JUMAPILI JUMA LA 6 LA PASAKA
SALA ZA MCHANA
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya.
UTENZI
Njoo Roho Mtakatifu,
Ndani yetu sisi uishi,
Pamoja nawe waje pia
Mungu Baba na Mungu Mwana,
Nazo zako tele neema
Njoo upate tujalia,
Zitufanye watakatifu,
Pia tuwe kitu kimoja.
Imara katika upendo
Na viwe, roho na ulimi,
Yako sifa kuitangaza
Kila mahali duniani,
Na ule upendo jalie-
Ulio mwetu mioyoni-
Mioyo mingine iwashwe
Kutokana na mwako wake.
Ee Mtukufu kabisa
Utatu ulio upendo,
Moyo wake bin-Adamu
Kwa ajili yako 'liumbwa,
Kwako Wewe na iwe sifa
Kwa wimbo usio na mwisho,
Haki yako Wewe pekee
Kwabudiwa hata milele.
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya.
Zab.23 Mungu mchungaji wetu
Mwana-kondoo atakuwa mchungaji wao, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji ya
uzima (Ufu.7:17)
Mungu ni mchungaji wangu;*
sitapungukiwa chochote,
Hunipumzisha kwenye malisho mabichi;/
huniongoza kwenye maji matulivu na safi,*
na kunirudishia nguvu.
Huniongoza katika njia iliyo sawa,*
kwa ajili ya jina lake.
Nijapopita katika giza kuu, sitaogopa,/
kwa kuwa wewe Mungu u pamoja nami;*
fimbo yako na bakora yako vyanilinda.
Waniandalia karamu mbele ya adui zangu;/
umenipaka mafuta kichwani mwangu,*
na kikombe changu wakijaza mpaka kufurika.
Hakika wema wako na upendo wako mkuu,/
vitakuwa pamoja nami maisha yangu yote.*
Nitakaa nyumbani mwako muda wote niishipo.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Zab.76 Mungu Mshindi
Watamwona Mwana wa Mtu akija juu ya mawingu ya angani (Mt.24:30)
I
Mungu anajulikana katika Yuda;*
jina lake ni kuu katika Israeli.
Hema lake liko huko Salemu;*
makao yake yako huko Sion.
Huko alivunja mishale ya adui;*
alivunja ngao, panga na silaha.
Wewe, Ee Mungu, watukuka mno;/
umejaa fahari kuu unaporudi,*
kutoka milimani ulikowashinda adui.
Washupavu wao wamenyang'anywa nyara zao,/
sasa wanalala usingizi wao wa mwisho,*
ushujaa wao wote haukuwafaa kitu.
Ulipowakemea, Ee Mungu wa Yakobo,*
farasi na wapanda farasi walikufa ganzi.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
II
Wewe, Ee Mungu, ni wa kutisha mno!*
Nani awezaye kustahimili ukikasirika?
Umejulisha hukumu yako toka mbinguni,*
nayo dunia ikaogopa na kunyamaa;
wakati ulipoinuka, Ee Mungu, kutoa hukumu,*
kuwaokoa wote wanaodhulumiwa duniani.
Ghadhabu ya watu husababisha tu sifa kwako;*
na walioponea huko Emati watafanya sikukuu zako.
Mpeni Mungu, Mungu wenu, yale mliyoahidi;*
enyi mlio karibu, mpeni vipaji Mungu wa kutisha.
Yeye huwanyenyekesha wakuu;*
huwatisha wafalme wa dunia.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT.: Aleluya, aleluya, aleluya.
MASOMO
Kabla ya Adhuhuri: 1Kor.15:3b-5
Kristo alikufa kwa ajili ya dhambi zetu, kufuatana na Maandiko matakatifu; alizikwa, akafufuka
siku ya tatu kama ilivyoandikwa; alimtokea kwanza Kefa, na baadaye aliwatokea wale kumi na wawili.
K. Bwana amefufuka kweli, aleluya.
W. Amemtokea Simoni, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Adhuhuri: Ef.2:4-6
Mungu ni mwenye huruma nyingi. Alitupenda kwa mapendo yasiyopimika, hata ingawa tulikuwa tumekufa
kwa sababu ya dhambi, alitufanya hai pamoja na Kristo. Kwa neema ya Mungu ninyi mmeokolewa. Kwa
kuungana na Kristo Yesu, Mungu alitufufua pamoja naye, tukatawale pamoja naye mbinguni.
K. Wanafunzi walifurahi, aleluya.
W. Walipomwona Bwana, aleluya.
Sala: tazama chini kabisa ukurasa huu
---
Baada ya Adhuhuri: Rom.6:4
Tulipobatizwa tuliungana na kifo chake, tukazikwa pamoja naye, ili kama vile Kristo alivyofufuliwa
katika wafu kwa kitendo kitukufu cha Baba, sisi pia tuweze kuishi maisha mapya.
K. Kaa nasi, Bwana, aleluya.
W. Maana usiku unakaribia, aleluya.
SALA:
Tuombe: Mungu Mwenyezi, utujalie neema ya kuadhimisha kiaminifu siku hizi za furaha zilizowekwa
kwa ajili ya heshima ya Bwana Mfufuka. Utufundishe kuzingatia kimatendo fumbo hili tunalolikumbuka
katika ibada. Tunaomba hayo kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
W. Amina.
K. Tumtukuze Bwana.
(W.) tumshukuru Mungu.