Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 7 LA PASAKA
MASIFU YA JIONI II

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI chagua 1-5(32-36)
1 (32)
Roho Muumbaji njoo kwetu
Ushuke toka juu uliko,
Njoo uzitwae roho zetu,
Zote uzifanye mali yako.

Wewe unaitwa Mfariji,
Thawabu isiyo na kifani,
Ni chemchemi na moto hai,
Ndiwe manukato na upendo.

Mtoaji wa vipaji saba,
Kidole cha kuume cha Mola;
Sisi wadogo watufundisha
Kusema na pia kuelewa.

Uziangaze akili zetu,
Washa upendo mioyo yetu;
Na kwa zako za daima nguvu
Iimarishe miili yetu.

Mfukuzie mbali mwuaji,
Amani ya kweli tuipate;
Na kila janga utuepushe
Kwa zako mbawa utulinde.

Kumjua Baba tujalie
Na huyo wa milele Mwanae,
Wewe Roho pia tukujue,
Watatu nyie Mungu Mmoja.

Baba utukufu wote kwako,
Na kwa Mwanao mlio sawa,
Pia kwa Mfariji Mkuu:
Ninyi mtukuzwe bila mwisho.


2 (33) Njoo, Ewe Muumbaji,
Njoo, Roho mtukufu,
Uje ujipumzishe
Rohoni mwetu karibu;
Uje na neema zako
Na misaada ya mbingu,
Ili tele kuijaza
Mioyo uloiumba.

E Mfariji Mkuu,
Tunakulilia Bwana,
Ewe karama kamambe
'Toka kwa Mungu Mkuu,
Chemchemi ya Uzima,
Ewe Moto wa Upendo,
Na mafuta ya kupaka -
Mazuri kutoka juu!

Wewe unajulikana
Kwa mapaji yako saba;
U kidole, tunakiri,
Cha mkono wake Mungu;
Wewe pia ni ahadi
Ya Baba Mwenyezi Mungu,
Ulimi waujalia
Uwezo wa kuongea.

Viwashe vyetu vionjo
Kutoka juu uliko,
Na zifanye zetu nyoyo
Zifurike kwa upendo;
Twondolee udhaifu
Wa hii miili yetu,
Saburi utugawie
Nazo fadhila kamambe.

Fukuzia mbali nasi
Adui tumwogopaye,
Na badala yake tupe
Amani yako ya kweli;
Wewe ukituongoza
Nasi tukikufuata,
Basi hatutaiacha
Njia ile ya uzima.

Twaomba yako neema
Itujalie, twaomba,
Kumjua yeye Baba,
Mwanae na Wewe pia,
Ambaye kila wakati
Bila mwisho tunakiri
U Roho wa Baba, Mwana,
Roho wao wa milele.

Utukufu wote wote,
Tena kwa nyakati zote,
Kwake yeye Mungu Baba
Na pia kwa wake Mwana,
Mfufuka 'toka wafu;
Pia kwako utukufu,
E Roho Mtakatifu,
Kwa milele mtukufu.

3 (34)
Ewe Roho wa Mungu Mwenyezi,
Juu ya nchi tupu gizani
Kwa uwezo mwingi uliruka
Ulimwengu ulipoumbika;

Mambo mazuri ukatengeza
Kwa ule udongo na vurugu,
Uzima wa Mungu livuvia
Katika pua yake adamu;

Njoo ili upande uhai
Katika nafsi zetu duni,
Sali ndani yetu, utuunde
Tuwe wana ndani yake Mwana.

Ee Roho uliye muweza,
Nyoyo zetu kwako elekeza,
Utuingize katika uzima
Ndani ya Utatu, Mungu 'Moja.
Stanbrook Abbey Hymnal

4 (35)
Shuka chini, Upendo wa Kimungu,
Uitafute hii roho yangu,
Na itembelee kwa ari yako,
Kwa ari yako hiyo iwakayo;
E Mfariji sogea karibu,
Jitokeze ndani ya moyo wangu,
Na uuwashe na kuupatia
Mwako wako mtakatifu sana.

Uuache uwake peke yake,
Mpaka tamaa za kidunia
Zitapoungua kwa joto lake
Na kuwa vumbi na majivu hasa;
Nayo hiyo nuru yako tukufu
Na iniangazie macho yangu,
Na inifunike mimi kabisa
Wakati yanimulikia njia.

Unipe upendo mtakatifu
Ili uwe vazi langu la nje,
Unipatie na unyenyekevu
Ili uwe vazi langu la ndani:
Unyenyekevu halisi wa moyo,
Ambao hutwaa yaliyo duni,
Na ambao hulia kwa uchungu
Juu ya kasoro zake wenyewe.

Na hivi ile tamaa ya roho,
Hamu kubwa isiyo na kipimo,
Wanadamu watashindwa kabisa
Kuieleza na kusimulia;
Maana hakuna anayeweza,
Kukisia hasa yake neema
Mpaka mwenyewe awe makao,
Makao ya Mtakatifu Roho.
Bianco da Siena +1434

5 (36)
Pendo la Baba na la Mungu Mwana,
Pendo ulo chanzo cha vitu vyote,
Ulotengeza uzuri wa mbingu,
Lengo na uhai wa ulimwengu.

Ewe Mwenyezi na Mtakatifu,
Amani na haki watuletea,
Viumbe kwa wema wavitendea,
Na waviepusha na kila ovu.
Usafi, cheo, hekima, haki,
Ukweli: vyote unavyo kamili;
Kwa njia ya Kristo mwenyewe,
Watutenga na mambo ya dunia.

Watu wote wakuabudu wewe,
Uliye mtukufu kwa milele
Tufariji sisi viumbe wako,
Jalia tufaidi mwanga wako.
Robert Bridges 1844-1930

ANT. I: Baada ya kufuta dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Mungu Mwenyezi aliye juu, aleluya.

Zab.110:1-5,7 Kutawazwa kwa mfalme mteule
Maana Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini ya miguu yake (Kor.15:25)

Mungu amemwambia bwana wangu,*
"Keti upande wangu wa kulia,

Mpaka niwafanye maadui zako,*
kama kibao cha kuegemea miguu yako."

Toka Sion Mungu ataeneza enzi yako.*
Asema: "Tawala juu ya adui zako!"

Watu wako watajitolea,*
siku utakapopambana na adui.

Vijana wako watakujia kwenye milima mitakatifu,*
kama vile umande wa asubuhi.

Mungu ameapa, wala hataghairi:/
"Kwamba wewe ni kuhani milele,*
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."

Mungu yuko upande wako wa kulia;*
atakapokasirika, atawaponda wafalme.

Njiani mfalme atakunywa maji ya kijito;*
kwa hiyo atainua kichwa juu kwa ushindi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Baada ya kufuta dhambi, aliketi mkono wa kuume wa Mungu Mwenyezi aliye juu, aleluya.

ANT. II: Bwana amewaokoa watu wake, aleluya.

Zab.111 Mungu asifika kwa matendo yake
Bwana, Mungu Mwenyezi, matendo yako ni makuu mno (Ufu.15:3)

Nitamshukuru Mungu kwa moyo wangu wote,*
katika jumuiya ya watu.

Matendo ya Mungu ni ya ajabu mno!*
Wote wanaoyafurahia hutaka kuyaelewa.

Kila afanyacho kimejaa utukufu na fahari;*
na uadilifu wake wadumu milele.

Mungu hutukumbusha matendo yake ya ajabu;*
Mungu ni mwema na mwenye huruma.

Huwapa chakula wenye kumcha;*
hasahau kamwe agano lake.

Amewaonesha watu wake enzi yake,*
kwa kuwapatia nchi za mataifa mengine.

Matendo yake ni ya haki, na ya kuaminika;*
amri zake zote ni za kutegemewa daima.

Amri zake zadumu daima na milele;*
zimetolewa kwa ukweli na uadilifu.

Aliwakomboa watu wake,/
na kufanya nao agano la milele.*
Yeye ni mtakatifu na wa kutisha mno.

Kumcha Mungu ni msingi wa hekima;/
wote wanaozitii amri zake hujaliwa busara.*
Sifa zake zadumu milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. II: Bwana amewaokoa watu wake, aleluya.

ANT. III: Aleluya, Bwana Mungu wetu ni mfalme; tufurahi na tumtukuze, aleluya.

WIMBO: Ufu.19:1,2,5-7 Arusi ya Mwana-kondoo

Aleluya.
Wokovu, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu!*
(W. Aleluya)
Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote,*
(W. Aleluya)
Nanyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Bwana, Mungu wetu Mwenyezi , ni Mfalme!*
(W. Aleluya)
Tufurahi na kushangilia; tumtukuze.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Wakati wa arusi ya Mwana-kondoo umefika,*
(W. Aleluya)
Na bibi arusi yuko tayari.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Atukuzwe Baba na Mwana, na Roho Mtakatifu,*
(W. Aleluya)
Kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele. Amina.*
W. Aleluya (aleluya).

ANT. III: Aleluya, Bwana Mungu wetu ni mfalme; tufurahi na tumtukuze, aleluya.

SOMO: Ebr.10:12-14
Kristo alitoa sadaka moja kwa ajili ya dhambi, sadaka ifaayo milele, kisha, akaketi upande wa kulia wa Mungu. Huko anangoja mpaka adui zake watakapowekwa kama kibao chini ya miguu yake. Basi, kwa sadaka yake moja, amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wanaotakaswa dhambi zao.

KIITIKIZANO
K. Roho Mtakatifu ni Msaidizi, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Atawafundisheni kila kitu.
W. Aleluya, aleluya..
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Roho...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Nitamtuma kwenu Msaidizi, Roho wa kweli atokaye kwa Baba. Yeye atanishuhudia, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Nitamtuma kwenu Msaidizi, Roho wa kweli atokaye kwa Baba. Yeye atanishuhudia, aleluya.

MAOMBI
Kristo Bwana wetu alituhimiza tusali, na Roho Mtakatifu akaja kuzijaza nyoyo na akili zetu.
W. Tunaomba Roho Mtakatifu atutetee.

Mchungaji wa milele, uwape wachungaji wa Kanisa lako hekima na ufahamu;
- uwajalie wawaongoze waamini wako katika njia ya wokovu. (W.)

Kristo wa mbinguni, umejaa rehema na huruma;
- usiwasahau fukara na maskini uliowaacha hapa duniani. (W.)

Kwa uwezo wa Roho Mtakatifu, Bikira Maria alikuchukua mimba;
- udumishe katika watawa wanawake moyo wa kutoa huduma kwa mapendo. (W.)

Kristo, padre wetu, unamtukuza Baba katika Roho Mtakatifu;
- uwaunganishe watu wote pamoja katika utenzi wako wa sifa. (W.)

Uwajalie marehemu uhuru mtukufu wa wana wa Mungu,
- na ukombozi kamili wa miili yao. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, tunasadiki kwamba Mwokozi wa wanadamu anatawala nawe katika utukufu. Isikilize sala yetu, na, kama alivyotuahidi mwenyewe, utuwezeshe kuhisi uwepo wake kati yetu mpaka mwisho wa nyakati. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.