JUMATANO JUMA 28 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Rum.2:1-11
Wewe mtu uwaye yote uhukumuye, huna udhuru; kwa maana katika hayo umhukumuyo mwingine wajihukumu mwenyewe kuwa na hatia; kwa maana wewe uhukumuye unafanya yale yale. Nasi twajua ya kuwa hukumu ya Mungu ni ya kweli juu yao wafanyao hayo. Wewe binadamu, uwahukumuye wale wafanyao hayo na kutenda yayo hayo mwenyewe, je! Wadhani ya kwamba utajiepusha na hukumu ya Mungu? Au waudharau wingi wa wema wake na ustahimili wake na uvumilivu wake, usijue ya kuwa wema wa Mungu wakuvuta upate kutubu? Bali kwa kadiri ya ugumu wako, na kwa moyo wako usio na toba, wajiwekea akiba ya hasira kwa siku ile ya hasira na ufunuo wa hukumu ya haki ya Mungu, atakayemlipa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake; wale ambao kwa saburi katika kutenda mema wanatafuta utukufu na heshima na kutokuharibika, watapewa uzima wa milele; na wale wenye fitina, wasioitii kweli, bali wakubalio dhuluma, watapata hasira na ghadhabu; dhiki na shida juu ya kila nafsi ya mwanadamu atendaye uovu, Myahudi kwanza na Myunani pia; bali utukufu na heshima na amani kwa kila mtu atendaye mema, Myahudi kwanza na Myunani pia; kwa maana hakuna upendeleo kwa Mungu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.62:1-2,5-6,8 (K)12
1. Nafsi yangu yamngoja Mungu peke yake kwa kimya, Wokovu wangu hutoka kwake. Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana.

(K) Bwana humlipa kila mtu sawasawa na haki yake.

2. Nafsi yangu, umngoje Mungu peke yake kwa kimya. Tumaini langu hutoka kwake. Yeye tu ndiye mwamba wangu na wokovu wangu, Ngome yangu, sitatikisika sana. (K)

3. Enyi watu, mtumainini sikuzote, Ifunueni mioyo yenu mbele zake; Mungu ndiye kimbilio letu. (K)

SHANGILIO: Zab.27:11
Aleluya, aleluya!
Ee Bwana, unifundishe njia yako,
na kuniongoza katika njia iliyonyoka.
Aleluya!

INJILI: Lk.11:42-46
Yesu aliwaambia Mafarisayo: Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwatoa zaka za mnanaa na mchicha na kila mboga, na huku mwaacha mambo ya adili, na upendo wa Mungu; iliwapasa kuyafanya hayo ya kwanza, bila kuyaacha hayo ya pili. Ole wenu, Mafarisayo, kwa kuwa mwapenda kuketi mbele katika masinagogi, na kusalimiwa masokoni. Ole wenu, kwa kuwa mmefanana na makaburi yasiyoonekana, ambayo watu wapitao juu yake hawana habari nayo. Mtu mmoja katika wanasheria akajibu, akamwambia, Mwalimu, kwa kusema hayo umetushutumu sisi nasi. Akasema, Nanyi wanasheria, ole wenu, kwa sababu mwawatwika watu mizigo isiyochukulika, wala ninyi wenyewe hamwigusi mizigo hiyo hata kwa kimoja cha vidole vyenu.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Mungu, umetufunulia kuwa kila mtu atalipwa kwa kadiri ya matendo yake; na kwamba kwako hakuna upendeleo. Basi, twakuomba:-

Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Baba Mtakatifu wetu F. na viongozi wote wa Kanisa waimarishwe, katika kuwahubiria watu bila woga, juu ya ukweli wa Injili yako. Ee Bwana.

2. Serikali yetu isichoke kupambana na waovu ili, sheria ikishachukua mkondo wake, watu waishi kwa furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu, upole na kiasi. Ee Bwana.

3. Wote wasiokukiri Wewe Mungu wavutwe na wema wako usio na mipaka na kutubu. Ee Bwana.

4. Kila mmoja wetu ajaliwe kujiepusha na hukumu yako ya mwisho kwa kuishi kitakatifu siku zote. Ee Bwana.

5. Uwarudishe waliopotoshwa; na marehemu wetu wapewe msamaha wa dhambi na taji ya utukufu usio na mwisho. Ee Bwana.

Ee Mungu unayetaka tutangulize upendo katika yote uliyotuamuru, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.