JUMATANO JUMA 17 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kut.34:29-35
Hata ikawa, Musa aliposhuka katika mlima Sinai, na ztie mbao mbili za ushuhuda zilikuwa mkononi
mwa Musa, hapo aliposhuka katika mlima, Musa hakujua ya kuwa ngozi ya uso wake iling’aa kwa sababu
amesema na Bwana. Basi Haruni na wana wote wa Israeli walipomwona Musa, tazama, ngozi ya uso wake
iling’aa; nao wakaogopa kumkaribia. Musa akawaita; Haruni na wakuu wote wa kusanyiko wakarudi
kwake; Musa akasema nao. Baadaye wana wa Israeli wote wakakaribia; akawausia maneno yote ambayo
Bwana amemwambia katika mlima Sinai. Na Musa alipokuwa amekwisha kusema nao, akatia utaji juu ya
uso wake. Lakini desturi ya Musa ilikuwa alipoingia mbele za Bwana kusema naye, kuuvua huo utaji
mpaka atoke; akatoka akawaambia wana wa Israeli maneno yote aliyoambiwa. Wana wa Israeli wakauona
uso wa Musa ya kuwa ngozi ya uso wake Musa iling’aa; naye Musa akautia utaji juu ya uso wake tena,
hata alipoingia kusema naye.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.99:5-7,9 (K)9
1. Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu,
sujuduni penye kiti cha miguu yake, ndiye mtakatifu.
(K) Bwana, Mungu wetu, ndiye mtakatifu.
2. Musa na Haruni miongoni mwa makuhani wake,
na Samweli miongoni mwao waliitiao jina lake,
walipomwita Bwana aliwaitikia. (K)
3. Katika nguzo ya wingu alikuwa akisema nao.
Walishika shuhuda zake na amri aliyowapa. (K)
4. Mtukuzeni Bwana, Mungu wetu,
sujuduni mkiukabili mlima wake mtakatifu,
maana Bwana, Mungu wetu, ndiye mtakatifu. (K)
SHANGILIO: Yak.1:18
Aleluya, aleluya!
Kwa kupenda kwake mwenyewe,
Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli,
tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya!
INJILI: Mt.13:44-46
Yesu aliwaambia makutano mifano, Ufalme wa mbinguni umefanana na hazina iliyositirika katika
shamba; ambayo mtu alipoiona, aliificha; na kwa furaha yake akaenda akauza alivyo navyo vyote
akalinunua shamba lile. Tena ufalme wa mbinguni umefanana na mfanya biashara, mwenye kutafuta
lulu nzuri; naye alipoona lulu moja ya thamani kubwa, alikwenda akauza alivyo navyo vyote
akainunua.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu uliyempa Musa kibali cha kuongea nawe, uso
kwa uso, twakuomba:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Ulimwengu wote uonje uwepo wa Mwanao Yesu
Kristo, Kichwa cha Kanisa, katika nafsi ya Papa wetu
F. Ee Bwana.
2. Uongee hata na watawala wa dunia, wapate kukukiri
Wewe Mungu na kuona umuhimu wa kuruhusu na
kuuheshimu uhuru wa kukuabudu. Ee Bwana.
3. Utuwezeshe sisi sote kudumu katika imani uliyotujalia,
tupate kuumiliki ufalme wako ambao ni kama
hazina au lulu nzuri. Ee Bwana.
4. Tunawaombea wote wenye shida za pekee,
wasikate tamaa; bali neno lako liwe kwao chakula
cha kila siku, liwape furaha na shangwe ya mioyo
yao; kwani Wewe umewaita kwa jina lako. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wasemehewe dhambi zao na kuuona
uso wako mtukufu. Ee Bwana.
Ee Mungu, uliyesema na wana wa Israeli, uyapokee
maombi yetu kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.