JUMATANO JUMA 11 LA MWAKA WA 1
MASOMO
SOMO 1: 2Kor.9:6–11
Nasema neno hili, Apandaye haba atavuna haba; apandaye kwa ukarimu atavuna kwa ukarimu. Kila mtu
na atende kama alivyokusudia moyoni mwake, si kwa huzuni, wala si kwa lazima; maana Mungu humpenda
yeye atoaye kwa moyo wa ukunjufu. Na Mungu aweza kuwajaza kila neema kwa wingi, ili ninyi, mkiwa
na riziki za kila namna siku zote, mpate kuzidi sana katika kila tendo jema; kama ilivyoandikwa,
Ametapanya, amewapa maskini, haki yakaa milele. Na yeye ampaye mbegu mwenye kupanda, na mkate uwe
chakula, atawapa mbegu za kupanda na kuzizidisha, naye atayaongeza mazao ya haki yenu; mkitajirishwa
katika vitu vyote mpate kuwa na ukarimu wote, umpatiao Mungu shukrani kwa kazi yetu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.112:1–2,4–9 (K)1
1. Heri mtu yule amchaye Bwana,
Apendezwaye sana na maagizo yake.
Wazao wake watakuwa hodari duniani;
Kizazi cha wenye adili kitabarikiwa.
(K) Heri mtu yule amchaye Bwana.
2. Nuru huwazukia wenye adili gizani;
Ana fadhili na huruma na haki. (K)
3. Amekirimu, na kuwapa maskini,
Haki yake yakaa milele,
Pembe yake itatukuzwa kwa utukufu.(K)
SHANGILIO: Yak.1:18
Aleluya, aleluya!
Kwa kupenda kwake mwenyewe,
Baba alituzaa sisi kwa neno la kweli,
tuwe kama limbuko la viumbe vyake.
Aleluya!
INJILI: Mt.6:1-6,16-18
Yesu aliwaambia wanafunzi wake; Angalieni msifanye wema wenu machoni pa watu, kusudi mtazamwe
na wao; kwa maana mkifanya kama hayo, hampati thawabu kwa Baba yenu aliye mbinguni. Basi wewe
utoapo sadaka, usipige panda mbele yako, kama wanafiki wafanyavyo katika masinagogi na njiani,
ili watukuzwe na watu. Amin, nawaambieni, Wamekwisha kupata thawabu yao. Basi wewe utoapo sadaka,
hata mkono wako wa kushoto usijue ufanyalo mkono wako wa kuume; sadaka yako iwe kwa siri; na Baba
yako aonaye sirini atakujazi. Tena msalipo, msiwe kama wanafiki; kwa maana wao wapenda kusali hali
wamesimama katika masinagogi na katika pembe za njia, ili waonekane na watu. Amin, nawaambia,
Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe usalipo, ingia katika chumba cha ndani, na ukiisha kufunga
mlango wako, usali mbele za Baba yako aliye sirini; na Baba yako aonaye sirini atakujazi. Tena
mfungapo, msiwe kama wanafiki wenye uso wa kukunjamana; maana hujiumbua nyuso zao; ili waonekane
na watu kuwa wanafunga, Amin, nawaambia, Wamekwisha kupata thawabu yao. Bali wewe ufungapo, jipake
mafuta kichwani, unawe uso; ili usionekane na watu kuwa unafunga, ila na Baba yako aliye sirini;
na Baba yako aonaye sirini atakujazi.
--------------
--------------
MAOMBI
Ndugu, Yesu ametufundisha jinsi ya kufanya matendo
mema kama vile kutoa sadaka, kusali na kufunga. Ili
Mungu atukuzwe, nasi tupate thawabu yetu, tuombe:-
Kiitikio: Upokee ombi letu.
1. Uwasaidie viongozi wa Kanisa katika juhudi zao za
kuyainua maisha ya waamini wao kiroho na kimwili.
Ee Bwana.
2. Uamshe mioyo ya viongozi wa serikali, ili
wawaunge mkono viongozi wa dini katika kuinua
hali ya maisha ya watu, hasa katika sekta za afya,
elimu na uchumi. Ee Bwana.
3. Ili viongozi wa dini na wa kijamii wazidi
kuwaandaa na kuwarithisha wafuasi wao mambo
yote muhimu kwa ustawi wa jamii kiroho na
kimwili. Ee Bwana.
4. Umjalie kila mmoja wetu kutenda mema kwa ukarimu
na unyofu wa moyo. Ee Bwana.
5. Uwarehemu ndugu zetu marehemu na kuwapa uzima
usio na mwisho huko mbinguni. Ee Bwana.
Ee Mungu, ulituzaa kwa neno la kweli ili tuwe kama
limbuko la viumbe vyako. Uyapokee maombi yetu. Kwa
njia ya Kristo Bwana wetu. Amina.