JUMATANO JUMA 22 LA MWAKA WA 1
MASOMO

SOMO 1: Kol.1:1-8
Paulo, mtume wa Kristo Yesu kwa mapenzi ya Mungu, na Timotheo, ndugu yetu, kwa ndugu watakatifu, waaminifu katika Kristo, walioko Kolosai. Neema na iwe kwenu, na amani, zitokazo kwa Mungu Baba yetu. Twamshukuru Mungu, Baba yake Bwana wetu Yesu Kristo, siku zote tukiwaombea; tangu tuliposikia habari za imani yenu katika Kristo Yesu, na upendo mlio nao kwa watakatifu wote; kwa sababu ya tumaini mlilowekewa akiba mbinguni; ambalo habari zake mlizisikia zamani kwa neno la kweli ya Injili; iliyofika kwenu, kama ilivyo katika ulimwengu wote, na kuzaa matunda na kukua, kama inavyokua kwenu pia, tangu siku mlipoisikia mkaifahamu sana neema ya Mungu katika kweli; kama mlivyofundishwa na Epafra, mjoli wetu mpenzi, aliye mhudumu mwaminifu wa Kristo kwa ajili yenu; naye alitueleza upendo wenu katika Roho.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.52:8-9 (K)8
1. Bali mimi ni kama mzeituni Umeao katika nyumba ya Mungu. Nazitumainia fadhili za Mungu milele na milele.

(K) Nazitumainia fadhili za Mungu milele na milele.

2. Nitakushukuru milele kwa maana umetenda; Nitalingojea jina lako kwa kuwa ni jema; Mbele ya wacha Mungu wako. (K)

SHANGILIO: Yak.1:18
Aleluya, aleluya!
Kwa kupenda kwake mwenyewe alituzaa kwa neno lake la ukweli,
ili tuwe katika nafasi ya kwanza miongoni mwa viumbe vyake.
Aleluya!

INJILI: Lk.4:38-44
Yesu alitoka katika sinagogi, akaingia katika nyumba ya Simoni. Naye mkwewe Simoni, mamaye mkewe alikuwa ameshikwa na homa kali, wakamwomba kwa ajili yake. Akasimama karibu naye, akaikemea ile homa, ikamwacha; mara hiyo akaondoka, akawatumikia. Na jua lilipokuwa likichwa, wote waliokuwa na wagonjwa wenye maradhi mbalimbali waliwaleta kwake, akaweka mikono yake juu ya kila mmoja akawaponya. Pepo nao waliwatoka watu wengi, wakipiga kelele na kusema, Wewe u Mwana wa Mungu. Akawakemea, asiwaache kunena, kwa sababu walimjua kuwa ndiye Kristo. Hata kulipokucha alitoka akaenda mahali pasipokuwa na watu; makutano wakawa wakimtafuta-tafuta, wakafika kwake, wakataka kumzuia asiondoke kwao. Akawaambia, Imenipasa kuihubiri habari njema ya ufalme wa Mungu katika miji mingine pia; maana kwa sababu hiyo nalitumwa. Basi, alikuwa akihubiri katika masinagogi ya Galilaya.

--------------

--------------
MAOMBI
Ee Mungu, Habari Njema imefika kwetu. Kwa vile tunapaswa kuieneza ulimwenguni kote kwa maneno na matendo, tunaomba neema yako tukisema.

Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Ili Maaskofu na Mapadre wako wote waendelee kuwabariki watu wako na kuwatakia neema, amani na upendo toka kwako. Ee Bwana.

2. Viongozi wa serikali, vyama na taasisi mbalimbali hapa nchini wafanye kazi bila malumbano, wakijua kuwa wote ni wafanyakazi pamoja na Mungu, na kila mmoja atapata thawabu yake. Ee Bwana.

3. Ili hata pepo wamkiri Mwanao kuwa ndiye Kristo, na hivi kuturahisishia kazi ya utangazaji Injili kwa mataifa. Ee Bwana.

4. Ili imani tuliyoipokea kwa Mwano, na upendo tulionao kwa wenzetu vituimarishe katika tumaini la uzima tuliowekewa akiba mbinguni. Ee Bwana.

5. Ili wenye pepo waachwe huru, wagojwa wapone, wote wenye shida wasaidiwe; na marehemu wafikishwe mbinguni. Ee Bwana.

Ee Mungu uliyetaka Injili yako ikue, ienee na kuzaa matunda, uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.