JUMATANO JUMA 31 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Rum.13:8-10
Msiwiwe na mtu chochote, isipokuwa kupendana; kwa maana ampendaye mwenzake ameitimiza sheria. Maana
kule kusema, Usizini, Usiue, Usiibe, Usitamani, na ikiwapo amri nyingine yoyote, inajumlishwa katika
neno hili, ya kwamba, Mpende jirani yako kama nafsi yako. Pendo halimfanyii jirani neno baya; basi
pendo ndilo utimilifu wa sheria.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.112:1-2,4-5,9
1. Aleluya,
Heri mtu yule amchaye Bwana,
Apendezwaye sana na maagizo yake.
Wazao wake watakuwa hodari duniani;
Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.
(K) Heri atendaye fadhili na kukopesha.
2. Nuru huwazukia wenye adili gizani;
Ana fadhili na huruma na haki.
Heri atendaye fadhili na kukopesha;
Atengenezaye mambo yake kwa haki. (K)
3. Amekirimu, na kuwapa maskini,
Haki yake yakaa milele,
Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu. (K)
SHANGILIO: Mt.11:25
Aleluya, aleluya!
Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi,
kwa kuwa mambo haya uliwaficha wenye hekima na akili,
ukawafunulia watoto wachanga.
Aleluya!
INJILI: Lk.14:25-33
Makutano mengi walipokuwa wakifuatana na Yesu, aligeuka, akawaambia, Kama mtu akija kwangu naye
hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume kwa wake, na wanawe,
na ndugu zake waume kwa wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Mtu
yeyote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu. Maana ni nani
katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya
kuumalizia? Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki,
wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza. Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda
kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi
ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini? Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe
kutaka sharti za Amani, mtu yule akali mbali. Basi, kadhlika kila mmoja wenu asiyeacha vyote alivyo
navyo, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, Wewe ni upendo na umetuhimiza kupendana,
kwa kuwa pendo ndilo utimilifu wa sheria. Basi,
twakuomba:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Baba Mtakatifu wetu F. na Maaskofu
wote wazidi kulipenda Kanisa ulilowakabidhi, lipate kustawi
kimwili na kiroho siku hadi siku. Ee Bwana.
2. Viongozi wenye dhamana ya kuwahudumia watu,
serikalini na kwenye taasisi na sekta binafsi, watende
mambo yote pasipo manung'uniko wala lawama yoyote. Ee Bwana.
3. Wote wasiolitukuza jina lako wajaliwe kujihoji na
kujipatanisha nawe kwa upendo kabla ya siku ya hukumu. Ee Bwana.
4. Msalaba wa Kristo utukumbushe daima juu ya sadaka
tunayopaswa kukutolea Wewe Mungu, kwa kuacha yote na kukufuata
kwa upendo. Ee Bwana.
5. Ndugu zetu marehemu waliojitahidi kuuishi upendo
wapewe huruma yako na kuurithi ufalme wako wa mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetaka tuyafanye yote kwa upendo,
uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Amina.