Generic placeholder image

JUMAPILI JUMA LA 6 LA PASAKA
MASIFU YA JIONI II

K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele. Amina. Aleluya

UTENZI chagua 1-7(25-31)
1 (25)
Kristo Bwana amefufuka!
Kila mnyororo Bwana kakata,
Sikilizeni, hao malaika
Makelele kwa shangwe wanapiga,
Milele mbinguni juu waimba,
Aleluya!

Aliyekufa kwa ajili yetu,
Na mateso mengi kuvumilia -
Kuvumilia kwa ajili yetu,
Ni Kondoo wetu wa Paska leo!
Nasi pia kwa shangwe tunaimba.
Aleluya!

Yeye aliyepata maumivu
Na hasara yote msalabani,
Sasa yupo katika utukufu,
Akitwombea, huko mbinguni,
Na anasikia kilio chetu.
Aleluya!

Sasa atuagiza tutangaze
Pote pote ulimwenguni jinsi
Ya kuokoka waliopotea,
Na ya kusamehewa wenye toba,
Na tuwezavyo ingia mbinguni.
Aleluya!
Mikaeli Weisse yapata 1480-1534

2 (26)
Aleluya! Aleluya!
Angani inatanda Pasaka!
Yesu ni mzima, hafi tena!
Giza limetokomezwa lote,
Na Bwana wa nuru Mfufuka!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Mama Maria mwone Mwanao,
Anavyofurahi kwa ushindi!
Mateso mlishiriki nyote,
Milele mtatawala nyote!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Watafuta waliopotea!
Naye Petro anakulilia!
Mwimarishe awe mwamba,
Kundi lako alichunge!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Mzima haishi kaburini,
Kristo yupo ghorofani!
Utukufu wake kauficha,
Mwili wake hai aonesha!
Aleluya! Aleluya!

Aleluya! Aleluya!
Japo uso wake hatuoni,
Yupo na sisi kama mwanzoni!
Ni padre wetu mtukufu,
Twashangilia mtu mzima!
Aleluya! Aleluya!
Yakobo Quinn SJ

3 (27)
Aleluya, mwimbieni Yesu,
Enzi na ufalme ni vyake.
Aleluya, fanaka ni yake,
Ushindi ni wake peke yake.
Sikizeni, nyimbo za Sion
Zinanguruma kama tufani,
Zinasikika kama gharika:
Kwa damu yake ilo azizi,
Yesu ametukomboa sisi,
Watu kutoka kila taifa.

Aleluya, katika huzuni
Kama yatima hatujaachwa;
Aleluya, yu karibu nasi,
Imani yasadiki kabisa,
Haiulizi kwa jinsi gani
Ingawa Bwana alitoweka,
Akafunikwa nayo mawingu
Siku ile ya arobaini,
Tutasahau ahadi yake:
'Nipo nanyi daima milele'?
S. S. Wesley 1810-1876

4 (28)
Kwenye Karamu ya Mwana-Kondoo
Mfalme mshindi twamwimbia,
Alotuosha kwa wingi wa maji
Kutoka penye tobo ubavuni.

Yeye analo pendo la kimungu
Waalikwa wanyweshwa damu yake,
Na awapa waule mwili wake
Pendo ndilo kafara na kuhani.

Panapomwagwa damu ya Pasaka
Mwuaji upanga aufutika;
Jeshi la Israeli lapita
Askari adui wafa maji.

Kristo kondoo aliyechinjwa,
Kafara na mkate wa Pasaka;
Tuile manna itokayo juu
Kwa unyofu na upendo halisi.

Kafara shujaa kutoka juu,
Nguvu za kuzimu ni chini yako;
Vitani mauti umeyashinda,
Uzima na mwanga kutuletea.

Bendera sasa waipeperusha,
Shetani na kaburi watiisha;
Malaika waungana kusifu
Kupinduliwa kwa bwana shetani.

Ushindi na furaha ya Pasaka
Dhambi tu ndo yaweza viharibu;
Tukinge na kifo cha dhambi Bwana,
Tulozaliwa upya ndani yako.

Tenzi za fahari, nyimbo za sifa
Tunakuimbia mpenzi Baba;
Na sifa zote milele mpate,
Bwana Mfufuka na wewe Roho.
Karne ya 7

5 (29)
Utangazeni ushindi wake,
Ewe mbingu na wewe dunia,
Maana Kristo amefufuka
Kama mwenyewe alivyosema:
Ndie yule alosulibiwa,
Ni Mungu kweli aliye hai,
Aliyekaa kwa siku tatu
Kati ya wafu huko kuzimu.

Kristo alikufa kwa aibu
Kwa ajili yetu sisi watu,
Lakini sasa aishi tena
Akiwa na nguvu na uweza;
Moto wake na haujazimwa,
Mwali wake unaoangaza
Ulimwengu wote waujaza
Kwa furaha tele na mwangaza.

Sifa na heshima kwake Baba
Ambaye hakika Hakuumbwa,
Na kwa Mwanae aliye hai
Ambaye hakika hakushindwa,
Bali anatawala kwa enzi
Pamoja na Roho wake Mungu,
Utatu ulio Mtukufu,
Katika yeye Mungu Mmoja.
Stanbrook Abbey Hymnal

6 (30)
Njoni, enyi waamini, njoni,
Mkashangilie kwa furaha;
Mungu kawapa Israeli
Furaha baada ya huzuni;
Wana na binti zake Yakobo
Si watumwa tena wa Farao;
Kawavusha miguu mikavu
Katikati ya Bahari ya Shamu.

Leo ndio roho zachipua;
Kristo jela kabomoa,
Japo siku tatu kawa mfu
Leo kachomoza kama jua;
Kipupwe chote cha dhambi zetu,
Cha muda mrefu na cha kiza,
Metokomezwa kwa yako nuru
Wewe tukusifuye daima.

Milango imara ya mauti,
Wala kaburi pana la giza,
Wala walinzi, wala muhuri,
Havikushiki uwe maiti
Maana leo ulisimama.
Kati yao Kumi na Wawili,
Amani yako ukawapatia
Ipitayo ufahamu wetu.
Mt. Yohane wa Damasko yapata 750

7 (31)
Hakika vita sasa vimekwisha,
Majeshi ya motoni yakimbia;
Tupige ukelele wa ushindi
Kwa furaha na shangwe, aleluya.

Kristo aliyeuvumilia
Ule mti utiao aibu,
Twamkaribisha tukimsifu
Aloshinda mauti, aleluya.

Asubuhi ya tatu kafufuka,
Amevishwa nuru ya utukufu.
Ambayo wenye imani thabiti
Mbinguni watavishwa, aleluya.

Ile milango duni ya kuzimu
Ufunguo wao yaachilia,
Mlango wa Paradisi u wazi;
Tusichoke kuimba, aleluya.

Bwana, kwa mapigo tulokupiga,
Tujalie tuwe mbali na kifo,
Ili tuendelee kukariri
Salamu yetu hii, aleluya.
Simphonia Sirenum 1695

ANT. I: Alimfufufa Kristo kutoka wafu, akamketisha mkono wake wa kuume mbinguni, aleluya.

Zab.110:1-5,7 Kutawazwa kwa mfalme mteule
Kristo sharti atawale mpaka Mungu atakapowashinda adui zake na kuwaweka chini ya miguu yake (Kor.15:25)

Mungu amemwambia bwana wangu,*
"Keti upande wangu wa kulia,

Mpaka niwafanye maadui zako,*
kama kibao cha kuegemea miguu yako."

Toka Sion Mungu ataeneza enzi yako.*
Asema: "Tawala juu ya adui zako!"

Watu wako watajitolea,*
siku utakapopambana na adui.

Vijana wako watakujia kwenye milima mitakatifu,*
kama vile umande wa asubuhi.

Mungu ameapa, wala hataghairi:/
"Kwamba wewe ni kuhani milele,*
kufuatana na utaratibu wa ukuhani wa Melkisedeki."

Mungu yuko upande wako wa kulia;*
atakapokasirika, atawaponda wafalme.

Njiani mfalme atakunywa maji ya kijito;*
kwa hiyo atainua kichwa juu kwa ushindi.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. I: Alimfufufa Kristo kutoka wafu, akamketisha mkono wake wa kuume mbinguni, aleluya.

ANT. II: Mmeongolewa, mkaziacha sanamu na kumgeukia Mungu aliye hai, aleluya.

Zab.115 Mungu mmoja wa kweli
Mmemgeukia Mungu, mkaziacha sanamu, ili kumtumikia Mungu aliye hai na wa kweli (1Tes.1:9)

Sio sisi, Ee Mungu, sio sisi;/
bali wewe peke yako utukuzwe,*
kwa ajili ya upendo wako mkuu na uaminifu wako.

Kwa nini mataifa yanatuuliza:*
"Mungu wenu yuko wapi?"

Mungu wetu yuko mbinguni;*
yote anayotaka huyafanya.

Miungu yao imefanywa kwa fedha na dhahabu;*
imetengenezwa kwa mikono ya wanadamu.

Ina vinywa lakini haisemi;*
ina macho lakini haioni.

Ina masikio lakini haisikii;*
ina pua lakini hainusi.

Ina mikono lakini haipapasi;/
ina miguu lakini haitembei.*
Haiwezi kamwe kutoa sauti.

Wote wanaoitengeneza wanafanana nayo,*
kadhalika na wote walio na imani nayo.

Enyi watu wa Israeli mtumainieni Mungu;*
yeye ni msaidizi wenu na ngao yenu.

Enyi wazao wa Aroni mtumainieni Mungu;*
yeye ni msaidizi wenu na mlinzi wenu.

Enyi mnaomcha Mungu mtumainieni Mungu;*
yeye ni msaidizi wenu na mlinzi wenu.

Mungu anatukumbuka, na atatubariki;/
atawabariki watu wa Israeli,*
atawabariki wazao wa Aron.

Atawabariki wote wamchao,*
atawabariki wazao wa Aron.

Mungu awajalieni watoto;*
awajalie ninyi na wazao wenu!

Mbarikiwe na Mungu,*
aliyeumba mbingu na dunia.

Mbingu ni mali yake Mungu,*
bali dunia amewapa wanadamu.

Sio wafu wanaomsifu Mungu,*
wala ye yote aliyeshuka kuzimuni.

Basi ni sisi tutakaomsifu Mungu,*
sasa na hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

ANT. II: Mmeongolewa, mkaziacha sanamu na kumgeukia Mungu aliye hai, aleluya.

ANT. III: Aleluya, ushindi na utukufu na uwezo vina Mungu wetu, aleluya.

WIMBO: Ufu.19:1,2,5-7 Arusi ya Mwana-kondoo

Aleluya.
Wokovu, utukufu na nguvu ni mali yake Mungu wetu!*
(W. Aleluya)
Maana hukumu yake ni ya kweli na ya haki.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Msifuni Mungu enyi watumishi wake wote,*
(W. Aleluya)
Nanyi nyote mnaomcha, wadogo kwa wakubwa.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Bwana, Mungu wetu Mwenyezi , ni Mfalme!*
(W. Aleluya)
Tufurahi na kushangilia; tumtukuze.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Wakati wa arusi ya Mwana-kondoo umefika,*
(W. Aleluya)
Na bibi arusi yuko tayari.
W. Aleluya (aleluya).

Aleluya.
Atukuzwe Baba na Mwana, na Roho Mtakatifu,*
(W. Aleluya)
Kama mwanzo na sasa na siku zote, na milele. Amina.*
W. Aleluya (aleluya).

ANT. III: Aleluya, ushindi na utukufu na uwezo vina Mungu wetu, aleluya.

SOMO: Ebr.10:12-14
Kristo alitoa sadaka moja kwa ajili ya dhambi, sadaka ifaayo milele, kisha, akaketi upande wa kulia wa Mungu. Huko anangoja mpaka adui zake watakapowekwa kama kibao chini ya miguu yake. Basi, kwa sadaka yake moja, amewafanya kuwa wakamilifu milele wale wanaotakaswa dhambi zao.

KIITIKIZANO
K. Bwana amefufuka kweli, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Amemtokea Simoni.
W. KAleluya, aleluya..
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Bwana...

Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda yeye, nasi tutakuja kwake na kukaa naye, aleluya.

WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.

Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.

Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.

Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.

Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;

amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.

Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.

Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,

kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.

Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.

Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina

Ant. Mtu akinipenda atashika neno langu, na Baba yangu atampenda yeye, nasi tutakuja kwake na kukaa naye, aleluya.

MAOMBI
Tumwombe Mungu Baba, aliyemfufua Kristo na kumtukuza kwa kumketisha mkono wake wa kuume.
W. Bwana, uwalinde watu wako kwa utukufu wa Kristo.

Baba, kwa ushindi wa msalaba umemwinua Yesu kutoka duniani;
- na awavutie watu wote kwake. (W.)

Kwa kutukuzwa kwake Kristo, umpeleke Roho wako katika Kanisa;
- ufanye awe ishara ya umoja kwa familia yote ya binadamu. (W.)

Umepata kuwa Baba wa watu kwa njia ya maji na Roho;
- uwadumishe katika kushika kiaminifu ahadi zao za ubatizo mpaka wanapoingia katika uzima wa milele. (W.)

Kwa kutukuzwa kwake Mwanao, uwainue wenye huzuni, uwafungulie wafungwa, uwaponye wagonjwa;
- ulimwengu mzima na ufurahie zawadi zako za ajabu. (W.)

Uliwalisha waamini marehemu kwa mwili na damu ya Kristo;
- uwawezeshe kushiriki utukufu wake siku ya ufufuko. (W.)

Sala ya Baba yetu:
K. Tutekeleze agizo la Bwana wetu, na kusema:

Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.

SALA:
Mungu Mwenyezi, utujalie neema ya kuadhimisha kiaminifu siku hizi za furaha zilizowekwa kwa ajili ya heshima ya Bwana Mfufuka. Utufundishe kuzingatia kimatendo fumbo hili tunalolikumbuka katika ibada. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.

W. Amina.

K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.

(W.) Amina.