JUMATANO JUMA 19 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kum.34:1-12
Musa alipanda kutoka uwanda wa Moabu mpaka mlima Nebo, hata kilele cha Pisga kukabili Yeriko. Bwana
akamwonyesha nchi yote ya Galiadi hata Dani; na Naftali yote, na nchi ya Efraimu na Manase, na nchi
yote ya Yuda, mpaka bahari ya magharibi; na Negebu, na uwanja wa bonde la Yeriko, mji wa mitende,
hata mpaka Soari. Bwana akamwambia, Hii ndiyo nchi niliyowaapia Ibrahimu, na Isaka, na Yakobo,
nikisema, Nitawapa wazao wako. Basi nimekuonyesha kwa macho yako, lakini hutavuka huko. Basi Musa,
mtumishi wa Bwana, akafa huko, katika nchi ya Moabu, kwa neno la Bwana. Akamzika bondeni, katika
nchi ya Moabu, kukabili Beth-peori; lakini hapana mtu ajuaye kaburi lake hata leo. Musa alikuwa mtu
wa miaka mia na ishirini alipokufa; jicho lake halikupofuka, wala nguvu za mwili wake hazipunguka.
Wana wa Israeli wakamwomboleza Musa katika uwanda wa Moabu siku thelathini; basi siku za maombolezo
ya matanga ya Musa zikaisha. Na Yoshua. mwana wa Nuni, alikuwa amejaa roho ya hekima; maana Musa
alikuwa amemwekea mikono yake juu yake; wana wa Israeli wakamsikiliza, wakafanya kama Bwana
alivyowamuru Musa. Musa, hajainuka tena katika Israeli nabii kama Musa, ambaye Bwana alimjua uso
kwa uso; katika ishara zote na maajabu yote, ambayo Bwana alimtuma kuyatenda katika nchi ya Misri,
kwa Farao, na kwa watumishi wake wote, na kwa nchi yake yote; na katika ule mkono wa nguvu wote,
katika ule utisho mkuu wote, alioutenda Musa machoni pa Israeli wote.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.66:1-3,5,8,16-17 (K)20:9
1. Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote,
imbeni utukufu wa jina lake,
tukuzeni sifa zake.
Mwambieni Mungu: Matendo yako yatisha kama nini.
(K) Ahimidiwe Mungu, aliyeweka nafsi yetu katika uhai.
2. Njani yatazameni matendo ya Mungu,
Hutisha kwa mambo awetendayo wanadamu.
Enyi mataifa, mtukuzeni Munug wetu,
itangazeni sauti ya sifa zake. (K)
3. Njoni sikieni, ninyi nyotc mnaomcha Mungu,
nami nitayatangaza alivyonitendea roho yangu.
Nalimwita kwa kinywa changu,
na sifa kuu zilikuwa chini ya ulimi wangu. (K)
SHANGILIO: 2Kor.5:19
Aleluya, aleluya!
Mungu alikuwa ndani ya Kristu,
akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake
ametia ndani yetu neno la upatanisho.
Aleluya!
INJILI: Mt.18:15-20
Yesu aliwaambia wanafunzi wake: Ndugu yako akikukosa, enenda ukamwonye, wewe na yeye peke
yenu; akikusikia, umempata nduguyo. La, kama hasikii, chukua pamoja nawe tena mtu mmoja au
wawili, ili kwa vinywa vya mashahidi wawili au watatu kila neno lithibitike. Na asipowasikiliza
wao, liambie kanisa; na asipolisikiliza kanisa pia, na awe kwako kama mtu wa mataifa na mtoza
ushuru. Amin, nawaambieni, yo yote mtakayoyafunga duniani yatakuwa yamefungwa mbinguni; na yo
yote mtakayoyafungua duniani yatakuwa yamefunguliwa mbinguni. Tena nawaambia, ya kwamba wawili
wenu watakapopatana duniani katika jambo lo lote watakaloliomba, watafanyiwa na Baba yangu
aliye mbinguni. Kwa kuwa walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina langu, nami nipo papo
hapo katikati yao.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu, Mwanao Yesu Kristo ametuhakikishia kuwa
walipo wawili watatu wamekusanyika kwa jina lake, naye
yupo papo hapo katikati yao. Basi, tunakuomba:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Uwajalie afya na nguvu Baba Mtakatifu na Maaskofu
wetu wote; uwakirimie roho ya hekima, wapate kulichunga
vema kundi lako. Ee Bwana.
2. Uwajalie daima watu wako viongozi waadilifu na
wenye bidii, ili wasibaki kama kondoo wasio na mchungaji.
Ee Bwana.
3. Umjalie kila mmoja wetu busara katika kutatua matatizo
yanayojitokeza katika jamii zetu; ili haki itendeke
na upendo wa kweli utawale jumuiya zetu. Ee Bwana.
4. Usikilize dua za watu wanaougua na kulia kwa
sababu ya machukizo yote yanayofanyika duniani;
na uwaokoe wazee, vijana na watoto wanaokutumainia. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wasamehewe dhambi zao na kuurithi
uzima wa milele. Ee Bwana.
Ee Mungu, tunaamini kuwa wanaopatana duniani katika jambo lolote
wanaloliomba kwako watafanyiwa. Uyapokee maombi yetu kwa njia ya
Kristo Bwana wetu. Amina.