JUMATANO JUMA 21 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 1The.2:9-13
Ndugu, mnakumbuka taabu yetu na masumbufu yetu; kwa kuwa mchana na usiku tulifanya kazi tusije
tukamlemea mtu wa kwenu awaye yote, tukawahubiri hivi Injili ya Mungu. Ninyi ni mashahidi, na
Mungu pia, jinsi tulivyokaa kwenu ninyi mnaoamini, kwa utakatifu, na kwa haki, bila kulaumiwa;
vile vile, kama mjuavyo, jinsi tulivyomwonya kila mmoja wenu kama baba awaonyavyo watoto wake
mwenyewe, tukiwatia moyo na kushuhudia; ili mwenende kama ilivyo wajibu wenu kwa Mungu, mwenye
kuwaita ninyi ili mwingie katika ufalme wake na utukufu wake. Kwa sababu hiyo sisi nasi twamshukuru
Mungu bila kukoma, kwa kuwa, mlipopata lile neno la ujumbe la Mungu mlilolisikia kwetu, mlilipokea
si kama neno la wanadamu, bali kama neno la Mungu; na ndivyo lilivyo kweli kweli; litendalo kazi
pia ndani yenu ninyi mnaoamini.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.139:7-12 (K)1
1. Niende wapi nijiepushe na roho yako?
Niende wapi niukimbie uso wako?
Kama ningepanda mbinguni, Wewe uko;
Ningefanya kuzimu kitanda changu, Wewe uko.
(K) Ee Bwana umenichunguza na kunijua.
2. Ningezitwaa mbawa za asubuhi,
Na kukaa pande za mwisho za bahari;
Huko nako mkono wako utaniongoza,
Na mkono wako wa kuume utanishika. (K)
3. Kama nikisema, Hakika giza litanifunika,
Na nuru inizungukayo ingekuwa usiku;
Giza nalo halikufichi kitu,
Bali usiku huangaza kama mchana; (K)
SHANGILIO: Yn.8:12
Aleluya, aleluya!
Mimi ndimi nuru ya ulimwengu,
asema Bwana,
yeye anifuataye hatakwenda gizani kamwe,
bali atakuwa na nuru ya uzima.
Aleluya!
INJILI: Mt.23:27-32
Yesu alisema, Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mmefanana na makaburi
yaliyopakwa chokaa, nayo kwa nje yaonekana kuwa mazuri, bali ndani yamejaa mifupa ya wafu,
na uchafu wote. Vivyo hivyo ninyi nanyi, kwa nje mwaonekana na watu kuwa wenye haki, bali
ndani mmejaa unafiki na maasi. Ole wenu, waandishi na Mafarisayo, wanafiki! Kwa kuwa mnayajenga
makaburi ya manabii, na kuyapamba maziara ya wenye haki, na kusema, Kama sisi tungalikuwako
zamani za baba zetu, hatungalishirikiana nao katika damu ya manabii. Hivi mwajishuhudia
wenyewe, ya kwamba ninyi ni wana wao waliowaua manabii. Kijazeni basi kipimo cha baba zenu.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, ni dhahiri kwamba tunahitaji msaada wa Mungu
ili neno lake lipate kutenda kazi ndani yetu sisi
tunaoamini. Tumwombe.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Kwa maombezi ya Mt. Yosefu, ulilinde Kanisa lako
dhidi ya kufuru, unafiki na maasi. Ee Bwana.
2. Viongozi wa serikali, waungane na viongozi wa
dini katika kuwaonya wahalifu, na kuwatia moyo
waadilifu, ili kujenga jamii isiyo na lawama yoyote. Ee Bwana.
3. Kila mmoja wetu aenende kama ilivyo wajibu wake
kwako Mungu, kwa utakatifu na haki, bila kumlemea mtu yeyote. Ee Bwana.
4. Tunawaombea wavivu wote, ili wajibidishe
kufanya kazi na kuzishika amri zako, wapate kula
matunda ya kazi zao. Ee Bwana.
5. Uwakirimie msamaha wa dhambi ndugu zetu marehemu
na kuwafikisha kwenye ufalme wako huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayetualika kukijaza kipimo cha wema wa
baba zetu, uyapokee maombi haya. Kwa njia ya Kristo
Bwana wetu. Amina.