JUMATANO JUMA 16 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kut.16:1-5,9-15
Walisafiri kutoka Elimu, na mkutano wote wa wana wa Israeli wakafikilia bara ya Sini, iliyoko kati
ya Elimu na Sinai, siku ya kumi na tano ya mwezi wa pili baada ya kutoka kwao nchi ya Misri. Na mkutano
mzima wa wana wa Israeli ukawanung’unikia Musa na Haruni, huko barani; wana wa Israeli wakawaambia,
Laiti tungalikufa kwa mkono wa Bwana katika nchi ya Misri, hapo tulipoketi karibu na zile sufuria za
nyama, tulipokula vyakula hata kushiba; kwani mmetutoa huko na kututia katika bara hii, ili kutuua
kwa njaa kusanyiko hili lote. Ndipo Bwana akamwambia Musa, Tazama, mimi nitawanyeshea ninyi mvua ya
mkate kutoka mbinguni; na hao watu watatoka nje na kuokota kila siku sehemu ya siku; ili nipate
kuwajaribu, kwamba watakwenda katika sheria yangu, ama sivyo. Kisha itakuwa siku ya sita, ya kwamba
watayaandaa hayo watakayoleta ndani, nayo yatakuwa ni mara mbili kuliko wayaokotayo kila siku. Musa
akamwambia Haruni, Haya, sema na mkutano wote wa wana wa Israeli. Njoni karibu mbele ya Bwana; kwa
kuwa yeye ameyasikia manung’uniko yetu. Ilikuwa Haruni aliponena na huo mkutano wote wa wana wa Israeli,
wakaangalia upande wa bara, na tazama, utukufu wa Bwna ukaonekana katika hilo wingu. Bwana akasema na
Musa, akinena, Nimeyasikia manung’uniko ya wana wa Israeli; haya! Sema nao, ukinena, Wakati wa jioni
mtakula nyama, na wakati wa asubuhi mtashiba mkate; nanyi mtajua ya kuwa mimi ndimi Bwana, Mungu wenu.
Ikawa wakati wa jioni; kware wakakaribia, wakakifunikiza kituo; na wakati wa asubuhi umande ulikuwa
juu ya nchi pande zote za kituo. Na ulipoinuka ule umande uliokuwa juu ya nchi, kumbe! Juu ya uso wa
bara kitu kidogo kilichoviringana, kidogo kama sakitu juu ya nchi. Wana wa Israeli walipokiona,
wakaambiana, Nini hiki? Maana hawakujua ni kitu gani. Musa akawaambia, Ndio mkate ambao Bwana amewapa
ninyi, mle.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.78:18-19,23-28 (K)24
1. Wakamjaribu Mungu mioyoni mwao
Kwa kutaka chakula kwa tamaa zao.
Naam, walimwambia Mungu, wakasema,
Je! Mungu aweza kuandika meza jangwani?
(K) Bwana aliwapa nafaka ya mbinguni.
2. Lakini aliyaamuru mawingu juu;
Akaifungua milango ya mbinguni;
Akawanyeshea mana ili wale;
Akawapa nafaka ya mbinguni. (K)
3. Mwanadamu akala chakula cha mashujaa;
Aliwapelekea chakula cha kuwashibisha.
Aliuelekeza upepo wa mashariki mbinguni;
Akaiongoza kusi kwa uweza wake. (K)
4. Akawanyeshea nyama kama mavumbi,
Na ndege wenye mbawa,
Kama mchanga wa bahari.
Akawaangusha kati ya matuo yao,
Pande zote za maskani zao. (K)
SHANGILIO:
Aleluya, aleluya!
Mbegu ni neno la Mungu, anayepanda ni Kristu,
atakayemkuta, ataishi milele.
Aleluya!
INJILI: Mt.13:1-9
Yesu alitoka nyumbani, akaketi kando ya bahari. Wakamkusanyikia makutano mengi, hata akapanda
chomboni, akaketi; na ule mkutano wote wakasimama pwani. Akawaambia mambo mengi kwa mifano,
akisema, Tazama, mpanzi alitoka kwenda kupanda. Hata alipokuwa akipanda, mbegu nyingine
zilianguka karibu na njia, ndege wakaja wakazila; nyingine zikaanguka penye miamba, pasipokuwa
na udongo mwingi; mara zikaota, kwa udongo kukosa kina; na jua lilipozuka ziliungua; na kwa
kuwa hazina mizizi zikanyauka. Nyingine zikaanguka penye miiba; ile miiba ikamea, ikazisonga;
nyingine zikaanguka penye udongo mzuri, zikazaa, moja mia, moja sitini, moja thelathini. Mwenye
masikio na asikie.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, ingawa twajua vema kuwa mtu hataishi kwa
mkate tu, ila kwa kila neno litokalo katika kinywa cha
Mungu, bado tunahitaji neema ya Mungu ili neno lake
lipate kuzaa matunda yaliyokusudiwa. Tuombe:-
Kiitikio: Pokea ombi letu.
1. Umjalie Baba Mtakatifu wetu F., na viongozi wote
wa Kanisa amani na utulivu, wapate kulihubiri
kwa ufasaha neno lako, na kuwaokoa wote
wanaolipokea neno hilo kwa imani. Ee Bwana.
2. Wote wenye madaraka serikalini na katika taasisi
mbalimbali wajaliwe moyo wa huruma kwa watu
wao; na watumie kiaminifu mali wanazopewa kwa
ajili ya walengwa. Ee Bwana.
3. Utujalie mazingira bora yatakayotuwezesha kulipokea
vema neno lako na kulielewa vizuri. Ee Bwana.
4. Utujalie kuipokea sauti yako inayotuita kuishi miito
uliyotujalia tangu tumboni mwa mama zetu, bila
masharti na bila kufuata mkumbo. Ee Bwana.
5. Ndugu zetu marehemu wasamehewe dhambi zao na
kupewa uzima wa milele huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu unayesikiliza sala za wale wanaokulilia,
uyapokee maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Amina.