DOMINIKA YA 5 KWARESIMA MWAKA C
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.43:1-2
Ee Bwana, unihukumu, unitetee kwa taifa lisilo haki, uniokoe na mtu wa hila asiye haki. Kwa kuwa wewe ndiwe Mungu uliye nguvu zangu.

KOLEKTA:
Ee Bwana Mungu wetu, tunaomba msaada wako, ili na sisi tuenende kwa ari katika upendo ule ambao kwao Mwanao aliupenda ulimwengu hata akajitoa afe. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Isa.43:16-21
Bwana asema hivi, yeye afanyaye njia katika bahari, na mahali pa kupita katika maji yenye nguvu; atoaye gari na farasi, jeshi la askari na uwezo; wamelala, hawataondoka; wametoweka, wamezimwa mfano wa utambi: Msiyakumbuke mambo ya kwanza, wala msiyatafakari mambo ya zamani. Tazama, nitatenda neno jipya; sasa litachipuka; je, hamtalijua sasa? Nitafanya njia hata jangwani, na mito ya maji nyikani. Wanyama wa kondeni wataniheshimu, mbweha pia na mbuni; kwa sababu nimewapa maji jangwani, na mito nyikani, ili kuwanywesha watu wangu, wateule wangu; watu wale niliojiumbia nafsi yangu, ili wazitangaze sifa zangu.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.126,(K)3
1. Bwana alipowarejeza mateka wa Sayuni,
Tulikuwa kama waotao ndoto.
Ndipo kinywa chetu kilipojaa kicheko.
Na ulimi wetu kelele za furaha.

(K) Bwana alitutendea mambo makuu,
Tulikuwa tukifurahi.

2. Ndipo waliposema katika mataifa,
Bwana amewatendea mambo makuu.
Bwana alitutendea mambo makuu,
Tulikuwa tukifurahi. (K)

3. Ee Bwana, uwarejeze watu wetu waliofungwa,
Kama vijito vya kusini.
Wapandao kwa machozi
Watavuna kwa kelele za furaha. (K)

4. Ingawa mtu anakwenda zake akilia,
Azichukuapo mbegu za kupanda.
Hakika atarudi kwa kelele za furaha,
Aichukuapo miganda yake. (K)

SOMO 2: Flp.3:8-14
Nayahesabu mambo yote kuwa hasara kwa ajili ya uzuri usio na kiasi wa kumjua Kristo Yesu, Bwana wangu; ambaye kwa ajili yake nimepata hasara ya mambo yote nikiyahesabu kuwa kama mavi ili nimpate Kristo; tena nionekane katika yeye, nisiwe na haki yangu mwenyewe ipatikanayo kwa sheria, bali ile ipatikanayo kwa imani iliyo katika Kristo, haki ile itokayo kwa Mungu, kwa imani; ili nimjue yeye, na uweza wa kufufuka kwake, na ushirika wa mateso yake, nikifananishwa na kufa kwake; ili nipate kwa njia yoyote kuifikia ufufuo wa wafu. Si kwamba nimekwisha kufika, au nimekwisha kuwa mkamilifu; la! bali nakaza mwendo ili nipate kulishika lile ambalo kwa ajili yake nimeshikwa na Kristo Yesu. Ndugu, sijidhanii nafsi yangu kwamba nimekwisha kushika; ila natenda neno moja tu; nikiyasahau yaliyo nyuma, nikiyachuchumilia yaliyo mbele; nakaza mwendo, niifikilie mede ya thawabu ya mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu.

SHANGILIO: Yoe.2:12,13
Lakini hata sasa, asema Bwana,
nirudieni mimi kwa mioyo yenu yote,
kwa maana ni mwenye neema na huruma.

INJILI: Yn.8:1-11
Yesu akaenda mpaka mlima wa Mizeituni. Hata asubuhi kulipokucha akaingia tena hekaluni, na watu wote wakamwendea; naye akaketi, akawa akiwafundisha. Waandishi na Mafarisayo wakamletea mwanamke aliyefumaniwa katika uzinzi, wakamweka katikati. Wakamwambia, Mwalimu, mwanamke huyu amefumaniwa alipokuwa akizini. Basi katika torati, Musa alituamuru kuwapiga kwa mawe wanawake namna hii; nawe wasemaje? Nao wakasema neno hilo wakimjaribu, ili wapate sababu ya kumshitaki. Lakini Yesu akainama, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao walipozidi kumhoji, alijiinua, akawaambia, Yeye asiye na dhambi miongoni mwenu na awe wa kwanza wa kumtupia jiwe. Akainama tena, akaandika kwa kidole chake katika nchi. Nao waliposikia, wakashitakiwa na dhamiri zao, wakatoka mmoja mmoja, wakianzia tangu wazee hata wa mwisho wao; akabaki Yesu peke yake, na yule mwanamke amesimama katikati. Yesu akajiinua asimwone mtu ila yule mwanamke, akamwambia, Mwanamke, wako wapi wale washitaki wako? Hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Akamwambia, Hakuna Bwana. Yesu akamwambia, Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako; wala usitende dhambi tena.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ndugu zangu, mafarisayo walimfumainia mwanamke mzinzi na kumpeleka mbele ya Yesu ili amhukumu! Yesu alimhurumia na kumsamehe, kwa kuwa washtaki wake wote walitenda dhambi vile vile wala hawakuwa na haki ya kumhukumu mwenzao.

Tumuombe Yesu,
1. Ee Bwana Yesu, udhaifu wetu wa kibinadmu unatuangusha kutenda dhambi. Uuangalie udhaifu wetu na kutusamehe makosa yote ya udhaifu wetu.

2. Ulimsamehe mama aliyefumainiwa akitenda dhambi. Tunaomba Utusamehe sisi makosa ya dhambi za siri.

3. Ulimwokoa mama aliyefumaniwa katika hukumnu ya kifo: Utuokoe sisi na hukumu ya milele na utukaribishe kwenye makao ya uzima wa milele.

4. Watu wanamhukumu mtu kadiri ya matendo wanayoona lakini wewe unasoma moyo wa mtu: Utusaidie, tusimhukumu mtu kadiri ya kipimo chetu cha kibinadamu.

5. Sisi sote tu wakosefu, kwa hiyo hatuna haki ya kumhukumu mtu. Utuwezeshe tuwatendee wenzetu haki badala ya kuwahukumu.

6. Ulituonesha kwamba msamaha unaweza kumbadilisha mtu tabia: Utuoneshe njia ya kuwasamehe wote waliotukosea.

Ee Mungu Baba, Mwana wako wa pekee alituonesha kwamba msamaha unamrekebisha mtu. Utusaidie kumfuata mfano wake anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu daima na milele. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Mungu mwenyezi, utusikilize, na uwajalie watumishi wako uliowaangaza kwa mafundisho ya imani ya kikristo, watakaswe kwa nguvu ya sadaka hii. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Yn.8:10-11
Mwanamke, hakuna aliyekuhukumu kuwa na hatia? Hakuna, Bwana. Wala mimi sikuhukumu. Enenda zako, wala usitende dhambi tena

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Mungu mwenyezi, tunakuomba tuhesabiwe daima kama viungo vyake Yeye, ambaye tunashiriki Mwili na Damu yake. Anayeishi na kutawala milele na milele.

SALA YA KUWAOMBEA WAAMINI:
Ee Bwana, uwabariki watu wako, wanaotarajia kupata zawadi ya rehema yako, na uwajalie ili wanachotamani kwa uvuvio wako wakipate kwa ukarimu wako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.