JUMATANO JUMA 33 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 2Mak.7:1,20-31
Ilitokea ya kuwa ndugu saba, pamoja na mama yao, walikamatwa kwa amri ya mfalme na kuteswa sana
kwa mijeledi na mapigo ili kuwashurutisha kuonja nyama marufuku ya nguruwe. Aliyekuwa wa ajabu
hasa, na kustahili kumbukumbu la heshima, ndiye yule mama. Maana aliwaona wanawe saba wakifa kwa
siku moja, akistahimili kwa moyo thabiti kwa ajili ya matumaini aliyoyaweka kwa Bwana. Kwa roho
hodari aliimarisha tabia yake ya kike kwa ushupavu wa kiume, akamfariji kila mtoto kwa lugha ya
wazee wao, akisema, Jinsi mlivyoingia tumboni mwangu sijui. Si mimi niliyekupeni roho na uzima,
wala si mimi niliyeziunga sehemu za miili yenu. Bali ni yeye, Muumba ulimwengu; yeye aumbaye
wanadamu na kukikusudia chanzo cha vitu vyote; naye kwa rehema zake akakurudishieni roho zenu
na uzima wenu, kwa kuwa ninyi sasa mnajihesabu kuwa si kitu kwa ajili ya amri zake. Antioko alijiona
anafedheheshwa, lakini bila kuangalia mzaha wa maneno yake, alimsihi yule mdogo, maana alikuwa
yungali hai, akamwambia, si kwa maneno tu ila pia kw auapa, ya kuwa, akama ataziacha sheria za
wazee wake, atampatia mali nyingi na hali njema; tena, atamfanya mmoja wa rafiki zake na kumkabidhi
kazi za ufalme. Yule kijana asipokubali, alimwita mama yake, akamtaka amshawishi mtoto ajiokoe.
Akasema naye kwa maneno mengi, hata mwisho alikubali kumshauri mwanawe. Akamwinamia na huku
anamdhihaki yule mfalme mkali akasema hivi kwa lugha ya wazee wake: Mwanangu, unirehemu mimi
niliyekuchukua tumboni mwangu kwa miezi tisa, na kukutunza na kukulea mpka sasa. Nakusihi, mwanangu,
inua macho yako utazame mbingu na nchi, ukaone vitu vyote vilivyomo; fahamu kwamba Mungu hakuviumba
kwa vitu vilivyokuwapo. Na ndivyo alivyofanya wanadamu pia. Usiogope mwuaji huyu; jionyeshe
umestahilika sawasawa na dnugu zako. Kubali kufa kwako, ili kwa rehema ya Mungu nikupokee tena
pamoja na ndugu zako. Hakudiriki kuyamaliza maneno yake, ila yule kijana alisema, Mnamngoja nini?
Mimi siitii amri ya mfalme, bali naitii amri ya sheria waliyopewa baba zetu kwa Musa. Wewe,
uliyebuni kila namna ya uovu juu ya Waebrania, hutaokoka kabisa katika mikono ya Mungu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.17:1,5-6,8,15 (K)15
1. Ee Bwana, usikie haki, ukisikilize kilio changu,
Utege sikio lako kwa maombi yangu,
Yasiotoka katika midomo ya hila.
(K) Nishibishe kwa sura yako, Ee Bwana.
2. Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako,
Hatua zangu hazikuondoshwa.
Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitikia,
Utege sikio lako ulisikie neno langu. (K)
3. Unilinde kama mboni ya jicho,
Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako.
Nikutazame uso wako katika haki,
Niamkapo nishibishwe kwa sura yako. (K)
SHANGILIO: Yn.10:27
Aleluya, aleluya!
Kondoo wangu waisikia sauti yangu,
nami nawajua, nao wanifuata.
Aleluya!
INJILI: Lk.19:11-28
Makutano waliposikia hayo, aliongeza kusema mfano, kwa sababu alikuwa karibu na Yerusalemu, na
wao walidhani ya kuwa ufalme wa Mungu utaonekana mara. Basi akasema, Mtu mmoja, kabaila, alisafiri
kwenda nchi ya mbali, ili ajipatie ufalme na kurudi. Akaita watu kumi katika watumwa wake, akawapa
mafungu kumi ya fedha, akawaambia, Fanyeni biashara hata nitakapokuja. Lakini watu wa mji wake
walimchukia, wakatuma wajumbe kumfuata na kusema, Hatumtaki huyu atutawale. Ikawa aliporudi,
ameupata ufalme wake, aliamuru waitwe wale watumwa aliowapa fedha, ili ajue faida aliyopata kila
mtu kwa biashara yake. Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi
zaidi. Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe
na mamlaka juu ya miji kumi. Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.
Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano. Akaja mwingine akasema, Bwana, hili ndilo fungu
lako, ambalo nililiweka akiba katika leso. Kwa maana nilikuogopa kwa kuwa u mtu mgumu; waondoa
usichoweka, wavuna usichopanda. Akamwambia, Nitakuhukumu kwa kinywa chako, mtumwa mwovu wewe.
Ulinijua kuwa ni mtu mgumu, niondoaye nisichoweka, na kuvuna nisichopanda; basi, mbona hukuiweka
fedha yangu kwa watoao riba, ili nijapo niipate pamoja na faida yake? Akawaambia waliosimama karibu,
Mnyang'anyeni hilo fungu, mkampe yule mwenye mafungu kumi. Wakamwambia, Bwana, anayo mafungu kumi.
Nawaambia, Kila aliye na kitu atapewa, bali yule asiye na kitu atanyang'anywa hata alicho nacho.
Tena, wale adui zangu, wasiotaka niwatawale, waleteni hapa mwachinje mbele yangu. Na alipokwisha
kusema hayo, alitangulia mbele akipanda kwenda Yerusalemu.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, daima tunaalikwa kumruhusu Mungu ayatawale maisha yetu. Lakini mara nyingi
tunashindwa kwa sababu ya vishawishi mbalimbali. Tuombe neema yake.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Maaskofu na Mapadre wetu wawe mfano bora katika kuvishinda vishawishi vya yule
mwovu, ili imani yao idhihirike daima katika matendo mema. Ee Bwana.
2. Watawala wa dunia wajaliwe unyenyekevu mbele yako na utii kwa amri zako. Ee Bwana.
3. Umsaidie kila mmoja wetu kuvitumia vema vipaji ulivyomjalia, ili siku ya mwisho
apate kutolea hesabu ya utumishi wake. Ee Bwana.
4. Uamshe mioyo ya wasioujali ukuu na utakatifu wako, wapate kukukiri Wewe uketiye
katika kiti cha enzi, uliyeumba vitu vyote na unayestahili kusifiwa na kuabudiwa
milele. Ee Bwana.
5. Kwa rehema yako, uwapokee ndugu zetu marehemu na kuwakaribisha kwenye nyumba
yako ya kifalme huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, Mwanao alisema kila aliye na kitu atapewa. Utujalie hayo tuliyokuomba.
Kwa njia ya huyo Kristo Bwana wetu. Amina.