JUMATANO JUMA 29 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Rum.6:12-18
Dhambi isitawale ndani ya miili yenu ipatikanayo na mauti, hata mkazitii tamaa zake; wala msiendelee
kuvitoa viungo vyenu kuwa silaha za dhuluma kwa dhambi; bali jitoeni wenyewe kwa Mungu kama walio hai
baada ya kufa, na viungo vyenu kwa Mungu kuwa silaha za haki. Kwa maana dhambi haitawatawala ninyi,
kwa sababu hamwi chini ya sheria, bali chini ya neema. Ni nini basi? Tufanye dhambi kwa sababu hatuwi
chini ya sheria bali chini ya neema? Hasha! Hamjui ya kuwa kwake yeye ambaye mnajitoa nafsi zenu kuwa
watumwa wake katika kumtii, mmekuwa watumwa wake yule mnayemtii, kwamba ni utumishi wa dhambi uletao
mauti, au kwamba ni utumishi wa utii uletao haki. Lakini Mungu na ashukuriwe, kwa maana mlikuwa watumwa
wa dhambi, lakini mliitii kwa mioyo yenu ile namna ya elimu ambayo mliwekwa chini yake; na mlipokwisha
kuwekwa huru mbali na dhambi, mkawa watumwa wa haki.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.124 (K)8
1. Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
Israeli na aseme sasa,
Kama si Bwana aliyekuwa pamoja nasi,
Wanadamu walipotushambulia.
Papo hapo wangalitumeza hai,
Hasira yao ilipowaka juu yetu.
(K) Msaada wetu u katika jina la Bwana.
2. Papo hapo maji yangalitugharikisha,
Mto ungalipita juu ya roho zetu;
Papo hapo yangalipita juu ya nafsi zetu Maji yafurikayo.
Na ahimidiwe Bwana;
Asiyetutoa kuwa mawindo kwa meno yao.
3. Nafsi yetu imeokoka kama ndege Katika mtego wa wawindaji,
Mtego umevunjika, nasi tumeokoka.
Msaada wetu u katika jina la Bwana,
Aliyezifanya mbingu na nchi. (K)
SHANGILIO: Yn.14:5
Aleluya, aleluya!
Bwana anasema: Mimi ndimi njia, na ukweli,
na uzima, mtu haji kwa Baba, ila kwa njia ya mimi.
Aleluya!
INJILI: Lk.12:39-48
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Fahamuni neno hili, Kwamba mwenye nyumba angalijua saa atakayokuja
mwivi; angalikesha, wala asingaliacha nyumba yake kuvunjwa. Nanyi jiwekeni tayari, kwa kuwa saa
msiyodhani ndipo ajapo Mwana wa Adamu. Petro akamwambia, Bwana, mithali hiyo umetuambia sisi tu,
au watu wote pia? Bwana akasema, Ni nani, basi, aliye wakili mwaminifu, mwenye busara, ambaye bwana
wake atamweka juu ya utumishi wake wote, awape watu posho kwa wakati wake? Heri mtumwa yule, ambaye
bwana wake ajapo atamkuta anafanya hivyo. Kweli nawaambia, atamweka juu ya vitu vyake vyote. Lakini,
mtumwa yule akisema moyoni mwake, Bwana wangu anakawia kuja, akaanza kuwapiga wajoli wake, wanaume
kwa wanawake, akila na kunywa na kulewa; bwana wake mtumwa huyo atakuja siku asiyodhani na saa asiyojua,
atamkata vipande viwili, na kumwekea fungu lake pamoja na wasioamini. Na mtumwa yule aliyejua mapenzi
ya bwana wake, asijiweke tayari, wala kuyatenda mapenzi yake, atapigwa sana. Na yule asiyejua, naye
amefanya yastahiliyo mapigo, atapigwa kidogo. Na kila aliyepewa vingi, kwake huyo vitatakwa vingi;
naye waliyemwekea amana vitu vingi, kwake huyo watataka na zaidi.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, kwa kuwa saa tusiyodhani ndiyo ajayo
Mwana wa Adamu, tusali kwa Mungu tukisema:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Upokee shukrani zetu kwa kuwa umewaweka
Maaskofu kuwa mawakili wako wenye busara, wapate
kuwa juu ya utumishi wa Kanisa lako na kuwaandaa
watu kwa ujio wa Mwanao. Ee Bwana.
2. Viongozi wetu wa serikali waimarishe mahusiano
mazuri na Mataifa jirani, kwani ni warithi pamoja
nasi wa urithi mmoja, na washiriki pamoja nasi wa
ahadi yako ya ukombozi. Ee Bwana.
3. Uwaongoe watumwa wa dhambi, wapate kuungojea
ujio wa Bwana kwa saburi. Ee Bwana.
4. Umjalie kila mmoja wetu kuwa mtumwa wa haki, kwa
kukesha kila siku na kuzitii amri zako. Ee Bwana.
5. Wote waliomaliza safari yao hapa duniani wapewe
rehema yako na uzima usio na mwisho huko kwenye
makao yako ya milele. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyesema kila aliyepewa vingi atatakiwa kutoa
vingi vile vile, uyapokee maombi haya tuliyokutolea.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.