JUMATANO JUMA 13 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: Mwa.21:5,8-20
Ibrahimu alikuwa mtu wa miaka mia, alipozaliwa mwana wake Isaka. Mtoto akakua, akaachishwa kunyonya;
Ibrahimu akafanya karamu kuu siku ile Isaka alipoachishwa kunyonya. Sara akamwona yule mwana wa Hajiri
Mmisri, ambaye alimzalia Ibrahimu, anafanya dhihaka. Kwa hiyo akamwambia Ibrahimu, Mfukuze mjakazi
huyu na mwanawe, maana mwana wa mjakazi hatarithi pamoja na mwanangu, Isaka. Na neno hilo lilikuwa
baya sana machoni pa Ibrahimu, kwa ajili ya mwanawe. Mungu akamwambia Ibrahimu, Neno hili lisiwe
baya machoni pako, kwa ajili ya huyo mwana, na huko mjakazi wako. Kila akuambialo Sara, sikiza
sauti yake, kwa maana katika Isaka uzao wako utaitwa. Naye mwana wa mjakazi nitamfanya kuwa taifa,
maana huyu naye ni uzao wako. Ibrahimu akaamka asubuhi na mapema akatwaa mkate na kiriba cha maji,
akampa Hajiri akimtwika begani pake, na kijana, akamruhusu; naye akatoka, akapotea katika jangwa
la Beer-sheba. Yale maji yakaishaisha katika kiriba, akamlaza kijana chini ya kijiti kimoja. Akaenda
akakaa akimkabili, mbali i kadiri ya mtupo wa mshale; maana alisema, Nisimwone kijana akifa; naye
akakaa akimkabili, akapazaza sauti yake, akalia. Mungu akasikia sauti ya kijana. Malaika wa Mungu
akamwita Hajiri kutoka mbinguni, akamwambia, Una nini, Hajiri? Usiogope, maana Mungu amesikia sauti
ya kijana huko aliko. Ondoka, ukamwinue kijana, ukamshike mkononi mwako, kwa kuwa nitamfanya kuwa
taifa kubwa. Mungu akamfumbua macho, naye akaona kisima cha maji; akaenda akakijaza kiriba maji,
akamnywesha kijana. Mungu akawa pamoja na huyo kijana, naye akakua, akakaa katika jangwa, akawa
mpiga upinde.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.34:6-7,9-13 (K)6
1. Maskini huyu aliita, Bwana akasikia,
Akamwokoa na taabu zake zote.
Malaika wa Bwana hufanya kituo,
akiwazungukia wamchao na kuwaokoa.
(K) Maskini huyu aliita, Bwana akasikia.
2. Mcheni Bwana, enyi watakatifu wake,
yaani, wamchao hawahitaji kitu.
Wana-simba hutindikiwa, huona njaa,
bali wamtafutao Bwana hawatahitaji kitu
chochote kilicho chema. (K)
3. Njoni, enyi wana, mnisikilize,
nami nitawafundisha kumcha Bwana.
Ni nani mtu yule apcndezwaye na uzima,
apendaye siku nyingi apate kuona mema? (K)
SHANGILIO: Zab.119:105
Aleluya, aleluya!
mungu alikuwa ndani ya Kristu,
Neno lako ni taa ya miguu yangu,
na mwanga wa njia yangu.
Aleluya!
INJILI: Mt.8:28-34
Yesu alipofika ng’ambo katika nchi ya Wagerasi, watu wawili wenye pepo walikutana naye, wanatoka
makaburini, wakali mno, hata mtu asiweze kuipitia njia ile. Na tazama, wakapiga kelele, wakisema,
Tuna nini nawe, Mwana wa Mungu? Je! Umekuja kututesa kabla ya muhula wetu? Basi, kulikuwako mbali
nao kundi la nguruwe wengi wakilisha. Wale pepo wakamsihi, wakisema, Ukitutoa, tuache twende,
tukaingie katika lile kundi la nguruwe. Akawaambia, Nendeni. Wakatoka, wakaingia katika nguruwe;
na kumbe! Kundi lote wakatelemka kwa kasi gengeni hata baharini, wakafa majini. Lakini wachungaji
walikimbia, wakaenda zao mjini, wakazieneza habari zote, na habari za wale wenye pepo pia. Na
tazama, mji wote ukatoka kwenda kumlaki Yesu; nao walipomwona, walimsihi aondoke mipakani mwao.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, si rahisi kuitekeleza amri ya mapendo kwa jirani,
hasa pale zinapokuwepo tofauti baina ya wahusika, mintarafu
uzao wa damu na usio wa damu. Tuombe neema ya Mungu tukisema:-
Kiitikio: Twakuomba utusikie.
1. Uwajalie Maaskofu na Mapadre wetu kushirikiana
vema zaidi na watenda kazi wao, bila ubaguzi
wa aina yoyote. Ee Bwana.
2. Wote wenye mamlaka wajaliwe roho ya kugawa
madaraka na raslimali zilizopo, kwa njia za haki
na amani bila upendeleo wowote ule. Ee Bwana.
3. Utujalie upendo wa kweli unaothamini na kuenzi
zaidi uhai wa binadamu wenzetu, kuliko kitu
kingine chochote. Ee Bwana.
4. Kila mmoja wetu ajibidishe kutafuta mema, wala si
mabaya; kwani Wewe hupendezwi na ibada ya
unafiki isiyoandamana na matendo mema. Ee Bwana.
5. Uwahurumie wagonjwa, wazee, wageni, yatima,
wajane na wote wasiojiweza. Nao marehemu wetu
wafikishwe mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu uliyetuamshia mapendo ya kweli, uyapokee
maombi yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.