DOMINIKA YA 4 MAJILIO

MASOMO MWAKA A

ANTIFONA YA KUINGIA: Isa.45:8 Vulg.
Dondokeni, enyi mbingu, toka juu, mawingu na yammwage mwenye haki; nchi ifunuke, na kumtoa Mwokozi.

KOLEKTA
Ee Bwana, tunakuomba utie neema yako mioyoni mwetu, ili sisi tuliojua kwa ujumbe wa Malaika kwamba Kristo Mwanao amejifanya mtu, kwa mateso na msalaba wake tufikishwe kwenye utukufu wa ufufuko. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Isa.7:10-14
Siku zile, Bwana akasema na Ahazi akinena, Jitakie ishara ya Bwana, Mungu wako; itake katika mahali palipo chini sana, au katika mahali palipo juu sana. Lakini Ahazi akasema, Sitaitaka, wala sitamjaribu Bwana. Naye akasema, Sikilizeni sasa, enyi nyumba ya Daudi; Je, ni neno dogo kwenu kuwachosha wanadamu, hata mkataka kumchosha Mungu wangu pia? Kwa hiyo Bwana mwenyewe atawapa ishara. Tazama, bikira atachuua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli. (Yaani Mungu pamoja nasi).

WIMBO WA KATIKATI: Zab.24:1-6(K)7,10
1. Nchi na vyote viijazavyo ni mali ya Bwana,
Dunia na wote wakaao ndani yake.
Maana ameiweka misingi yake juu ya bahari,
Na juu ya mito ya maji aliithibitisha.

(K) Mfalme mtukufu apate kuingia, Yeye ndiye Mfalme mtukufu.

2. Ni nani atakayepanda katika mlima wa Bwana?
Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?
Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe.
Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili. (K)

3. Atapokea baraka kwa Bwana,
Na haki kwa Mungu wa wokovu wake.
Hiki ndicho kizazi cha wamtafutao,
Wakutafutao uso wako, Ee Mungu wa Yakobo. (K)

SOMO 2: Rum.1:1-7
Paulo mtumwa wa Kristo Yesu, aliyeitwa kuwa mtume, na kutengwa aihubiri Injili ya Mungu; ambayo Mungu amekwisha kuiahidi kwa kinywa cha manabii wake katika Maandiko Matakatifu. Yaani, habari za Mwanawe, aliyezaliwa katika ukoo wa Daudi kwa jinsi ya mwili, na kudhihirishwa kwa uweza kuwa Mwana wa Mungu, kwa jinsi ya roho ya utakatifu, kwa ufufuo wa wafu, Yesu Kristo Bwana wetu; ambaye katika yeye tulipokea neema na utume ili mataifa yote wapate kujitiisha kwa imani, kwa ajili ya jina lake; ambao katika hao ninyi mmekuwa wateule wa Yesu Kristo; kwa wote walioko Rumi, wapendwao na Mungu, walioitwa kuwa watakatifu. Neema na iwe kwenu na amani itokayo kwa Mungu Baba yetu, na kwa Bwana Yesu Kristo.

SHANGILIO: Mt.1:23
Aleluya, aleluya!
Tazama bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana, Nao watamwita jina lake Imanueli: yaani Mungu pamoja nasi.
Aleluya!

SOMO 3: INJILI: Mt.1:18-25
Kuzaliwa kwake Yesu Kristo kulikuwa hivi. Mariamu mama yake alipokuwa ameposwa na Yusufu, kabla hawajakaribiana, alionekana ana mimba kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye Yusufu, mumewe, kwa vile alivyokuwa mtu wa haki, asitake kumwaibisha, aliazimu kumwacha kwa siri. Basi alipokuwa akifikiri hayo, tazama, malaika wa Bwana alimtokea katika ndoto, akisema, Yusufu, mwana wa Daudi, usihofu kumchukua Mariamu mkeo, maana mimba yake ni kwa uweza wa Roho Mtakatifu. Naye atazaa mwana, nawe utamwita jina lake Yesu, maana, yeye ndiye atakayewaokoa watu wake na dhambi zao. Hayo yote yamekuwa, ili litimie neno lililonenwa na Bwana kwa ujumbe wa Nabii akisema, Tazama, bikira atachukua mimba, Naye atazaa mwana; Nao watamwita jina lake Imanueli; Yaani, Mungu pamoja nasi. Naye Yusufu alipoamka katika usingizi, alifanya kama malaika wa Bwana alivyomwagiza; akamchukua mkewe.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Mungu alimtayarishia Mwana wake makao ya hapa duniani kwa kumchagua Mtakatifu Yosef awe baba mlishi wa familia takatifu, na kumteua Bikira Maria awe mama wa Mkombozi. Ee Mungu Mwenyezi,

1. Utusaidie kupokea kazi na wajibu ambazo umetukabidhi tuzitimize.

2. Uwajalie wakina baba wa familia ukarimu wa baba mlishi Yosef katika kuyaangalia mahitaji ya familia zao.

3. Uwaamshe wakina mama wa familia kutimiza vema kazi ya kuwalea watoto wao, kuwatunza na kuwaongoza katika njia ya imani.

4. Utupe sisi sote neema za kuitikia mwito wetu tuliopangiwa tuufuate kwa uaminifu.

5. Utupe moyo wa kuwatunza wazee wetu, kuwasaidia maskini, na kuwatayarishia wote wasiojiweza misaada ya kuyafanya maisha yao mazuri.

6. Uwakumbushe watu waliopewa wadhifa kutimiza mamlaka yao kwa manufaa ya watu waliokabidhiwa.

Tunaomba hayo kwa jina la Bwana wetu Yesu Kristo.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, Roho yule ambaye kwa uwezo wake Maria mwenye heri alipata mimba, avitakase vipaji vyetu tulivyoviweka juu ya altare yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

1. UTANGULIZI WA MAJILIO:
MAJILIO II:

K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye ambaye alitabiriwa na maaguzi ya manabii wote, Mama Bikira alimchukua kwa upendo wa ajabu, na Yohane Mbatizaji alishangilia kuja kwake na kumtambulisha alipofika. Yeye aliyetujalia kungojea kwa furaha fumbo la kuzaliwa kwake, atukute tukikesha katika sala na tukimshangilia kwa nyimbo za kumsifu.
Kwa sababu hiyo, sisi pamoja na Malaika na Malaika wakuu, pamoja na Viti vya enzi na Milki, na majeshi yote ya Malaika wa mbinguni, twaimba utenzi wa utukufu wako, tukisema bila mwisho:

W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Isa.7:14
Tazama, Bikira atachukua mimba, atazaa mtoto mwanamume, naye atamwita jina lake Imanueli.

SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Mungu mwenyezi, tumekwisha pokea amana ya ukombozi wa milele. Tunaomba jinsi inavyokaribia hiyo sikukuu ituleteayo wokovu, hivyo zizidi bidii za ibada yetu, tupate kuliadhimisha vema fumbo la kuzaliwa kwake Mwanao. Anayeishi na kutawala milele na milele.