JUMATANO JUMA 20 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Amu.9:6-15
Watu wote wa Shekemu walikusanyika pamoja, na jamaa yote ya Milo, wakaenda na kumtawaza Abimeleki
awe mfalme, karibu na huo mgandi ulio karibu na ngome iliyo katika Shekemu. Kisha walipomwambia
huyo Yothamu, yeye akaenda, akasimama juu ya kilele cha kilima cha Gerizimu, akapaza sauti yake,
akapiga kelele, na kuwaambia: Nisikieni mimi, enyi watu wa Shekemu, ili kwamba Mungu naye apate
kuwasikia ninyi. Siku moja miti ilitoka ili kuutia mmoja mafuta uwe mfalme juu yao; ikauambia mti
mzeituni, Tawala wewe juu yetu. Lakini huo mzeituni ukaiambia, Je! Niache mafuta yangu, ambayo
kwangu mimi watu wamheshimu Mungu na wanadamu, ili niende nikayongeyonge juu ya miti? Kisha miti
ikauambia mtini, Njoo wewe, utawale juu yetu. Lakini huo mtini ukaiambia, Je! Niuache utamu wangu,
na matunda yangu mazuri, niende nitayonge-yonge juu ya miti? Kisha miti ikauambia mzabibu, Njoo wewe,
utawale juu yetu. Huo mzabibu nao ukaiambia, Je! Niiache divai yangu, ambayo humfurahisha Mungu na
wanadamu, ili niende nikayonge-yonge juu ya miti? Ndipo hiyo miti yote ikauambia mti wa miiba, Njoo
wewe, utawale juu yetu. Huo mti wa miiba ukaiambia miti, Kwamba ninyi mwanitia mafuta niwe mfalme
juu yenu kwelikweli, basi njoni mtumaini kivuli changu; na kwamba sivyo, na utoke moto katika mti
wa miiba na kuitekete mierezi ya Lebanoni.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.21:1–6 (K)1
1. Ee Bwana, mfalme atazifurahia nguvu zako,
Na wokovu wako ataufanyia shangwe nyingi sana.
Umempa haja ya moyo wake,
Wala hukumzuilia matakwa ya midomo yake.
(K) Ee Bwana, mfalme atazifurahia nguvu zako.
2. Maana umesogezea Baraka za heri,
Umemvika taji ya dhahabu safi kichwani pake.
Alikuomba uhai, ukampa.
Muda mrefu wa siku nyingi, milele na milele. (K)
3. Utukufu umemsogezea Baraka za heri,
Umemvika taji ya dhahabu safi kichwani pake.
Alikuomba uhai, ukampa.
Muda mrefu wa siku nyingi, milele na milele. (K)
SHANGILIO: Zab.119:18
Aleluya, aleluya!
Unifumbue macho yangu niyatazame
maajabu yatokayo katika sheria yako.
Aleluya!
INJILI: Mt.20:1-16
Yesu aliwaambia wafuasi wake: Ufalme wa mbinguni umefanana na mtu mwenye nyumba aliyetoka
alfajiri kwenda kuajiri wakulima awapeleke katika shamba lake la mizabibu. Naye alipokwisha
kupatana na wakulima kuwapa kutwa dinari, aliwapeleka katika shamba lake la mizabibu. Akatoka
mnamo saa tatu, akaona wengine wamesimama sokoni wasiokuwa na kazi; na hao nao akawaambia,
Enendeni nanyi katika shamba langu la mizabibu, na iliyo haki nitawapa. Wakaenda. Akatoka
tena mnamo saa sita na saa kenda, akafanya vile vile. Hata kama saa kumi na moja akatoka,
akakuta wengine wamesimama, akawaambia, Mbona mmesimama hapa mchana kutwa bila kazi? Wakamwambia,
Kwa sababu hakuna mtu aliyetuajiri. Akawaambia, enendeni nanyi katika shamba la mizabibu.
Kulipokuchwa, yule bwana wa shamba akamwambia msimamizi wake, Waite wakulima, uwalipe ujira
wao, ukianzia wa mwisho hata wa kwanza. Na walipokuja wale wa saa kumi na moja, walipokea kila
mtu dinari. Na wale wa kwanza walipokuja, walidhani kwamba watapokea zaidi; na hao pia wakapokea
kila mtu dinari. Basi wakiisha kuipokea, wakamnung'unikia mwenye nyumba, wakisema, Hao wa mwisho
wametenda kazi saa moja tu, nawe umewasawazisha na sisi tuliostahimili taabu na hari za mchana
kutwa. Naye akamjibu mmoja wao, akamwambia, Rafiki, sikudhulumu; hukupatana nami kwa dinari?
Chukua iliyo yako, uende zako; napenda kumpa huyu wa mwisho sawa na wewe. Si halali yangu
kutumia vilivyo vyangu kama nipendavyo? Au jicho lako limekuwa ovu kwa sababu ya mimi kuwa
mwema? Vivyo hivyo wa mwisho watakuwa wa kwanza, na wa kwanza watakuwa wa mwisho.
--------------
--------------
MAOMBI
Wapendwa, sisi sote ni wafanyakazi katika shamba la
Bwana tunaotegemewa kuzaa matunda mazuri mfano
wa mzeituni, mtini na mzabibu. Tunahitaji msaada wa
Mungu aliyetukabidhi kazi hiyo. Basi, tumwombe.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Umkirimie Askofu wetu F. watenda kazi wengi
zaidi, wenye bidii, uaminifu na ushirikiano, ili jimbo
letu liweze kustawi vizuri zaidi kimwili na kiroho. Ee Bwana.
2. Uikinge dunia yetu na hila za watu hatari, wenye uchu
wa madaraka na wasio na nia njema kwa watu wako. Ee Bwana.
3. Viongozi wetu wa dini na wa serikali wazidi kuhamasisha
huduma za kijamii hasa kwa wagonjwa, walemavu, wenye njaa,
wasafiri, wakimbizi, wafungwa na wote wenye shida. Ee Bwana.
4. Uwahurumie na kuwainua wasio na ajira na wenye
kipato kidogo; nasi sote tujaliwe kutimiza wajibu zetu
vizuri na kuzaa matunda yaliyokusudiwa. Ee Bwana.
5. Kwa huruma yako, uwape uzima wa milele ndugu
zetu marehemu. Ee Bwana.
Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Yesu, Bwana na
Mungu wetu daima na milele. Amina.