Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 7 PASAKA
MASIFU YA JIONI I

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya.

UTENZI chagua 1-5(32-36)
1 (32)
Roho Muumbaji njoo kwetu
Ushuke toka juu uliko,
Njoo uzitwae roho zetu,
Zote uzifanye mali yako.

Wewe unaitwa Mfariji,
Thawabu isiyo na kifani,
Ni chemchemi na moto hai,
Ndiwe manukato na upendo.

Mtoaji wa vipaji saba,
Kidole cha kuume cha Mola;
Sisi wadogo watufundisha
Kusema na pia kuelewa.

Uziangaze akili zetu,
Washa upendo mioyo yetu;
Na kwa zako za daima nguvu
Iimarishe miili yetu.

Mfukuzie mbali mwuaji,
Amani ya kweli tuipate;
Na kila janga utuepushe
Kwa zako mbawa utulinde.

Kumjua Baba tujalie
Na huyo wa milele Mwanae,
Wewe Roho pia tukujue,
Watatu nyie Mungu Mmoja.

Baba utukufu wote kwako,
Na kwa Mwanao mlio sawa,
Pia kwa Mfariji Mkuu:
Ninyi mtukuzwe bila mwisho.


2 (33) Njoo, Ewe Muumbaji,
Njoo, Roho mtukufu,
Uje ujipumzishe
Rohoni mwetu karibu;
Uje na neema zako
Na misaada ya mbingu,
Ili tele kuijaza
Mioyo uloiumba.

E Mfariji Mkuu,
Tunakulilia Bwana,
Ewe karama kamambe
'Toka kwa Mungu Mkuu,
Chemchemi ya Uzima,
Ewe Moto wa Upendo,
Na mafuta ya kupaka -
Mazuri kutoka juu!

Wewe unajulikana
Kwa mapaji yako saba;
U kidole, tunakiri,
Cha mkono wake Mungu;
Wewe pia ni ahadi
Ya Baba Mwenyezi Mungu,
Ulimi waujalia
Uwezo wa kuongea.

Viwashe vyetu vionjo
Kutoka juu uliko,
Na zifanye zetu nyoyo
Zifurike kwa upendo;
Twondolee udhaifu
Wa hii miili yetu,
Saburi utugawie
Nazo fadhila kamambe.

Fukuzia mbali nasi
Adui tumwogopaye,
Na badala yake tupe
Amani yako ya kweli;
Wewe ukituongoza
Nasi tukikufuata,
Basi hatutaiacha
Njia ile ya uzima.

Twaomba yako neema
Itujalie, twaomba,
Kumjua yeye Baba,
Mwanae na Wewe pia,
Ambaye kila wakati
Bila mwisho tunakiri
U Roho wa Baba, Mwana,
Roho wao wa milele.

Utukufu wote wote,
Tena kwa nyakati zote,
Kwake yeye Mungu Baba
Na pia kwa wake Mwana,
Mfufuka 'toka wafu;
Pia kwako utukufu,
E Roho Mtakatifu,
Kwa milele mtukufu.

3 (34)
Ewe Roho wa Mungu Mwenyezi,
Juu ya nchi tupu gizani
Kwa uwezo mwingi uliruka
Ulimwengu ulipoumbika;

Mambo mazuri ukatengeza
Kwa ule udongo na vurugu,
Uzima wa Mungu livuvia
Katika pua yake adamu;

Njoo ili upande uhai
Katika nafsi zetu duni,
Sali ndani yetu, utuunde
Tuwe wana ndani yake Mwana.

Ee Roho uliye muweza,
Nyoyo zetu kwako elekeza,
Utuingize katika uzima
Ndani ya Utatu, Mungu 'Moja.
Stanbrook Abbey Hymnal

4 (35)
Shuka chini, Upendo wa Kimungu,
Uitafute hii roho yangu,
Na itembelee kwa ari yako,
Kwa ari yako hiyo iwakayo;
E Mfariji sogea karibu,
Jitokeze ndani ya moyo wangu,
Na uuwashe na kuupatia
Mwako wako mtakatifu sana.

Uuache uwake peke yake,
Mpaka tamaa za kidunia
Zitapoungua kwa joto lake
Na kuwa vumbi na majivu hasa;
Nayo hiyo nuru yako tukufu
Na iniangazie macho yangu,
Na inifunike mimi kabisa
Wakati yanimulikia njia.

Unipe upendo mtakatifu
Ili uwe vazi langu la nje,
Unipatie na unyenyekevu
Ili uwe vazi langu la ndani:
Unyenyekevu halisi wa moyo,
Ambao hutwaa yaliyo duni,
Na ambao hulia kwa uchungu
Juu ya kasoro zake wenyewe.

Na hivi ile tamaa ya roho,
Hamu kubwa isiyo na kipimo,
Wanadamu watashindwa kabisa
Kuieleza na kusimulia;
Maana hakuna anayeweza,
Kukisia hasa yake neema
Mpaka mwenyewe awe makao,
Makao ya Mtakatifu Roho.
Bianco da Siena +1434

5 (36)
Pendo la Baba na la Mungu Mwana,
Pendo ulo chanzo cha vitu vyote,
Ulotengeza uzuri wa mbingu,
Lengo na uhai wa ulimwengu.

Ewe Mwenyezi na Mtakatifu,
Amani na haki watuletea,
Viumbe kwa wema wavitendea,
Na waviepusha na kila ovu.
Usafi, cheo, hekima, haki,
Ukweli: vyote unavyo kamili;
Kwa njia ya Kristo mwenyewe,
Watutenga na mambo ya dunia.

Watu wote wakuabudu wewe,
Uliye mtukufu kwa milele
Tufariji sisi viumbe wako,
Jalia tufaidi mwanga wako.
Robert Bridges 1844-1930

ANT. I: Bwana Mungu yuko juu mbinguni, na humwinua mnyonge kutoka mavumbini, aleluya.

Zab.113 Sifa kwa Mungu mtukufu
Amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao. vya enzi, akawakweza wanyenyekevu (Lk.1:52)

Enyi watumishi wa Mungu,*
lisifuni jina lake!

Jina lake litukuzwe,*
sasa na hata milele.

Kutoka mashariki hata magharibi,*
litukuzwe jina la Mungu!

Mungu atawala mataifa yote,*
utukufu wake wazipita mbingu.

Hakuna aliye sawa na Mungu, Mungu wetu,*
ambaye anakaa juu kabisa;

lakini huinama chini*
kuzitazama mbingu na nchi.

Humwinua fukara kutoka mavumbini;*
humnyanyua maskini kutoka unyonge wake,

na kumweka pamoja na wakuu;*
naam, pamoja na wakuu wa watu wake.

Humrudishia hadhi mwanamke aliye tasa;*
na kumfurahisha kwa kumjalia watoto.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Bwana Mungu yuko juu mbinguni, na humwinua mnyonge kutoka mavumbini, aleluya.

ANT. II: Umevifungua vifungo vyangu, Ee Bwana; nitakutolea sadaka ya shukrani, aleluya.

Zab.116:10-19 Shukrani kwa kuokolewa kifoni
Kwa njia ya Yesu, tumtolee Mungu sadaka ya sifa daima (Ebr.13:15)

Nampenda Mungu, kwa maana anisikia,*
maana amesikiliza kilio cha ombi langu.

Yeye hunisikiliza*
kila ninapomlilia.

Hatari ya kifo ilinizunguka,/
vitisho vya kaburi vilinivamia;*
nilijawa mahangaiko na majonzi.

Kisha nikamlilia Mungu:*
"Ee Mungu, tafadhali unisalimishe!”

Mungu amejaa wema na haki;*
Mungu wetu ni mwenye huruma.

Mungu huwalinda wanyofu*
nilikuwa nimekandamizwa, naye akaniokoa.

Uwe na utulivu mkuu, ee roho yangu,*
kwa maana Mungu amenitendea vyema.

Ameniokoa kifoni na kufuta machozi yangu;*
akanilinda nisije nikaanguka.

Basi, nitatembea mbele yake Mungu,*
katika nchi ya watu walio hai.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Umevifungua vifungo vyangu, Ee Bwana; nitakutolea sadaka ya shukrani, aleluya.

ANT. III: Mwana wa Mungu alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; akawa chanzo cha wokovu wa milele, kwa watu wote wanaomtii, aleluya.

WIMBO: Filp.2:6-11 Kristo, mtumishi wa Mungu
Kristo Yesu, kwa asili,*
alikuwa daima Mungu;

lakini hakufikiri kwamba/
kule kuwa sawa na Mungu*
ni kitu cha kung'ang'ania kwa nguvu.

Bali, kwa hiari yake mwenyewe,*
aliachilia hayo yote,

akajitwalia hali ya mtumishi/
akawa sawa na wanadamu,*
akaonekana kama wanadamu.

Alijinyenyekeza na kutii mpaka kufa,*
hata kufa msalabani.

Kwa sababu hiyo*
Mungu alimkweza juu kabisa,

akampa jina lililo kuu zaidi*
kuliko majina yote.

Ili kwa heshima ya jina la Yesu,/
viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu,*
vipige magoti mbele yake;

Na kila mtu akiri/
Kwamba Yesu Kristo ni Bwana,*
kwa utukufu wa Mungu Baba.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. III: Mwana wa Mungu alijifunza kutii kwa mateso hayo yaliyompata; akawa chanzo cha wokovu wa milele, kwa watu wote wanaomtii, aleluya.

SOMO: 1Pet.2:9-10
Ninyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani, akawaingizeni katika mwanga wake mkuu. Wakati mmoja ninyi hamkuwa watu wa Mungu, lakini sasa ninyi ni watu wake; wakati mmoja hamkupewa huruma ya Mungu, lakini sasa mmeipokea.

KIITIKIZANO
K. Roho Mtakatifu ni Msaidizi, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Atawafundisheni kila kitu.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Roho...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Sitawaacha peke yenu kama yatima: sasa naenda zangu, lakini nitarudi kwenu, na hapo ndipo mioyo yenu itakapojaa furaha, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Sitawaacha peke yenu kama yatima: sasa naenda zangu, lakini nitarudi kwenu, na hapo ndipo mioyo yenu itakapojaa furaha, aleluya.

MAOMBI
Atukuzwe Kristo, Mwana wa Mungu. Kule mtoni Yordani Roho Mtakatifu alimshukia katika umbo la njiwa. Na tuthibitishe sala yetu kwake kwa kusema:
W. Amina. Amina.

Bwana Yesu, umtume Roho wako Mtakatifu, ayafanye upya maisha ya Kanisa,
- na kulifanya Kanisa ling'ae kwa matumaini. (W.)

Mataifa yote na yakusifu, yakikiri kuwa ndiwe mfalme na Bwana wao;
- uwafanye Waisraeli wawe watu wako. (W.)

Utufanye tuwe wakarimu na wanyenyekevu;
- utuwezeshe kusahau shida zetu wenyewe wakati tunapowahudumia wengine. (W.)

Siku ya Pentekoste ulitangua maafa ya Babeli, yaliyoigawanya na kuivuruga jamii ya watu;
- kwa njia ya Roho Mtakatifu, uwawezeshe watu wote kuongea lugha moja ya imani na mapendo. (W.)

Tunaomba Roho wako Mtakatifu akae ndani yetu,
- ili aipatie miili yetu uzima. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu: Baba Yetu...

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Bwana Mungu, tunasadiki kwamba Mwokozi wa wanadamu anatawala nawe katika utukufu. Isikilize sala yetu, na, kama alivyotuahidi mwenyewe, utuwezeshe kuhisi uwepo wake kati yetu mpaka mwisho wa nyakati. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.