JUMATANO JUMA 25 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Ezr.9:5-9
Wakati wa sadaka ya jioni, mimi Ezra niliinuka baada ya kunyenyekea kwangu, nguo yangu na joho yangu
zimeraruliwa, nikaanguka magotini nikakunjua mikono yangu mbele za Bwana, Mungu wangu; nikasema,
Ee Mungu wangu, nimetahayari, naona haya kuinua uso wangu mbele zako, Mungu wangu; kwa maana maovu
yetu ni mengi, hata yamefika juu ya vichwa vyetu, na hatia yetu imeongezeka na kufika mbinguni. Tangu
siku za baba zetu tumekuwa na hatia kupita kiasi hata leo; na kwa sababu ya maovu yetu sisi, na
wafalme wetu, na makuhani wetu, tumetiwa katika mikono ya wafalme wa nchi hizi, tumepigwa kwa upanga,
tumechukuliwa mateka, tumenyang’anywa mali zetu, tumetiwa haya nyuso zetu, kama hivi leo. Na sasa
kwa muda kidogo tumeneemeshwa na Bwana, Mungu wetu, hata akatuachia mabaki yaokoke, akatupa msumari
katika mahali pake patakatifu. Mungu wetu atutie nuru machoni mwetu, tuburudike kidogo katika
kufungwa kwetu. Maana sisi tu watumwa; lakini Mungu wetu hakutuacha katika utumwa wetu, bali
ametufikilizia rehema zake, mbele ya wafalme wa Uajemi, ili kutuburudisha, tuisimamishe nyumba
ya Mungu wetu, na kuitengeneza palipobomoka, atupe ukuta katika Yuda na Yerusalemu.
WIMBO WA KATIKATI: Tob.13:2-4,6 (K)1
1. Kwa maana hurudi, na kurehemu tena;
Hushusha hata kuzimu, na kuinua tena;
Wala hakuna awezaye kujiepusha na mkono wake.
(K) Amehimidiwa Mungu aishiye milele.
2. Enyi bani Israeli, mshukuruni mbele ya mataifa
Yeye ambaye ametutawanya katikati yao. (K)
3. Kuko huko utangazeni ukuu wake,
Mwadhimisheni mbele ya wote walio hai;
Kwa kuwa Yeye ndiye Bwana wetu,
Naye Mungu yu Baba wetu,
Naye Mungu yu Baba yetu milele. (K)
SHANGILIO: 1The.2:13
Aleluya, aleluya!
Ee Mungu, tunakusifu, tunakukiri kuwa Bwana.
Jamii tukufu ya Mitume inakusifu.
Aleluya!
INJILI: Lk.9:1-6
Yesu aliwaita wale Thenashara, akawapa uwezo na mamlaka juu ya pepo wote na kuponya maradhi.
Akawatuma wautangaze ufalme wa Mungu, na kupoza wagonjwa. Akawaambia, Msichukue kitu kwa safari
yenu, fimbo, wala mkoba, wala mkate wala fedha, wala mmoja wenu asiwe na kanzu mbili. Na nyumba
yoyote mtakayoingia kaeni humo, mpaka mtoke humo. Na wale wasiowakaribisha, mtokapo katika mji huo,
yakung’uteni hata mavumbi ya miguuni mwenu, kuwa ushuhuda juu yao. Wakaenda, wakazunguka katika
vijiji, wakihubiri Injili na kupoza watu kila mahali.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, Mungu amemwita kila mmoja wetu kama alivyo, ili
akaitangaze Injili yake. Kwa vile ni wajibu mkubwa, nasi tu
dhaifu, tuombe neema yake.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Umjalie Askofu wetu F. na
Mapadre wetu wote afya na nguvu, wapate kutekeleza sawa sawa
kazi za kitume, ulizowakabidhi kwa ajili ya Kanisa lako. Ee Bwana.
2. Wote waliodhaminiwa kuwatawala watu badala yako
wajaliwe kuwatumikia watu wako kadiri ya mapenzi yako. Ee Bwana.
3. Umwepushe na maovu kila mmoja wetu, ili tuondokane na
utumwa wa dhambi, na kuwa mfano mzuri wa fadhila kwa wenzetu. Ee Bwana.
4. Utuondolee ubatili na uwongo; utukarimu kadiri ya
kipimo tunachohitaji; na utujalie kutolitaja bure Jina lako Takatifu.
Ee Bwana.
5. Uwakumbuke ndugu zetu marehemu na uwashirikishe
uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Tunayaleta maombi yetu haya kwako, Ee Mungu Baba, kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.