JUMATANO JUMA 14 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Mwa.41:55-57;42:5-7,17-24
Nchi yote ya Misri ilipoona njaa, watu walilia Farao awape chakula. Farao akawaambia Wamisri wote,
Enendeni kwa Yusufu; atakavyowaambia, fanyeni. Njaa ikawa katika dunia yote pia. Yusufu akazifungua
ghala zote, akawauzia Wamisri. Njaa ikawa nzito katika nchi ya Misri. Watu wa nchi zote wakaja Misri
kwa Yusufu; ili wanunue nafaka; kwa sababu njaa imekuwa nzito katika dunia yote. Wana wa Israeli
wakaja wanunue chakula miongoni mwao waliokuja, kwa kuwa kulikuwa na njaa katika nchi ya Kanaani.
Naye Yusufu alikuwa ni liwali juu ya nchi, ndiye aliyewauzia watu wote wa nchi. Nao ndugu zake
Yusufu wakaja, wakainama kifudifudi mbele yake. Yusufu akawaona nduguze akawatambua, lakini
alijifanya kama mgeni kwao. Akasema nao kwa maneno makali, akawaambia, Mmetoka wapi ninyi? Wakasema,
Tumetoka nchi ya Kanaani, ili tununue chakula. Akawatia wote gerezani siku tatu. Yusufu akawaambia
siku ya tatu, Fanyeni hivi, mkaishi, maana mimi namcha Mungu. Kama ni wa kweli ninyi, ndugu yenu
mmoja na afungwe gerezani, nanyi nendeni mkachukue nafaka kwa njaa ya nyumba zenu, mkamlete ndugu
yenu mdogo kwangu; hivyo maneno yenu yatahakikishwa, wala hamtakufa. Ndivyo walivyofanya.
Wakaambiana, Kweli sisi tulimkosa ndugu yetu, kwa kuwa tuliona shida ya roho yake, alipotusihi,
wala hatukusikia; kwa hiyo shida hii imetupata. Reubeni akajibu, akawaambia, Sikuwaambia, nikisema,
msimkose kijana? Wala hamkusikia; kwa hiyo damu yake inatakwa tena. Wala hawakujua ya kwamba Yusufu
anawasikia, kwa sababu alikuwapo mkalimani kati yao. Akajitenga nao akalia. Kisha akawarudia, na
kusema nao, akamtwaa Simeoni miongoni mwao, akamfunga mbele ya macho yao.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.33:1-2,10-11,18-19 (K)22
1. Mpigieni Bwana vigelegele, enyi wenye haki,
kusifu kunawapasa wanyofu wa moyo.
Mshukuruni Bwana kwa kinubi,
Kwa kinanda cha nyuzi kumi mwimbieni sifa.
(K) Ee Bwana fadhili zako zikae nasi,
kama vile tulivyokungoja Wewe.
2. Bwana huyabatilisha mashauri ya mataifa,
huyatangua makusudi ya watu.
Shauri la Bwana lasimama milele,
makusudi ya moyo wake vizazi na vizazi. (K)
3. Tazama jicho la Bwana li kwa wamchao
Wazingojeao fadhili zake.
Yeye huwaponya nafsi zao na mauti
na kuwahuisha wakati wa njaa. (K)
SHANGILIO: Kol.3:16,17
Aleluya, aleluya!
Neno la Kristo likae kwa wingi
ndani yenu katika hekima yote,
mkishukuru Mungu Baba kwa Yeye.
Aleluya!
INJILI: Mt.10:1-7
Yesu aliwaita wanafunzi wake kumi na wawili, akawapa amri juu ya pepo wachafu, wawatoe, na
kupoza magonjwa yote na udhaifu wa kila aina. Na majina ya hao mitume kumi na wawili ni haya;
Wa kwanza Simoni aliyeitwa Petro, na Andrea nduguye; Yakobo wa Zebedayo, na Yohane nduguye;
Filipo, na Bartholomayo; Tomaso, na Mathayo mtoza ushuru; Yakobo wa Alfayo, na Thadayo; Simoni
Mkananayo, na Yuda Iskariote, naye ndiye mwenye kumsaliti. Hao Thenashara Yesu aliwatuma,
akawaagiza, akisema. Katika njia ya Mataifa msiende, wala katika mji wowote wa Wasamaria msiingie.
Afadhali shikeni njia kuwaendea kondoo waliopotea wa nyumba ya Israeli. Na katika kuenenda kwenu,
hubirini, mkisema, Ufalme wa mbinguni umekaribia.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, kwa Ubatizo sisi sote tumeitikia wito wa kuwa
watangazaji wa Injili. Kwa vile sisi ni viumbe dhaifu
na kazi hiyo si rahisi hivi, tuombe msaada wa Mungu
tukisema.
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Upende kumlinda Askofu wetu F. na wote
uliowateua kuirithi kazi ya mitume. Ee Bwana.
2. Ubariki juhudi za viongozi wetu wa serikali na wa
taasisi mbalimbali katika kutafuta ufumbuzi wa mata-
tizo ya njaa, ajira na yote yanayozikera jamii zetu. Ee
Bwana.
3. Watu wote duniani watambue kuwa sasa wakati
umewadia wa kukutafuta Wewe, hata utakapokuja
na kuwanyeshea haki. Ee Bwana.
4. Kila mmoja wetu aitikie kwa vitendo wito wa kuwa
mtangazaji wa msamaha, upendo wa kidugu na Habari
Njema ya wokovu kwa watu wote. Ee Bwana.
5. Ufalme wako uwafikie kwa namna ya pekee ndugu
zetu marehemu tuliowapenda na kuwategemea
kimwili na kiroho. Ee Bwana.
Ee Mungu unayewapa watu wako mahitaji ya kimwili
na kiroho kwa namna ya ajabu, uyapokee maombi yetu.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.