JUMATANO JUMA 15 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Kut.3:1-6,9-12
Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya jangwa,
akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto uliotoka
katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! Kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea. Musa
akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. Bwana alipoona
ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa! Musa!
Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali hapa
unaposimama ni nchi takatifu. Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa
Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu. Bwana
akasema: Tazama, kilio cha wana wa Israeli kimenifikilia; tena nimeyaona hayo mateso ambayo Wamisri
wanawatesa. Haya, basi, nitakutuma sasa kwa Farao, nikawatoe wana wa Israeli watoke Misri? Akasema,
Bila shaka mimi nitakuwa pamoja nawe; na dalili ya kuwa nimekutuma ndiyo hii; utakapokuwa umekwisha
kuwatoa hao watu katika Misri, mtamwabudu Mungu katika mlima huu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.103:1-4,6-7 (K)8
1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Naam vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K) Bwana amejaa huruma na neema.
2. Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote.
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema. (K)
3. Bwana ndiye afanyaye mambo ya haki,
Na hukumu kwa wote wanaoonewa.
Akimjulisha Musa njia zake,
Wana wa Israeli matendo yake. (K)
SHANGILIO: Zab.19:8
Aleluya, aleluya!
Amri ya Bwana ni safi,
huyatia macho nuru.
Aleluya!
INJILI: Mt.11:25-27
Wakati ule Yesu alijibu akasema, Nakushukuru, Baba, Bwana wa mbingu na nchi, kwa kuwa mambo
haya uliwaficha wenye hekima na akili, ukawafunulia watoto wachanga. Naam, Baba, kwa kuwa
ndivyo ilivyopendeza mbele zako. Akasema, Nimekabidhiwa vyote na baba yangu; wala hakuna
amjuaye Mwana, ila Baba; wala hakuna amjuaye Baba, ila Mwana, na yenyote ambaye Mwana apenda
kumfunulia.
--------------
--------------
MAOMBI
Ee Mungu uliyemwambia Musa: “Mimi ni Mungu wa
baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka na
Mungu wa Yakobo, "twakuomba:-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Umjalie Askofu wetu F. na Mapadre wote kudumu
katika kutimiza kiaminifu viapo vyao vya utii; na hivi
kuwa tayari kuwahudumia kondoo wako kwa upendo
usio na dosari. Ee Bwana.
2. Watawala wa dunia wajaliwe hekima na akili ya
kukujua na kukuogopa Wewe Mungu wa kweli, na
Mwanao wa pekee, Yesu Kristo uliyemtuma kwetu.
Ee Bwana.
3. Utujalie unyenyekevu kama ule wa watoto wachanga,
tupate kulipokea neno lako kwa moyo unyofu
na kuliishi kwa hekima na akili. Ee Bwana.
4. Uwahurumie wenye makosa mazito; ghadhabu
yako isianguke juu yao; bali uwaamshie moyo wa
toba wapate kuirudia njia iliyo sawa. Ee Bwana.
5. Marehemu wetu wapokelewe nyumbani Mwako,
wapate kukusifu na kukushukuru milele. Ee Bwana.
Ee Baba, Bwana wa mbingu na nchi, uyapokee maombi
yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.