JUMATANO JUMA 26 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Neh.2:1-8
Ikawa katika mwezi wa Nisani, mwaka wa ishirini wa mfalme Artashasta, na divai imewekwa mbele yake, nikaishika ile divai, nikampa mfalme. Nami mpaka sasa sikuwa na huzuni mbele ya mfalme wakati wo wote. Basi mfalme akaniambia, Mbona umesikitika uso wako, nawe huna ugonjwa? Nini hii, isipokuwa ni huzuni ya moyo? Ndipo nikaogopa sana. Nikamwambia mfalme, Mfalme na aishi milele; kwani uso wangu usiwe na huzuni, iwapo mji, ulio mahali pa makaburi ya baba zangu, unakaa ukiwa, na malango yake yameteketezwa kwa moto? Ndipo mfalme akaniambia, Una haja gani unayotaka kuniomba? Basi nikamwomba Mungu wa mbinguni. Nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na ikiwa mimi, mtumishi wako, nimepata kibali machoni pako, tafadhali unipeleke mpaka Yuda, niuendee mji wa makaburi ya baba zangu, nipate kuujenga. Mfalme akaniuliza, (malkia naye ameketi karibu naye), Safari yako itakuwa ya siku ngapi? Nawe utarudi lini? Hivyo mfalme akaona vema kunipeleka; nami nikampa muda. Tena nikamwambia mfalme, Mfalme akiona vema, na nipewe nyaraka kwa maliwali walio ng'ambo ya Mto, ili waniache kupita mpaka nifike Yuda; nipewe na waraka kwa Asafu, mwenye kuutunza mwitu wa mfalme, ili anipe miti ya kufanyizia boriti kwa malango ya ngome ya nyumba, na kwa ukuta wa mji; na kwa nyumba ile nitakayoingia mimi. Naye mfalme akanipa, kama mkono mwema wa Mungu wangu ulivyokuwa juu yangu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.137:1-6 (K)6
1. Kando ya mito ya Babeli ndiko tulikoketi,
Tukalia tulipoikumbuka Sayuni.
Katika miti iliyo katikati yake
Tulivitundika vinubi vyetu.

(K) Ulimi wangu na ugandamane
na kaakaa ka kinywa changu,
nisipokukumbuka.

2. Maana huko waliotuchukua mateka
Walitaka tuwaimbie;
Na waliotuonea walitaka furaha;
Tuimbieni baadhi ya nyimbo za Sayuni. (K)

3. Tuuimbeje wimbo wa Bwana
Katika nchi ya ugeni?
Ee Yerusalemu, nikikusahau wewe,
Mkono wangu wa kuume na usahau. (K)

Ulimi wangu na ugandamane
Na kaakaa la kinywa changu, nisipokukumbuka.
Nisipoikuza Yerusalemu
Zaidi ya furaha yangu iliyo kuu. (K)

SHANGILIO: Zab.147:12
Aleluya, aleluya!
Msifu Bwana, Ee Yerusalemu,
huipeleka amri yake juu ya nchi.
Aleluya!

INJILI: Lk.9:57-62
Yesu na wanafunzi wake walipokuwa wakienda njiani, mtu mmoja alimwambia, Nitakufuata kokote utakakokwenda. Yesu akamwambia, Mbweha wana pango, na ndege wa angani wana vioto, lakini Mwana wa Adamu hana pa kujilaza kichwa chake. Akamwambia mwingine, Nifuate. Akasema, Bwana, nipe ruhusu kwanza niende nikamzike baba yangu. Akamwambia, Waache wafu wawazike wafu; bali wewe enenda ukautangaze ufalme wa Mungu. Mtu mwingine pia akamwambia, Bwana, nitakufuata; lakini, nipe ruhusu kwanza nikawaage watu wa nyumbani mwangu. Yesu akamwambia, Mtu aliyetia mkono wake kulima, kisha akaangalia nyuma, hafai kwa ufalme wa Mungu.

--------------

--------------
MAOMBI
Wapendwa, Mungu anataka tuitikie wito wake na tuvitumie vipaji vyetu kwa manufaa ya Kanisa. Basi, tuombe msaada na neema yake.

Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwabariki Askofu wetu F. na Mapadre wetu wote, na uwabidishe katika kuwashirikisha waamini wao katika shughuli za kitume, ili Kanisa listawishwe kwa vipaji ulivyotujalia. Ee Bwana.

2. Uwabariki viongozi na watawala wote wanaolitakia mema Kanisa lako na kutoa ushirikiano katika kulijenga na kulistawisha kimwili na kiroho. Ee Bwana.

3. Utujalie kuuitikia wito wako kila siku bila masharti, tupate kwenda wakati wowote na kokote unakotutuma, kadiri ya, wito na nafasi ya kila mmoja wetu. Ee Bwana.

4. Wote waliopatwa na majanga au matatizo makubwa, wasikose imani kwako na katika uwezo wako wa kuokoa; bali waendelee kukuita wakitumaini kusikilizwa nawe. Ee Bwana.

5. Uwaite marehemu wetu wapate kuingia kwenye makao yako ya milele huko mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu, uyapokee maombi yetu kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.