JUMAPILI JUMA LA 6 PASAKA
MASIFU YA JIONI I
K. Ee Mungu, uje kutusaidia.
W. Ee Bwana, utusaidie hima.
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu, kama mwanzo, na sasa, na siku zote, na milele.
Amina. Aleluya
UTENZI chagua 1-7(25-31)
1 (25)
Kristo Bwana amefufuka!
Kila mnyororo Bwana kakata,
Sikilizeni, hao malaika
Makelele kwa shangwe wanapiga,
Milele mbinguni juu waimba,
Aleluya!
Aliyekufa kwa ajili yetu,
Na mateso mengi kuvumilia -
Kuvumilia kwa ajili yetu,
Ni Kondoo wetu wa Paska leo!
Nasi pia kwa shangwe tunaimba.
Aleluya!
Yeye aliyepata maumivu
Na hasara yote msalabani,
Sasa yupo katika utukufu,
Akitwombea, huko mbinguni,
Na anasikia kilio chetu.
Aleluya!
Sasa atuagiza tutangaze
Pote pote ulimwenguni jinsi
Ya kuokoka waliopotea,
Na ya kusamehewa wenye toba,
Na tuwezavyo ingia mbinguni.
Aleluya!
Mikaeli Weisse yapata 1480-1534
2 (26)
Aleluya! Aleluya!
Angani inatanda Pasaka!
Yesu ni mzima, hafi tena!
Giza limetokomezwa lote,
Na Bwana wa nuru Mfufuka!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Mama Maria mwone Mwanao,
Anavyofurahi kwa ushindi!
Mateso mlishiriki nyote,
Milele mtatawala nyote!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Watafuta waliopotea!
Naye Petro anakulilia!
Mwimarishe awe mwamba,
Kundi lako alichunge!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Mzima haishi kaburini,
Kristo yupo ghorofani!
Utukufu wake kauficha,
Mwili wake hai aonesha!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Japo uso wake hatuoni,
Yupo na sisi kama mwanzoni!
Ni padre wetu mtukufu,
Twashangilia mtu mzima!
Aleluya! Aleluya!
Yakobo Quinn SJ
3 (27)
Aleluya, mwimbieni Yesu,
Enzi na ufalme ni vyake.
Aleluya, fanaka ni yake,
Ushindi ni wake peke yake.
Sikizeni, nyimbo za Sion
Zinanguruma kama tufani,
Zinasikika kama gharika:
Kwa damu yake ilo azizi,
Yesu ametukomboa sisi,
Watu kutoka kila taifa.
Aleluya, katika huzuni
Kama yatima hatujaachwa;
Aleluya, yu karibu nasi,
Imani yasadiki kabisa,
Haiulizi kwa jinsi gani
Ingawa Bwana alitoweka,
Akafunikwa nayo mawingu
Siku ile ya arobaini,
Tutasahau ahadi yake:
'Nipo nanyi daima milele'?
S. S. Wesley 1810-1876
4 (28)
Kwenye Karamu ya Mwana-Kondoo
Mfalme mshindi twamwimbia,
Alotuosha kwa wingi wa maji
Kutoka penye tobo ubavuni.
Yeye analo pendo la kimungu
Waalikwa wanyweshwa damu yake,
Na awapa waule mwili wake
Pendo ndilo kafara na kuhani.
Panapomwagwa damu ya Pasaka
Mwuaji upanga aufutika;
Jeshi la Israeli lapita
Askari adui wafa maji.
Kristo kondoo aliyechinjwa,
Kafara na mkate wa Pasaka;
Tuile manna itokayo juu
Kwa unyofu na upendo halisi.
Kafara shujaa kutoka juu,
Nguvu za kuzimu ni chini yako;
Vitani mauti umeyashinda,
Uzima na mwanga kutuletea.
Bendera sasa waipeperusha,
Shetani na kaburi watiisha;
Malaika waungana kusifu
Kupinduliwa kwa bwana shetani.
Ushindi na furaha ya Pasaka
Dhambi tu ndo yaweza viharibu;
Tukinge na kifo cha dhambi Bwana,
Tulozaliwa upya ndani yako.
Tenzi za fahari, nyimbo za sifa
Tunakuimbia mpenzi Baba;
Na sifa zote milele mpate,
Bwana Mfufuka na wewe Roho.
Karne ya 7
5 (29)
Utangazeni ushindi wake,
Ewe mbingu na wewe dunia,
Maana Kristo amefufuka
Kama mwenyewe alivyosema:
Ndie yule alosulibiwa,
Ni Mungu kweli aliye hai,
Aliyekaa kwa siku tatu
Kati ya wafu huko kuzimu.
Kristo alikufa kwa aibu
Kwa ajili yetu sisi watu,
Lakini sasa aishi tena
Akiwa na nguvu na uweza;
Moto wake na haujazimwa,
Mwali wake unaoangaza
Ulimwengu wote waujaza
Kwa furaha tele na mwangaza.
Sifa na heshima kwake Baba
Ambaye hakika Hakuumbwa,
Na kwa Mwanae aliye hai
Ambaye hakika hakushindwa,
Bali anatawala kwa enzi
Pamoja na Roho wake Mungu,
Utatu ulio Mtukufu,
Katika yeye Mungu Mmoja.
Stanbrook Abbey Hymnal
6 (30)
Njoni, enyi waamini, njoni,
Mkashangilie kwa furaha;
Mungu kawapa Israeli
Furaha baada ya huzuni;
Wana na binti zake Yakobo
Si watumwa tena wa Farao;
Kawavusha miguu mikavu
Katikati ya Bahari ya Shamu.
Leo ndio roho zachipua;
Kristo jela kabomoa,
Japo siku tatu kawa mfu
Leo kachomoza kama jua;
Kipupwe chote cha dhambi zetu,
Cha muda mrefu na cha kiza,
Metokomezwa kwa yako nuru
Wewe tukusifuye daima.
Milango imara ya mauti,
Wala kaburi pana la giza,
Wala walinzi, wala muhuri,
Havikushiki uwe maiti
Maana leo ulisimama.
Kati yao Kumi na Wawili,
Amani yako ukawapatia
Ipitayo ufahamu wetu.
Mt. Yohane wa Damasko yapata 750
7 (31)
Hakika vita sasa vimekwisha,
Majeshi ya motoni yakimbia;
Tupige ukelele wa ushindi
Kwa furaha na shangwe, aleluya.
Kristo aliyeuvumilia
Ule mti utiao aibu,
Twamkaribisha tukimsifu
Aloshinda mauti, aleluya.
Asubuhi ya tatu kafufuka,
Amevishwa nuru ya utukufu.
Ambayo wenye imani thabiti
Mbinguni watavishwa, aleluya.
Ile milango duni ya kuzimu
Ufunguo wao yaachilia,
Mlango wa Paradisi u wazi;
Tusichoke kuimba, aleluya.
Bwana, kwa mapigo tulokupiga,
Tujalie tuwe mbali na kifo,
Ili tuendelee kukariri
Salamu yetu hii, aleluya.
Simphonia Sirenum 1695
ANT. I: Kila nayeishi kadiri ya ukweli, huingia katika mwanga, aleluya.
Zab.119:105-112 XIV Sheria ya Mungu ni mwanga
Hii ndiyo amri yangu: pendaneni; pendaneni kama nilivyowapenda ninyi (Yoh.15:12)
Neno lako ni taa ya kuniongoza,*
na mwanga katika njia yangu.
Nimeapa na kuthibitisha kiapo changu,*
kwamba nitashika maagizo yako maadilifu.
Ee Mungu, ninateseka mno;*
unipe uhai kama ulivyoahidi.
Ee Mungu, upokee sala yangu ya shukrani;*
na unifundishe maagizo yako.
Maisha yangu yamo hatarini daima,*
lakini siisahau sheria yako.
Waovu wamenitegea mtego kuninasa,*
lakini sikiuki amri zako.
Maagizo yako ni rasilimali yangu daima;*
naam, ni furaha ya moyo wangu.
Nimekusudia kwa moyo wote*
kutimiza kanuni zako milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Kila nayeishi kadiri ya ukweli, huingia katika mwanga, aleluya.
ANT. II: Bwana amefufuka; Bwana ameushinda uchungu wa mauti, aleluya.
Zab.16 Kuomba usalama
Mungu alimfufua Yesu, akamwokoa kutoka katika maumivu ya kifo (Mate.2:24)
Unilinde, Ee Mungu;*
nakimbilia usalama kwako.
Nimemwambia Mungu: “Wewe ni Bwana wangu;*
mema yote niliyo nayo yatoka kwako."
Ni bora sana hao watakatifu walioko nchini;*
kukaa nao ndiyo furaha yangu.
Lakini wanaokimbilia miungu mingine,*
wanajizidishia taabu wao wenyewe.
Damu ya matambiko sitawatolea kamwe;*
na majina ya miungu hiyo sitayataja kamwe.
Ee Mungu, wewe peke yako, ndiwe tegemeo langu;/
wewe wanipa mahitaji yangu yote;*
maisha yangu yamo mikononi mwako.
Umenipimia sehemu nzuri sana;*
naam, kila ulichonipa ni kizuri sana.
Nitamtukuza Mungu kwa kuniongoza,*
na usiku dhamiri yangu yanionya.
Namweka Mungu mbele yangu daima,*
yuko karibu nami, wala sitatikisika.
Kwa hiyo nafurahi na kushangilia,*
nami nitakaa salama salimini,
kwani wanikinga na nguvu za kuzimu,*
wala humwachi mpendwa wako apotee huko ahera.
Utanionesha njia ya kufikia uzima;/
kuwako kwako kwanijaza furaha,*
uwezo wako waniletea raha daima.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. II: Bwana amefufuka; Bwana ameushinda uchungu wa mauti, aleluya.
ANT. III: Je, haikumpasa Kristo kuyapata mateso hayo, na kuingia
katika utukufu wake? Aleluya.
WIMBO: Filp.2:6-11 Kristo, mtumishi wa Mungu
Yesu, kwa asili,*
alikuwa daima Mungu;
lakini hakufikiri kwamba/
kule kuwa sawa na Mungu*
ni kitu cha kung'ang'ania kwa nguvu.
Bali, kwa hiari yake mwenyewe,*
aliachilia hayo yote,
akajitwalia hali ya mtumishi/
akawa sawa na wanadamu,*
akaonekana kama wanadamu.
Alijinyenyekeza na kutii mpaka kufa,*
hata kufa msalabani.
Kwa sababu hiyo*
Mungu alimkweza juu kabisa,
akampa jina lililo kuu zaidi*
kuliko majina yote.
Ili kwa heshima ya jina la Yesu,/
viumbe vyote mbinguni, duniani na kuzimu,*
vipige magoti mbele yake;
Na kila mtu akiri/
Kwamba Yesu Kristo ni Bwana,*
kwa utukufu wa Mungu Baba.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
ANT. III: Je, haikumpasa Kristo kuyapata mateso hayo, na kuingia
katika utukufu wake? Aleluya.
SOMO: 1Pet.2:9-10
Ninyi ni ukoo mteule, makuhani wa Mfalme, taifa takatifu; watu wake Mungu mwenyewe, mlioteuliwa
kutangaza matendo makuu ya Mungu aliyewaiteni kutoka gizani, akawaingizeni katika mwanga wake mkuu.
Wakati mmoja ninyi hamkuwa watu wa Mungu, lakini sasa ninyi ni watu wake; wakati mmoja hamkupewa
huruma ya Mungu, lakini sasa mmeipokea.
KIITIKIZANO
K. Wanafunzi walifurahi, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Walimwona Bwana.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Wanafunzi...
Ant. Wimbo wa Bikira Maria
Nitamwomba Baba, naye atawapeni Msaidizi mwingine awe pamoja nanyi milele, aleluya.
WIMBO WA BIKIRA MARIA
Lk.1:46-55 Roho yangu inamfurahia Bwana.
Moyo wangu wamtukuza Bwana,/
Roho yangu inafurahi*
kwa sababu ya Mungu Mwokozi wangu.
Kwa kuwa amemwangalia kwa huruma/
mtumishi wake mdogo,*
hivyo tangu sasa watu wote wataniita mwenye heri.
Kwa kuwa Mwenyezi Mungu amenitendea makuu,*
jina lake ni takatifu.
Huruma yake kwa watu wanaomcha*
hudumu kizazi hata kizazi.
Amefanya mambo makuu kwa mkono wake:*
amewatawanya wenye kiburi katika mawazo ya mioyo yao;
amewashusha wenye vyeo kutoka viti vyao vya enzi,*
akawakweza wanyeyekevu.
Wenye njaa amewashibisha mema,*
matajiri amewaacha waende mikono mitupu.
Amempokea Israeli mtumishi wake,*
akikumbuka huruma yake,
kama alivyowaahidia wazee wetu,*
Abrahamu na uzao wake hata milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Nitamwomba Baba, naye atawapeni Msaidizi mwingine awe pamoja
nanyi milele, aleluya.
MAOMBI
Mungu, Baba yetu, kwa mapendo makubwa hutuongoza mbele kuelekea kwenye siku ya furaha,
tutakapoingia katika pumziko lake.
W. Matumaini yetu yote ni kwako, Ee Bwana Mungu.
Tunawaombea Papa wetu F..., na Askofu wetu F...:
- uwaongoze na uwabariki katika kazi zao. (W.)
Uwasaidie wagonjwa wayavumilie mateso yao pamoja na Kristo,
- ili wapate katika Kristo ukamilifu wa maisha na mapendo. (W.)
Kristo hakuwa na mahali pa kulaza kichwa chake:
- utuwezeshe sisi kutambua shida na haja za wale wasio na maskani. (W.)
Uwabariki wakulima wote:
- utujalie tuyapokee kwa shukrani mazao ya nchi. (W.)
Baba, uwahurumie wale waliofariki dunia wakiwa katika amani ya Kristo:
- uwaingize katika makao uliyokwisha watayarishia. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu:
Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Mungu Mwenyezi, utujalie neema ya kuadhimisha kiaminifu siku hizi za furaha zilizowekwa kwa
ajili ya heshima ya Bwana Mfufuka. Utufundishe kuzingatia kimatendo fumbo hili tunalolikumbuka
katika ibada. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao, anayeishi na kutawala
nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe
kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.