JUMATANO JUMA LA 2 PASAKA
MASOMO
SOMO: Mdo.5:17-26
Akaondoka Kuhani Mkuu na wote waliokuwa pamoja naye, (hao ndio walio wa madhehebu ya Masadukayo),
wamejaa wivu, wakawakamata mitume wakawaweka ndani ya gereza; lakini malaika wa Bwana akafungua
milango ya gereza usiku, akawatoa, akasema, Enendeni mkasimame hekaluni mkawaambie watu maneno
yote ya Uzima huu. Nao waliposikia wakaenda alfajiri hekaluni, wakaanza kufundisha. Akaja Kuhani
Mkuu nao waliokuwa pamoja naye, wakawakutanisha watu wa baraza, na wazee wote wa wana wa Israeli,
wakatuma watu gerezani ili wawalete. Hata watumishi walipofika hawakuwaona gerezani, wakarudi wakatoa
habari, wakisema, Gereza tumeikuta imefungwa salama, nao walinzi wamesimama mbele ya mlango;
lakini tulipoufungua hatukukuta mtu ndani. Basi jemadari wa hekalu na wakuu wa makuhani waliposikia
haya, wakaingiwa na shaka kwa ajili yao, litakuwaje jambo hilo. Mtu mmoja akaja akawapasha habari ya
kwamba, Watu wale mliowaweka gerezani wako ndani ya hekalu, wamesimama wakiwafundisha watu. Ndipo
yule jemadari akaenda pamoja na watumishi, wakawaleta, lakini si kwa nguvu, kwa maana waliogopa watu
wasije wakawapiga kwa mawe.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.34:1-8(K)6
1. Nitamhimidi Bwana kila wakati,
Sifa zake zi kinywani mwangu daima.
Katika Bwana nafsi yangu itajisifu,
Wanyenyekevu wasikie wakafurahi.
(K) Maskini huyu aliita, Bwana akasikia.
2. Mtukuzeni Bwana pamoja nami,
Na tuliadhimishe jina lake pamoja.
Nalimtafuta Bwana akanijibu,
Akaniponya na hofu zangu zote. (K)
3. Wakamwelekea macho wakatiwa nuru,
Wala nyuso zao hazitaona haya.
Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote. (K)
4. Malaika wa Bwana hufanya kituo,
Akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
Onjeni mwone ya kuwa Bwana yu mwema;
Heri mtu yule anayemtumaini. (K)
SHANGILIO: Rum.6:9
Aleluya, aleluya,
Kristo akiisha kufufuka,
katika wafu hafi tena.
Mauti haimtawali tena.
Aleluya.
INJILI: Yn.3:16-21
Kwa maana jinsi hii Mungu aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu
amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. Maana Mungu hakumtuma Mwana ulimwenguni
ili auhukumu ulimwengu, bali ulimwengu uokolewe katika yeye. Amwaminiye yeye hahukumiwi;
asiyeamini amekwisha kuhukumiwa; kwa sababu hakuliamini jina la Mwana pekee wa Mungu. Na
hii ndiyo hukumu; ya kuwa nuru imekuja ulimwenguni, na watu wakapenda giza kuliko nuru;
kwa maana matendo yao yalikuwa maovu. Maana kila mtu atendaye mabaya huichukia nuru, wala
haji kwenye nuru, matendo yake yasije yakakemewa. Bali yeye aitendaye kweli huja kwenye
nuru, ili matendo yake yaonekane wazi ya kuwa yametendwa katika Mungu.
MAOMBI
Mungu alimtuma Mwanae ulimwenguni ili tupate kuokolewa kwa fumbo la Paska. Kwa imani na matumaini tumwombe
katika shida zetu.
Kiitikio: Twakuomba utusikie
1. Malaika wako wawalinde viongozi wetu wa Kanisa dhidi ya maadui wasiokujua wewe.
2. Ubariki juhudi za viongozi wetu wa nchi katika kuyastawisha maisha safi ya raia wao.
3. Sisi sote tupende maisha ya nuru na tushirikiane katika kukemea matendo maovu.
4. Marehemu waliomwamini Mwanao wasipotee, bali wapate uzima wa milele pamoja naye huko mbinguni.
Tunaomba hayo na utukirimie hata yale tusiyodiriki kukuomba. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.