DOMINIKA 4 YA PASAKA MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.33:5-6
Nchi imejaa fadhili za Bwana; kwa neno la Bwana mbingu zilifanyika, aleluya!
Utukufu husemwa.
KOLEKTA
Ee Mungu mwenyezi wa milele, utuongoze hadi kushiriki furaha za mbinguni; ili sisi kundi la
kondoo wako wanyonge tufike huko alikotangulia mchungaji wetu shujaa. kwa njia ya Bwana wetu
Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele
na milele.
SOMO 1: Mdo.13:14,43-52
Paulo na Barnaba walitoka Perge, wakapita kati ya nchi, wakafika Antiokia, mji wa Pisidia,
wakaingia katika sinagogi siku ya sabato, wakaketi. Sinagogi ilipofumukana, Wayahudi na waongofu
watauwa wengi wakashikamana na Paulo na Barnaba; ambao, wakisema nao, wakawatia moyo kudumu katika
neema ya Mungu. Hata sabato ya pili, watu wengi, karibu mji wote, wakakusanyika walisikie neno
la Mungu. Bali Wayahudi walipowaona makutano, wakajaa wivu, wakayakanusha maneno yaliyonenwa na
Paulo, wakibisha na kutukana. Paulo na Barnaba wakanena kwa ushujaa wakasema, Ilikuwa lazima neno
la Mungu linenwe kwenu kwanza; lakini kwa kuwa mnalisukumia mbali, na kujiona nafsi zenu kuwa
hamkustahili uzima wa milele, angalieni, twawageukia Mataifa. Kwa sababu ndivyo tulivyoamriwa na
Bwana, Nimekuweka uwe nuru ya Mataifa, Upate kuwa wokovu hata mwisho wa dunia. Mataifa waliposikia
hayo wakafurahi, wakalitukuza neno la Bwana, nao waliokuwa wamekusudiwa uzima wa milele wakaamini.
Neno la Bwana likaenea katika nchi ile yote. Lakini Wayahudi wakawafitinisha wanawake watauwa
wenye cheo na wakuu wa mji, wakawataharakisha watu wawaudhi Paulo na Barnaba; wakawatoa katika
mipaka yao. Nao wakawakung'utia mavumbi ya miguu yao, wakaenda Ikonio. Na wanafunzi walijaa
furaha na Roho Mtakatifu.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.100:1-3,5 (K)3
1. Mfanyieni Bwana shangwe, dunia yote;
Mtumikieni Bwana kwa furaha;
Njoni mbele zake kwa kuimba.
(K)Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake.
au:
Aleluya!
2. Jueni kwamba Bwana ndiye Mungu;
Ndiye aliyetuumba na sisi tu watu wake;
Tu watu wake, na kondoo wa malisho yake. (K)
3. Kwa kuwa Bwana ndiye mwema;
Rehema zake ni za milele;
Na uaminifu wake vizazi na vizazi. (K)
SOMO 2: Ufu.7:9,14-17
Wakati ule, mimi, Yohane, niliona, na tazama, mkutano mkubwa sana ambao hapana mtu awezaye
kuuhesabu, watu wa kila taifa, na kabila, na jamaa, na lugha, wamesimama mbele ya kile kiti
cha enzi, na mbele za Mwanakondoo, wamevikwa mavazi meupe, wana matawi ya mitende mikononi
mwao. Mmoja wa wale wazee akaniambia, Hao ndio wanatoka katika dhiki ile iliyo kuu, nao wamefua
mavazi yao, na kuyafanya meupe katika damu ya Mwanakondoo. Kwa hiyo wako mbele ya kiti cha enzi
cha Mungu, nao wanamtumikia mchana na usiku katika hekalu lake, na yeye aketiye katika kiti cha
enzi atatanda hema yake juu yao. Hawataona njaa tena, wala hawataona kiu tena, wala jua
halitawapiga, wala hari iliyo yote. Kwa maana huyo Mwanakondoo, aliye katikati ya kiti cha enzi,
atawachunga, naye atawaongoza kwenye chemchemi za maji yenye uhai, na Mungu atayafuta machozi
yote katika macho yao.
SHANGILIO: Yn.10:14
Aleluya, aleluya!
Mimi ndimi mchungaji mwema;
nao walio wangu nawajua;
Nao walio wangu wanijua mimi .
Aleluya!
INJILI: Yn.10:27-30
Yesu alisema, Kondoo wangu waisikia sauti yangu; nami nawajua, nao wanifuata. Nami nawapa uzima
wa milele; wala hawatapotea kamwe; wala hakuna mtu atakayewapokonya katika mkono wangu. Baba
yangu aliyenipa hao ni mkuu kuliko wote; wala hakuna mtu awezaye kuwapokonya katika mkono wa Baba
yangu. Mimi na Baba tu umoja.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Ndugu wapendwa, tunasikia sauti ya Yesu anayetuita kwa njia mbalimbali. Yesu anayetuita anatuumbia
moyo wa kufahamu sauti yake.
Tuombe,
1. Ee Bwana Yesu, uliahidi kutupa uzima wa kweli. Utuwezeshe kuthamini uhai wa kila mmoja kama zawadi
ya thamani kubwa uliyotujalia.
2. Ee Bwana Yesu, ulisema kwamba hakuna awezaye kutupokonya katika mikono yako. Ushike mikono yetu na
kutuongoza, kama ulivyoishika mikono ya Petro aliyetaka kuzama baharini.
3. Ee Bwana Yesu ulisema kwamba Baba ni mkubwa kupita vitu vyote. Utusaidie kutegemea zaidi msaada wa
Mungu katika shida zetu.
4. Ee Bwana Yesu uliye mchungaji wetu: Usituache kamwe bali utuokoe katika hatari ya kujitenga nawe.
5. Ee Bwana Yesu, Uwe mwanga wetu katika giza la mashaka yetu, Uwe msaada katika shida, Uwe kimbilio
katika hatari.
Ee Mungu Baba, tunakushukuru kwa njia ya Mwana wako aliyekuja kwetu awe kiongozi wetu katika mabonde
ya shida na giza duniani hapa. Utusaidie tusiache kusikia sauti yake Bwana wetu anayeishi na kutawala
pamoja nawe na Roho Mtakatifu, daima na milele. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, tunakuomba utujalie tufurahi daima katika kuadhimisha mafumbo haya ya Pasaka, ili
kazi ya ukombozi inayoendelea kutimizwa ndani yetu iwe kwetu sababu ya furaha ya milele. Kwa
njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Lk.24:46-47
Amefufuka Mchungaji mwema, aliyeutoa uhai wake kwa ajili ya kondoo zake, akakubali kufa kwa
ajili ya kundi lake, aleluya!
SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Mchungaji mwema, ulitazame kwa wema kundi lako. Nao kondoo, uliowakomboa kwa damu ya thamani
ya Mwanao, upende kuwaweka kwenye malisho ya milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.