikwa wanyweshwa damu yake,
Na awapa waule mwili wake
Pendo ndilo kafara na kuhani.

Panapomwagwa damu ya Pasaka
Mwuaji upanga aufutika;
Jeshi la Israeli lapita
Askari adui wafa maji.

Kristo kondoo aliyechinjwa,
Kafara na mkate wa Pasaka;
Tuile manna itokayo juu
Kwa unyofu na upendo halisi.

Kafara shujaa kutoka juu,
Nguvu za kuzimu ni chini yako;
Vitani mauti umeyashinda,
Uzima na mwanga kutuletea.

Bendera sasa waipeperusha,
Shetani na kaburi watiisha;
Malaika waungana kusifu
Kupinduliwa kwa bwana shetani.

Ushindi na furaha ya Pasaka
Dhambi tu ndo yaweza viharibu;
Tukinge na kifo cha dhambi Bwana,
Tulozaliwa upya ndani yako.

Tenzi za fahari, nyimbo za sifa
Tunakuimbia mpenzi Baba;
Na sifa zote milele mpate,
Bwana Mfufuka na wewe Roho.
Karne ya 7

5 (29)
Utangazeni ushindi wake,
Ewe mbingu na wewe dunia,
Maana Kristo amefufuka
Kama mwenyewe alivyosema:
Ndie yule alosulibiwa,
Ni Mungu kweli aliye hai,
Aliyekaa kwa siku tatu
Kati ya wafu huko kuzimu.

Kristo alikufa kwa aibu
Kwa ajili yetu sisi watu,
Lakini sasa aishi tena
Akiwa na nguvu na uweza;
Moto wake na haujazimwa,
Mwali wake unaoangaza
Ulimwengu wote waujaza
Kwa furaha tele na mwangaza.

Sifa na heshima kwake Baba
Ambaye hakika Hakuumbwa,
Na kwa Mwanae aliye hai
Ambaye hakika hakushindwa,
Bali anatawala kwa enzi
Pamoja na Roho wake Mungu,
Utatu ulio Mtukufu,
Katika yeye Mungu Mmoja.
Stanbrook Abbey Hymnal

6 (30)
Njoni, enyi waamini, njoni,
Mkashangilie kwa furaha;
Mungu kawapa Israeli
Furaha baada ya huzuni;
Wana na binti zake Yakobo
Si watumwa tena wa Farao;
Kawavusha miguu mikavu
Katikati ya Bahari ya Shamu.

Leo ndio roho zachipua;
Kristo jela kabomoa,
Japo siku tatu kawa mfu
Leo kachomoza kama jua;
Kipupwe chote cha dhambi zetu,
Cha muda mrefu na cha kiza,
Metokomezwa kwa yako nuru
Wewe tukusifuye daima.

Milango imara ya mauti,
Wala kaburi pana la giza,
Wala walinzi, wala muhuri,
Havikushiki uwe maiti
Maana leo ulisimama.
Kati yao Kumi na Wawili,
Amani yako ukawapatia
Ipitayo ufahamu wetu.
Mt. Yohane wa Damasko yapata 750

7 (31)
Hakika vita sasa vimekwisha,
Majeshi ya motoni yakimbia;
Tupige ukelele wa ushindi
Kwa furaha na shangwe, aleluya.

Kristo aliyeuvumilia
Ule mti utiao aibu,
Twamkaribisha tukimsifu
Aloshinda mauti, aleluya.

Asubuhi ya tatu kafufuka,
Amevishwa nuru ya utukufu.
Ambayo wenye imani thabiti
Mbinguni watavishwa, aleluya.

Ile milango duni ya kuzimu
Ufunguo wao yaachilia,
Mlango wa Paradisi u wazi;
Tusichoke kuimba, aleluya.

Bwana, kwa mapigo tulokupiga,
Tujalie tuwe mbali na kifo,
Ili tuendelee kukariri
Salamu yetu hii, aleluya.
Simphonia Sirenum 1695

ANT. I: Kwako wewe, Bwana, ndiko iliko chemchemi ya uzima, aleluya.

Zab.36 Uovu wa binadamu
Anayenifuata mimi hatembei kamwe gizani, bali atakuwa na mwanga wa uzima (Yoh.8:12)

Dhambi huongea na mtu mwovu, ndani kabisa moyoni mwake;*
wala jambo la kumcha Mungu, halimo kabisa kwake.

Kwa vile anajiona maarufu sana,/
anafikiri uovu wake hautagunduliwa*
na kulaaniwa na Mungu.

Kila asemacho ni uovu na uwongo*
ameacha kutumia hekima na kutenda mema.

Alalapo huwaza kutenda maovu,/
mwenendo wake hauna lolote jema,*
haepukani na chochote kibaya.

Wema wa Mungu
Ee Mungu, upendo wako mkuu/
wafika hata mbinguni;*
uaminifu wako wafika hata mawinguni.

Uadilifu wako ni kama milima mikubwa mikubwa,/
hukumu zako ni kama vilindi vya bahari.*
Wewe, Ee Mungu, wawalinda wanadamu na wanyama.

Upendo wako, Ee Mungu, ni mkuu ajabu:*
Wanadamu hukimbilia kivulini mwa mabawa yako.

Wawashibisha kwa utajiri wa nyumba yako;*
wawanywesha katika mto wa wema wako.

Wewe ndiwe asili ya uhai;*
kwa mwanga wako twaona mwanga.

wanaokutambua, uendelee kuwapenda;*
kwa waadilifu, uzidi kuwa mwema.

Usikubali wenye majivuno wanivamie,*
wala watu waovu wanikimbize.

Kumbe, watendao maovu wameanguka;*
wameangushwa chini, hawawezi kuinuka.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. I: Kwako wewe, Bwana, ndiko iliko chemchemi ya uzima, aleluya.

ANT. II: Ulimtuma Roho wako, navyo vikaumbwa, aleluya.

WIMBO: Yud.16:1-2a,13-15 Bwana, mwumba wa dunia, huwalinda watu wake
Basi, wakaimba wimbo huu mpya (Ufu.5:9)

Mwimbieni Mungu wangu kwa matari;*
Mwimbieni Bwana wangu kwa matoazi;

Mwimbieni zaburi na nyimbo za shangwe;/
Mtukuzeni, mliitieni jina lake.*
Maana BWANA ndiye Mungu azivunjaye silaha za vita.

Nitamwimbia Mungu wangu wimbo mpya./
Ee BWANA, Wewe ndiwe mkuu, mwenye fahari;*
Wa ajabu katika uweza wako, hakuna kama Wewe.

Viumbe vyako vyote vikutumikie,*
Maana ulisema vikafanyika,

Ulitoa Roho vikaumbwa,*
Wala hakuna atakayeshindana na sauti yako.

Milima husukasuka katika misingi yake kama maji;/
Miamba huyeyuka kama nta mbele yako;*
Lakini u mwenye rehema kwao wanaokucha.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Ulimtuma Roho wako, navyo vikaumbwa, aleluya.

ANT. III: Mungu ni mfalme juu ya dunia yote; imbeni sifa kwa ustadi wenu wote, aleluya.

Zab.47 Mtawala Mkuu
Ameketi kuume kwa Baba, na ufalme wake hautakuwa na mwisho

Enyi watu wote, pigeni makofi!*
Msifuni Mungu kwa shangwe!

Maana Mungu, Mungu Mkuu, anatisha.*
Ni mfalme mkuu wa ulimwengu wote.

Ametuwezesha kuwashinda watu wa mataifa,*
ameyaweka mataifa chini ya mamlaka yetu.

Ametuchagulia nchi hii iwe urithi wetu,*
ambayo ni fahari ya Yakobo anayempenda.

Mungu amepanda juu huku akishangiliwa,*
Mungu amepanda juu akipigiwa tarumbeta.

Mwimbieni Mungu sifa, mwimbieni!*
Mwimbieni Mfalme wetu sifa, mwimbieni!

Mungu ni mfalme wa ulimwengu wote;*
mwimbieni sifa kwa tenzi.

Mungu anayatawala mataifa yote;*
amekaa katika kiti chake cha enzi kitakatifu.

Watawala wa mataifa wanakusanyika,*
pamoja na watu wa Mungu wa Abrahamu.

Yeye ana nguvu kuliko majeshi yote,*
ametukuka juu yao wote.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Mungu ni mfalme juu ya dunia yote; imbeni sifa kwa ustadi wenu wote, aleluya.

SOMO: Rom.6:8-11
Basi, ikiwa tumekufa pamoja na Kristo, tunaamini kwamba tutaishi pia pamoja naye. Maana, tunajua kwamba Kristo amekwisha fufuliwa katika wafu; hafi tena, kifo hakimtawali tena. Hivyo kwa kuwa alikufa mara moja tu dhambi haina tena nguvu juu yake; na sasa anaishi maisha yake katika umoja na Mungu. Hali kadhalika, nanyi lazima mjione kuwa mmekufa kuhusu dhambi, lakini kama mnaoishi katika umoja na Mungu kwa njia ya Kristo Yesu.

KIITIKIZANO
K. Bwana amefufuka kutoka wafu, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Kwa ajili yetu alikufa msalabani.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Zakaria
Mimi ni mzabibu wa kweli, aleluya; nanyi ni matawi, aleluya.

WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.

Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.

Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,

kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.

Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.

Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,

ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.

Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,

utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;

kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.

Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,

na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote *
na milele. Amina

Ant. Mimi ni mzabibu wa kweli, aleluya; nanyi ni matawi, aleluya.

MAOMBI
Tumwombe Kristo aliyeuawa kwa sababu ya dhambi zetu, akafufuka ili atupatanishe na Mungu.
W. Bwana, utuokoe kwa ushindi wako.

Kristo Mwokozi wetu, umeyashinda mauti ili utupatie furaha, na umefufuka upate kutukweza juu kabisa;
- iamshe mioyo yetu, na ututakatifuze leo kwa nguvu ya Roho Mtakatifu. (W.)

Malaika wakutukuza mbinguni, na duniani watu wanakuabudu;
- katika kipindi hiki cha Pasaka, utuwezeshe kukuabudu kwa dhati. (W.)

Bwana Yesu, uwaangalie kwa wema watu wako wanaotumaini kupata ufufuko;
- utuhurumie sisi leo, na utukinge na maovu yote. (W.)

Kristo, uzima wetu, tunaitazamia siku ya ujio wako;
- utuwezeshe kuwa pamoja nawe siku hiyo, na kushiriki utukufu wako. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu wetu, waupenda moyo usio na hatia, tunapotenda dhambi wewe wafuta makosa yetu. Uiongoze kwako mioyo ya watu wakuchao, ili baada ya kuondolewa upofu wa utovu wa imani, kamwe wasiachane na mwanga wa ukweli wako. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.