DOMINIKA YA PASAKA
Misa ya mchana
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.139:18,5-6
Nimefufuka na ningali pamoja nawe, aleluya; umeniwekea mkono wako, aleluya; maarifa hayo ni ya ajabu, aleluya!

Au:
Lk.24:34; Ufu.1:6

Bwana amefufuka kweli kweli, aleluya! Utukufu na ukuu una Yeye hata milele na milele, aleluya, aleluya!

Utukufu husemwa.

KOLEKTA

Ee Mungu, umetufungulia siku ya leo mlango wa uzima wa milele kwa njia ya Mwanao pekee aliyeshinda mauti. Tunakuomba utujalie sisi tunaoadhimisha sherehe ya ufufuko wa Bwana, tupate kufufuka kwenye mwanga wa uzima kwa njia ya kufanywa wapya na Roho wako. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Mdo.10:34,37-43
Petro akafumbua kinywa chake, akasema, Jambo lile ninyi mmelijua, lililoenea katika Uyahudi wote likianzia Galilaya, baada ya Ubatizo aliohubiri Yohane; habari za Yesu wa Nazareti, jinsi Mungu alivyomtia mafuta kwa Roho Mtakatifu na nguvu; naye akazunguka huko na huko, akitenda kazi njema na kuponya wote walioonewa na Ibilisi; kwa maana Mungu alikuwa pamoja naye. Nasi tu mashahidi wa mambo yote aliyoyatenda katika nchi ya Wayahudi na katika Yerusalemu; ambaye walimwua wakamtundika mtini. Huyo, Mungu alimfufua siku ya tatu, akamjalia kudhihirika, si kwa watu wote, bali kwa mashahidi waliokuwa wamekwisha kuchaguliwa na Mungu, ndio sisi, tuliokula na kunywa naye baada ya kufufuka kwake kutoka kwa wafu. Akatuagiza tuwahubiri watu na kushuhudia ya kuwa huyu ndiye aliyeamriwa na Mungu awe Mhukumu wa wahai na wafu. Huyo, manabii wote humshuhudia, ya kwamba kwa jina lake kila amwaminiye atapata ondoleo la dhambi.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.118:1-2,16-17,22-23(K) 24
1. Aleluya!
Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Israeli na aseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele.

(K) Siku hii ndiyo aliyoifanya Bwana,
Tutashangilia na kuifurahia.

2. Mkono wa kuume wa Bwana umetukuzwa;
Mkono wa kuume wa Bwana hutenda makuu.
Sitakufa bali nitaishi,
Nami nitayasimulia matendo ya Bwana. (K)

3. Jiwe walilolikataa waashi
Limekuwa jiwe kuu la pembeni.
Neno hili limetoka kwa Bwana,
Nalo ni ajabu machoni petu. (K)

SOMO 2: Kol.3:1-4
Ndugu zangu, mkiwa mmefufuliwa pamoja na Kristo, yatafuteni yaliyo juu, Kristo aliko, ameketi mkono wa kuume wa Mungu. Yafikirini yaliyo juu, siyo yaliyo katika nchi. Kwa maana mlikufa, na uhai wenu umefichwa pamoja na Kristo katika Mungu. Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu.

Au:
1Kor.5:6-8

Ndugu zangu, kujisifu kwenu si kuzuri. Hamjui kwamba chachu kidogo hulichachusha donge zima? Basi, jisafisheni, mkatoe ile chachu ya kale, mpate kuwa donge jipya, kama vile mlivyo hamkutiwa chachu. Kwa maana Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani, Kristo; basi na tuifanye karamu, si kwa chachu ya kale, wala kwa chachu ya uovu na ubaya, bali kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli.

SEKWENSIA
(K) Kristo, Pasaka wetu,
amechinjwa sadaka,
Tuile karamuye
na twimbe aleluya!

1. Aliyejitoa
sadaka ya Pasaka
wakristo wamtolee
sadaka ya sifa.

2. Mwanakondoo amewakomboa kondoo:
Kristo asiye na dhambi
Amewapatanisha na Baba
watu wenye dhambi.

3. Mauti na uzima
vimeshindana ajabu:
Mkuu wa uzima aliyekufa
Atawala mzima.

4. Utuambie, Maria,
uliona nini njiani?
Niliona kaburi la Kristo mzima,
Na utukufu wa yeye aliyefufuka:

5. Mashahidi ni malaika,
Leso ya uso na mavazi.
Kristo tumaini langu kafufuka:
Atawatangulia Galilea.

6. Twajua Kristo amefufuka
kweli katika wafu:
Ewe Mfalme mshindaji, utuhurumie.
Amina. Aleluya!

SHANGILIO: 1Kor.5:7-8
Aleluya, aleluya!
Kristo, Pasaka wetu
amekwisha kutolewa kuwa sadaka;
Basi na tuifanye karamu katika Bwana!
Aleluya!

INJILI: Yn.20:1-9
Hata siku ya kwanza ya juma Mariamu Magdalene alikwenda kaburini alfajiri, kungali giza bado; akaliona lile jiwe limeondolewa kaburini. Basi akaenda mbio, akafika kwa Simoni Petro na kwa yule mwanafunzi mwingine ambaye Yesu alimpenda, akawaambia, Wamemwondoa Bwana kaburini, wala hatujui walikomweka. Basi Petro akatoka, na yule mwanafunzi mwingine, wakashika njia kwenda kaburini. Wakaenda mbio wote wawili; na yule mwanafunzi mwingine akaenda mbio upesi kuliko Petro, akawa wa kwanza wa kufika kaburini. Akainama na kuchungulia, akaviona vitambaa vya sanda vimelala; lakini hakuingia. Basi, akaja na Simoni Petro akimfuata, akaingia ndani ya kaburi; akavitazama vitambaa vilivyolala; na ile leso iliyokuwepo kichwani pake; haikulala pamoja na vitambaa, bali imezongwazongwa mbali mahali pa peke yake. Basi ndipo alipoingia naye yule mwanafunzi mwingine aliyekuwa wa kwanza wa kufika kaburini, akaona na kuamini. Kwa maana hawajalifahamu bado andiko, ya kwamba imempasa kufufuka.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ndugu wapendwa, leo ni sikukuu kubwa ya kumshangilia Yesu mfufuka. Ufufuko wake uligeuza hali ya maisha yetu na kutujalia matumaini ya kupata ushindi juu ya ubaya wote.

1. Utujalie kushirikishwa nguvu za uzima mpya wa ufufuko wa Mwanao kwa kumfuata katika maisha yetu ya kila siku.

2. Utusaidie tuoneshe uzima huu mpya katika bidii yetu ya kuwashirikisha wenzetu furaha, upendo na matumaini yetu.

3. Utusaidie kufanya maisha yetu yawavutie wengine wamwelekee Kristo aliye chemchemi ya uzima mpya.

4. Utusaidie kutokubali kuzima furaha ya mwanga wa Kristo kwa kushiriki tena maisha ya dhambi.

5. Ututie moyo wa kuushuhudia ukristo wetu kwa matendo yetu.

6. Uwakaribishe marehemu wetu kwenye furaha za ufufuko huko mbinguni.

Ee Mungu mwenyezi uliyetukuka katika tendo la ajabu la kumfufua Mwanao katika wafu, upokee maombi yetu kwa jina la Yesu aliyefufuka na kuingia katika utukufu wako. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, tunakutolea sadaka hii tukishangilia kwa furaha sikukuu ya Pasaka. Kwa namna ya ajabu Kanisa lako linazaliwa upya na kulishwa kwa sadaka hiyo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

UTANGULIZI: Fumbo la Pasaka.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W.Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, kukutukuza kila wakati, ee Bwana, lakini hasa siku hii ya leo kutangaza utukufu wako, kwa kuwa Kristo, Pasaka wetu, ametolewa sadaka.
Yeye ndiye Mwanakondoo wa kweli aliyeondoa dhambi za ulimwengu. Yeye ndiye aliyeangamiza mauti yetu kwa kufa kwake, na alitengeneza upya uzima kwa kufufuka kwake.
Kwa sababu hiyo, katika upeo wa furaha ya kipasaka, ulimwengu mzima unashangilia. Lakini pia nguvu za mbinguni na majeshi ya Malaika wanaimba utenzi wa utukufu wako, wakisema bila mwisho:

Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu

ANTIFONA YA KOMUNYO: 1Kor.5:7-8
Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani Kristo, aleluya; basi na tuifanye karamu kwa yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli, aleluya, aleluya!

SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Mungu, ulilinde Kanisa lako kwa wema wako wa daima, ili likiisha kufanywa upya kwa mafumbo ya Pasaka, lipate kuufikia mwangaza wa ufufuko. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.