DOMINIKA 3 YA PASAKA MWAKA C
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.66:1-2
Mpigie Mungu kelele za shangwe, nchi yote, imbeni utukufu wa jina lake. Tukuzeni sifa zake, aleluya.

Utukufu husemwa.

KOLEKTA

Ee Mungu, watu wako washangilie daima, kwa kujaliwa ujana mpya wa roho, ili, wanaofurahi sasa kwa kurudishiwa utukufu wa kuwa wanao, waitazamie kwa tumaini la furaha thabiti ile siku ya ufufuko. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Mdo.5:27b-32,40b-41
Kuhani Mkuu aliwauliza Mitume, akisema, Je, hatukuwaamuru ninyi kwa nguvu, msifundishe kwa jina hili? Nanyi, tazameni, mmeijaza Yerusalemu mafundisho yenu, na mnataka kuileta damu ya mtu yule juu yetu. Petro na mitume wakajibu, wakasema Imetupasa kumtii Mungu kuliko wanadamu. Mungu wa baba zetu alimfufua Yesu, ambaye ninyi mlimwua mkimtundika katika mti. Mtu huyo Mungu amemtukuza kwa mkono wake wa kuume, awe Mkuu na Mwokozi, awape Waisraeli toba na msamaha wa dhambi. Na sisi tu mashahidi wa mambo haya, pamoja na Roho Mtakatifu ambaye Mungu amewapa wote wamtiio. Nao walipowaita mitume, wakawapiga, wakawaamuru wasinene kwa jina lake Yesu; kisha wakawaacha waende zao. Nao wakatoka katika ile baraza, wakifurahi kwa sababu wamehesabiwa kuwa wamestahili kuaibishwa kwa ajili ya Jina hilo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.30:1,3,5,10-12(K)1
1. Ee Bwana, nitakutukuza kwa maana umeniinua,
Wala hukuwafurahisha adui zangu juu yangu.
Umeniinua nafsi yangu,
Ee Bwana, kutoka kuzimu.
Umenihuisha na kunitoa
Miongoni mwao washukao shimoni.

(K) Ee Bwana, Mungu wangu,
Nalikulilia ukaniponya.
Au:
Aleluya.

2. Mwimbieni Bwana zaburi,
Enyi watauwa wake,
Na kufanya shukrani,
Kwa kumbukumbu la utakatifu wake.
Maana ghadhabu zake ni za kitambo kidogo,
Katika radhi yake mna uhai.
Huenda kilio huja kukaa usiku,
Lakini asubuhi huwa furaha. (K)

3. Ee Bwana, usikie, unirehemu,
Bwana, uwe msaidizi wangu.
Uligeuza matanga yangu kuwa machezo;
Ulinivua gunia, ukanivika furaha.
Ee Bwana, Mungu wangu,
Nitakushukuru milele. (K)

SOMO 2: Ufu.5:11-14
Mimi, Yohane, niliona nikasikia sauti ya malaika wengi pande zote za kile kiti cha enzi, na za wale wenye uhai, na za wale wazee, na hesabu yao ilikuwa elfu kumi mara elfu kumi na elfu mara elfu, wakisema kwa sauti kuu, Astahili Mwanakondoo aliyechinjwa, kuupokea uweza na utajiri na hekima na nguvu na heshima na utukufu na baraka. Na kila kiumbe kilichoko mbinguni na juu ya nchi na chini ya nchi na juu ya bahari, na vitu vyote vilivyomo ndani yake, nalivisikia, vikisema, Baraka na heshima na utukufu na uweza una yeye aketiye juu ya kiti cha enzi, na yeye Mwanakondoo, hata milele na milele. Na wale wenye uhai wanne wakasema, Amina. Na wale wazee wakaanguka, wakasujudu.

SHANGILIO: Lk.24:32
Aleluya, aleluya!
Bwana Yesu, utufunulie Maandiko;
Uwashe mioyo yetu unaposema nasi.
Aleluya!

INJILI: Yn.21:1-19
Siku ile, Yesu alijidhihirisha tena kwa wanafunzi wake, penye bahari ya Tiberia, naye alijidhihirisha hivi. Simoni Petro, na Tomaso aitwaye Pacha, na Nathanaeli wa Kana ya Galilaya, na wana wa Zebedayo, na wengine wawili wa wanafunzi wake, walikuwapo pamoja. Simoni Petro aliwaambia, Naenda kuvua samaki. Nao wakamwambia, Sisi nasi tutakwenda nawe. Basi wakaondoka, wakapanda chomboni; ila usiku ule hawakupata kitu. Hata asubuhi kulipokucha, Yesu alisimama ufuoni; walakini wanafunzi hawakujua ya kuwa ni Yesu. Basi Yesu akawaambia, Wanangu, mna kitoweo? Wakamjibu, La. Akawaambia, Litupeni jarife upande wa kuume wa chombo, nanyi mtapata. Basi wakatupa; wala sasa hawakuweza kulivuta tena kwa sababu ya wingi wa samaki. Basi yule mwanafunzi ambaye Yesu alimpenda akamwambia Petro, Ndiye Bwana. Naye Simoni Petro, aliposikia ya kwamba ni Bwana, akajifunga vazi lake, (maana alikuwa uchi), akajitupa baharini. Nao hao wanafunzi wengine wakaja katika mashua; maana hawakuwa mbali na nchi kavu; ila yapata dhiraa mia mbili, huku wakilikokota lile jarife lenye samaki. Basi waliposhuka pwani, wakaona huko moto wa makaa, na juu yake pametiwa samaki, na mkate. Yesu akawaambia, Leteni hapa baadhi ya samaki mliowavua sasa hivi. Basi Simoni Petro akapanda chomboni, akalivuta jarife pwani, limejaa samaki wakubwa, mia hamsini na watatu; na ijapokuwa ni wengi namna hiyo, jarife halikupasuka. Yesu akawaambia, Njoni mfungue kinywa. Wala hakuna mtu katika wale wanafunzi aliyethubutu kumwuliza, U nani wewe? Wakijua ya kuwa ni Bwana. Yesu akaenda akautwaa mkate, akawapa, na samaki vivyo hivyo. Hiyo ndiyo mara ya tatu ya Yesu kuonekana na wanafunzi wake baada ya kufufuka katika wafu. Basi walipokwisha kula, Yesu akamwambia Simoni Petro, Je, Simoni wa Yohane, wewe wanipenda kuliko hawa? Akamwambia, Naam, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Lisha wanakondoo wangu. Akamwambia tena mara ya pili, Simoni wa Yohane wanipenda? Akamwambia, Ndiyo, Bwana, wewe wajua kuwa nakupenda. Akamwambia, Chunga kondoo zangu. Akamwambia mara ya tatu, Simoni wa Yohane, wanipenda? Petro alihuzunika kwa vile alivyomwambia mara ya tatu, Wanipenda? Akamwambia, Bwana, wewe wajua yote; wewe umetambua ya kuwa nakupenda. Yesu akamwambia, Lisha kondoo zangu. Akasema, Amin, amin, nakuambia, Wakati ulipokuwa kijana, ulikuwa ukijifunga mwenyewe na kwenda utakako; lakini utakapokuwa mzee, utainyosha mikono yako na mwingine atakufunga na kukuchukua usikotaka. Akasema neno hilo kwa kuonesha ni kwa mauti gani atakayomtukuza Mungu. Naye akiisha kusema hayo, akamwambia, Nifuate.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ndugu zangu, ingawa wafuasi waliisharudia kazi yao ya kawaida ya uvuvi, waligundua kwamba Bwana mfufuka yupo pamoja nao. Uvuvi wa samaki ni mfano wa uchungaji ambao mitume watakabidhiwa na Yesu mfufuka.

Tuombe,
1. Ee Bwana Yesu, uliwaambia Petro na wenzake watupe jarife ili kuvua samaki. Utusaidie katika shughuli zetu za uchungaji ili kuwaongoza wenzetu kwako.

2. Wafuasi walifanya kazi ngumu katika ziwa, lakini walifanikiwa kuvuta samaki mpaka pwani kwenye usalama. Ubariki kazi zetu zitoe matunda ya uzima wa milele.

3. Tunawajibika kukazana ili kufika kwako unapotungojea. Utusaidie kushika njia inayotuongoza kwenye usalama wa bandari yako ya heri.

4. Ulimchagua Petro kuwa kiongozi wa waumini wako na kumhakikishia wadhifa wake. Uwaimarishe Baba Mtakatifu wetu J. na Askofu wetu J. katika kazi yao ya uchungaji.

Ee Mungu Baba, uyasikilize maombi yetu kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, tunakuomba uvipokee vipaji vya kanisa linalofanya shangwe; na wale uliowafanya wafurahi sana sasa, uwajalie pia tunda la furaha ya milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Lk.24:46-47
Ilimpasa Kristo ateswe, na kufufuka katika wafu siku ya tatu; na kwamba mataifa yote watahubiriwa kwa jina lake habari ya toba, na ondoleo la dhambi, alaluya!

SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Bwana, tunakuomba uwaangalie kwa wema watu wako, nao uliopenda kuwafanya wapya kwa mafumbo ya milele, uwajalie waufikie ufufuko usioharibika wa miili itakayotukuzwa. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.