JUMATANO JUMA 24 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 1Tim.3:14-16
Nakuandikia hayo, nikitaraji kuja kwako hivi karibu. Lakini nikikawia, upate kujua jinsi iwapasavyo
watu kuenenda katika nyumba Mungu, iliyo kanisa la Mungu aliye hai, nguzo na msingi wa kweli. Na bila
shaka siri ya utauwa ni kuu: Mungu alidhihirishwa katika mwili, Akajulika kuwa na haki katika roho,
Akaonekana na malaika, Akahubiriwa katika mataifa, Akaaminiwa katika ulimwengu, Akachukuliwa juu
katika utukufu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.111:1-6 (K)2
1. Nitamshukuru Bwana kwa moyo wangu wote,
Barazani pa wanyofu wa moyo na katika mkutano.
Matendo ya Bwana ni makuu.
Yafikiriwa sana na wapendezwao nayo.
(K) Heri taifa ambalo Bwana ni Mungu wao.
2. Kazi yake ni heshima na adhama,
Na haki yake yakaa milele.
Amefanya ukumbusho wa matendo yake ya ajabu;
Bwana ni mwenye fadhili na rehema. (K)
3. Amewapa wamchao chakula;
Atalikumbuka agano lake milele.
Amewajulisha watu wake uwezo wa matendo yake,
Kwa kuwapa urithi wa mataifa. (K)
SHANGILIO: Lk.6:63,68
Aleluya, aleluya!
Maneno yako, Bwana, ni roho na uzima.
Wewe unayo maneno ya uzima wa milele.
Aleluya!
INJILI: Lk.7:31-35
Yesu aliwaambia makutano: Niwafananishe na nini watu wa kizazi hiki? Nao wamefanana na nini?
Wamefanana na watoto walioketi sokoni na kuitana, wakisema, Tuliwapigia filimbi wala hamkucheza;
tuliomboleza, wala hamkulia. Kwa kuwa Yohane Mbatizaji alikuja, hali mkate wala hanywi divai,
nanyi mwasema, ana pepo. Mwana wa Adamu amekuja, anakula na kunywa; nanyi mwasema, Tazama,
mlafi huyu, na mnywaji wa divai, rafiki wao watoza ushuru na wenye dhambi. Na hekima imejulikana
huwa ina haki kwa watoto wake wote.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kanisa ni nyumba ya Mungu na mahali rasmi
pa kukutana na kuongea naye. Kwa vile yupo tayari
kutusikiliza, tumwombe.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwajalie wachungaji wetu udumifu katika kuwaelekeza
kwa upole watu wote, kuitikia mwito wa kulitunza na
kulitumia vema kanisa lako. Ee Bwana.
2. Ubariki juhudi za viongozi wa serikali, asasi na
taasisi zake, katika kutimiza amri yako ya upendo kwa watu
wote. Ee Bwana.
3. Wote waliojitenga nawe na wenye dhambi wajaliwe
moyo wa kumkaribia Mwanao, Yesu Kristo, aliyekuja kwa ajili
yao. Ee Bwana.
4. Sisi sote tujaliwe kuijua siri kuu ya utaua, tupate
kukudhihirisha na kukuhubiri kwa mataifa, ili nao wapate kukuamini
na kuokoka. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wapokelewe huko mbinguni na kupewa
uzima wa milele. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetaka hekima ijulikane kuwa ina haki kwa
watoto wake wote, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.