JUMATANO JUMA 23 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kol.3:1-11
Mkiwa mmefufunuliwa pamoja na Kristo yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume
wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa
pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa
pamoja naye katika utukufu. Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu,
tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu; kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu
ya Mungu. Katika hayo ninyi nanyi mlitembea zamani, mlipoishi katika hayo. Lakini sasa yawekeni mbali
nanyi haya haya yote, hasira, na ghadhabu, na uovu, na matukano, na matusi vinywani mwenu. Msiambiane
uongo, kw akuwa mmevua kabisa utu wa kale, pamoja na matendo yake; mkivaa utu mpya, unaofanywa upya
upate upafamu sawasawa na mfano wake yeye aliuumba. Hapo hapana Myunani wala Myahudi, kutahiriwa wala
kutokutahiriwa, mgeni wala mshenzi mtumwa wala mwungwana, bali kristo ni yote, na katika yote.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.145:2-3,10-13 (K)9
1. Kila siku nitakuhimidi,
Nitalisifu jina lako milele na milele.
Bwana ndiye mkuu mwenye kusifiwa sana,
Wala ukuu wake hautambulikani.
(K) Bwana ni mwema kwa watu wote.
2. Ee Bwana, kazi zako zote zitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako,
Na kuuhadithia uweza wako. (K)
3. Ili kuwajulisha watu matendo yake makuu,
Na utukufu wa fahari ya ufalme wake.
Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote. (K)
SHANGILIO: Zab.119:28,33
Aleluya, aleluya!
Unitie nguvu sawasawa na neno lako,
Ee Bwana, unifundishe njia ya amri zako.
Aleluya!
INJILI: Lk.6:20-26
Yesu aliinua macho yake akawatazama wanafunzi wake, akasema, Heri ninyi mlio maskini, kwa
sababu ufalme wa Mungu ni wenu. Heri ninyi mlio na njaa sasa, kwa sababu mtashiba. Heri ninyi
mliao sasa, kwa sababu mtacheka. Heri ninyi watu watakapowachukia na kuwatenga, na kuwashutumu,
na kulitupa nje jina lenu kama neno ovu, kwa ajili ya Mwana wa Adamu. Furahiwani siku ile na
kuruka-ruka, kwa kuwa, tazama, thawabu yenu ni kubwa mbinguni; maana, baba zao waliwatenda
manabii vivyo hivyo. Lakini, ole wenu ninyi mlio na mali, kwa kuwa faraja yenu mmekwisha
kuipata. Ole wenu ninyi ambao mmeshiba sasa, kwa kuwa mtaona njaa. Ole wenu ninyi mnaocheka
sasa, kwa kuwa mtaomboleza na kulia. Ole wenu ninyi watu wote watakapowasifu, kwa kuwa baba
zao waliwatenda manabii wa uongo mambo kama hayo.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu wapendwa, kwa kuwa kila kitu kinao wakati wake
na mahali pake, tumwombe Mungu aliye asili ya hekima
yote.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Ili viongozi wetu wa Kanisa waongezewe ari ya kuihubiri
Injili, wakitoa heri na hata ole, ikibidi, ili kuuendeleza
unabii wa Mwanao Yesu Kristo. Ee Bwana.
2. Viongozi wetu wa serikali wajibidishe katika kutoa
huduma kwa jamii kwa wakati, kwani mambo ya ulimwengu huu
yanapita. Ee Bwana.
3. Uwaonye na kuwaangalisha walio na mali,
walioshiba na wanaocheka sasa, ili watumie vile
walivyonavyo kadiri ya mashauri ya Injili yako. Ee Bwana.
4. Utujalie sisi sote kutorudia maisha ya dhambi;
bali tuishi maisha mapya ya ufufuko na tujitenge
na maovu yaletayo ghadhabu yako. Ee Bwana.
5. Ndugu zetu marehemu wajaliwe uzima wa milele
huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetaka tumfuase Kristo aliye yote katika
yote, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya huyo Kristo
Bwana wetu. Amina.