JUMAPILI JUMA LA 3 PASAKA
MASIFU YA ASUBUHI
K. Ee Bwana, uifungue midomo yetu.
W. Nasi tutalisifu jina lako.
ANTIFONA YA MWALIKO:
Bwana amefufuka kweli, aleluya.
(K. Ant. ya Mwaliko - W. warudie Ant.)
Zab.95: Utenzi wa kumsifu Mungu
Njoni tumwimbie Mungu;
tumshangilie mwamba wa wokovu wetu!
Tuiongie kwake na nyimbo za shukrani;
tumshangilie kwa nyimbo za sifa. (W.Ant.)
Maana Mungu, ni Mungu Mkuu.
Mfalme mkuu juu ya miungu yote.
Dunia yote imo mikononi mwake,
mabonde, na vilele vya milima.
Bahari ni yake, ndiye aliyeifanya;
nchi kavu kadhalika, yeye aliiumba. (W.Ant.)
Njoni tusujudu na kumwabudu;
tumpigie magoti Mungu, Mwumba wetu!
Maana yeye ni Mungu wetu!
Nasi ni watu anaowalinda,
ni kondoo wake anaowachunga. (W.Ant.)
Laiti leo mngelisikiliza anachosema:
"Msiwe na mioyo migumu kama wazee wenu kule Meriba,
kama walivyokuwa siku ile, kule Masa jangwani!
Huko wazee wenu walinijaribu na kunipima,
ingawa waliyaona mambo niliyowatendea. (W.Ant.)
Kwa miaka arobaini nilichukizwa nao,
nikasema: 'Kweli hawa ni watu waliopotoka!
Hawajali kabisa mwongozo wangu!'
Basi, nilikasirika, nikaapa:
'Hawataingia kwangu wapumzike!' (W.Ant.)
Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu,
kama mwanzo, na sasa, na siku zote na milele.
Amina. (W.Ant.)
UTENZI chagua 1-7(25-31)
1 (25)
Kristo Bwana amefufuka!
Kila mnyororo Bwana kakata,
Sikilizeni, hao malaika
Makelele kwa shangwe wanapiga,
Milele mbinguni juu waimba,
Aleluya!
Aliyekufa kwa ajili yetu,
Na mateso mengi kuvumilia -
Kuvumilia kwa ajili yetu,
Ni Kondoo wetu wa Paska leo!
Nasi pia kwa shangwe tunaimba.
Aleluya!
Yeye aliyepata maumivu
Na hasara yote msalabani,
Sasa yupo katika utukufu,
Akitwombea, huko mbinguni,
Na anasikia kilio chetu.
Aleluya!
Sasa atuagiza tutangaze
Pote pote ulimwenguni jinsi
Ya kuokoka waliopotea,
Na ya kusamehewa wenye toba,
Na tuwezavyo ingia mbinguni.
Aleluya!
Mikaeli Weisse yapata 1480-1534
2 (26)
Aleluya! Aleluya!
Angani inatanda Pasaka!
Yesu ni mzima, hafi tena!
Giza limetokomezwa lote,
Na Bwana wa nuru Mfufuka!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Mama Maria mwone Mwanao,
Anavyofurahi kwa ushindi!
Mateso mlishiriki nyote,
Milele mtatawala nyote!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Watafuta waliopotea!
Naye Petro anakulilia!
Mwimarishe awe mwamba,
Kundi lako alichunge!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Mzima haishi kaburini,
Kristo yupo ghorofani!
Utukufu wake kauficha,
Mwili wake hai aonesha!
Aleluya! Aleluya!
Aleluya! Aleluya!
Japo uso wake hatuoni,
Yupo na sisi kama mwanzoni!
Ni padre wetu mtukufu,
Twashangilia mtu mzima!
Aleluya! Aleluya!
Yakobo Quinn SJ
3 (27)
Aleluya, mwimbieni Yesu,
Enzi na ufalme ni vyake.
Aleluya, fanaka ni yake,
Ushindi ni wake peke yake.
Sikizeni, nyimbo za Sion
Zinanguruma kama tufani,
Zinasikika kama gharika:
Kwa damu yake ilo azizi,
Yesu ametukomboa sisi,
Watu kutoka kila taifa.
Aleluya, katika huzuni
Kama yatima hatujaachwa;
Aleluya, yu karibu nasi,
Imani yasadiki kabisa,
Haiulizi kwa jinsi gani
Ingawa Bwana alitoweka,
Akafunikwa nayo mawingu
Siku ile ya arobaini,
Tutasahau ahadi yake:
'Nipo nanyi daima milele'?
S. S. Wesley 1810-1876
4 (28)
Kwenye Karamu ya Mwana-Kondoo
Mfalme mshindi twamwimbia,
Alotuosha kwa wingi wa maji
Kutoka penye tobo ubavuni.
Yeye analo pendo la kimungu
Waalikwa wanyweshwa damu yake,
Na awapa waule mwili wake
Pendo ndilo kafara na kuhani.
Panapomwagwa damu ya Pasaka
Mwuaji upanga aufutika;
Jeshi la Israeli lapita
Askari adui wafa maji.
Kristo kondoo aliyechinjwa,
Kafara na mkate wa Pasaka;
Tuile manna itokayo juu
Kwa unyofu na upendo halisi.
Kafara shujaa kutoka juu,
Nguvu za kuzimu ni chini yako;
Vitani mauti umeyashinda,
Uzima na mwanga kutuletea.
Bendera sasa waipeperusha,
Shetani na kaburi watiisha;
Malaika waungana kusifu
Kupinduliwa kwa bwana shetani.
Ushindi na furaha ya Pasaka
Dhambi tu ndo yaweza viharibu;
Tukinge na kifo cha dhambi Bwana,
Tulozaliwa upya ndani yako.
Tenzi za fahari, nyimbo za sifa
Tunakuimbia mpenzi Baba;
Na sifa zote milele mpate,
Bwana Mfufuka na wewe Roho.
Karne ya 7
5 (29)
Utangazeni ushindi wake,
Ewe mbingu na wewe dunia,
Maana Kristo amefufuka
Kama mwenyewe alivyosema:
Ndie yule alosulibiwa,
Ni Mungu kweli aliye hai,
Aliyekaa kwa siku tatu
Kati ya wafu huko kuzimu.
Kristo alikufa kwa aibu
Kwa ajili yetu sisi watu,
Lakini sasa aishi tena
Akiwa na nguvu na uweza;
Moto wake na haujazimwa,
Mwali wake unaoangaza
Ulimwengu wote waujaza
Kwa furaha tele na mwangaza.
Sifa na heshima kwake Baba
Ambaye hakika Hakuumbwa,
Na kwa Mwanae aliye hai
Ambaye hakika hakushindwa,
Bali anatawala kwa enzi
Pamoja na Roho wake Mungu,
Utatu ulio Mtukufu,
Katika yeye Mungu Mmoja.
Stanbrook Abbey Hymnal
6 (30)
Njoni, enyi waamini, njoni,
Mkashangilie kwa furaha;
Mungu kawapa Israeli
Furaha baada ya huzuni;
Wana na binti zake Yakobo
Si watumwa tena wa Farao;
Kawavusha miguu mikavu
Katikati ya Bahari ya Shamu.
Leo ndio roho zachipua;
Kristo jela kabomoa,
Japo siku tatu kawa mfu
Leo kachomoza kama jua;
Kipupwe chote cha dhambi zetu,
Cha muda mrefu na cha kiza,
Metokomezwa kwa yako nuru
Wewe tukusifuye daima.
Milango imara ya mauti,
Wala kaburi pana la giza,
Wala walinzi, wala muhuri,
Havikushiki uwe maiti
Maana leo ulisimama.
Kati yao Kumi na Wawili,
Amani yako ukawapatia
Ipitayo ufahamu wetu.
Mt. Yohane wa Damasko yapata 750
7 (31)
Hakika vita sasa vimekwisha,
Majeshi ya motoni yakimbia;
Tupige ukelele wa ushindi
Kwa furaha na shangwe, aleluya.
Kristo aliyeuvumilia
Ule mti utiao aibu,
Twamkaribisha tukimsifu
Aloshinda mauti, aleluya.
Asubuhi ya tatu kafufuka,
Amevishwa nuru ya utukufu.
Ambayo wenye imani thabiti
Mbinguni watavishwa, aleluya.
Ile milango duni ya kuzimu
Ufunguo wao yaachilia,
Mlango wa Paradisi u wazi;
Tusichoke kuimba, aleluya.
Bwana, kwa mapigo tulokupiga,
Tujalie tuwe mbali na kifo,
Ili tuendelee kukariri
Salamu yetu hii, aleluya.
Simphonia Sirenum 1695
ANT. I: Bwana ni mfalme, amefunikwa enzi, aleluya.
Zab.93 Mungu mfalme
Bwana, Mungu wetu Mwenyezi, ni Mfalme! Tufurahi. na kushangilia; tumtukuze (Ufu.19:6-7)
Mungu anatawala, amejivika fahari!/
Mungu amevaa fahari na nguvu!*
Ameuimarisha ulimwengu, hautatikisika kamwe.
Kiti cha enzi ni imara tangu awali;*
wewe umekuwapo kabla ya kuwako nyakati.
Ee Mungu, vilima vyapaaza sauti zao;*
naam, vyapaaza sauti na mvumo wao.
Mungu ana enzi kuu juu mbinguni,/
ana nguvu kuliko mlio wa bahari,*
ana nguvu kuliko mawimbi ya maji.
Ee Mungu, maagizo yako ni thabiti;*.
nyumba yako ni takatifu milele na milele.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. I: Bwana ni mfalme, amefunikwa enzi, aleluya.
ANT. II: Viumbe vyote vitafanywa huru, na vitafurahia utukufu na
uhuru wa watoto wa Mungu, aleluya.
WIMBO: Dan.3:37-88,56 Kila kiumbe kimsifu Bwana
Msifuni Mungu, enyi watumishi wake wote (Ufu.19:5)
Enyi viumbe vyote vya Bwana, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Malaika za Bwana, mhimidini Bwana;*
Enyi mbingu, mhimidini Bwana.
Maji yote yaliyo juu angani, mhimidini Bwana;*
Mawezo yote ya Bwana, mhimidini Bwana.
Jua na mwezi, mhimidini Bwana;*
Nyota za mbinguni, mhimidini Bwana.
Manyunyu yote na ukungu, mhimidini Bwana;*
Pepo zote, mhimidini Bwana.
Moto na hari, mhimidini Bwana;*
Kipupwe na musimu, mhimidini Bwana.
Umande na sakitu, mhimidini Bwana;*
Jalidi na baridi, mhimidini Bwana.
Barafu na theluji, mhimidini Bwana;*
Usiku na mchana, mhimidini Bwana.
Dunia na imhimidi Bwana;*
Imsifu na kumwadhimisha milele.
Milima na vilima, mhimidini Bwana;*
Mimea yote ya nchi, mhimidini Bwana.
Chemchemi, mhimidini Bwana;*
Bahari na mito, mhimidini Bwana.
Nyangumi na vyote viendavyo majini, mhimidini Bwana;*
Ndege zote za angani, mhimidini Bwana.
Hayawani na wanyama wafugwao, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Wanadamu, mhimidini Bwana;*
Bani Israeli, mhimidini Bwana.
Makuhani wa Bwana, mhimidini Bwana;*
Watumishi wa Bwana, mhimidini Bwana.
Roho na nafsi zao wenye haki, mhimidini Bwana;*
Watakatifu na wanyenyekevu moyoni, mhimidini Bwana.
Enyi Anania, Azaria, na Misaeli, mhimidini Bwana;*
Msifuni na kumwadhimisha milele.
Tumtukuze Baba, Mwana, na Roho Mtakatifu;*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
Umehimidiwa katika anga la mbinguni,*
Wastahili kusifiwa na kutukuzwa milele.
ANT. II: Viumbe vyote vitafanywa huru, na vitafurahia utukufu na
uhuru wa watoto wa Mungu, aleluya.
ANT. III: Jina la Bwana lasifiwa, mbinguni na duniani, aleluya.
Zab.148 Ulimwengu wote umsifu Mungu
Kwake yeye aketiye katika kiti cha enzi, na kwa Mwana-kondoo, iwe sifa na heshima na
utukufu na enzi milele (Ufu.5:13)
Msifuni Mungu kutoka mbinguni,*
msifuni enyi mnaoishi huko juu.
Msifuni enyi malaika wake wote,*
msifuni enyi jeshi lote la mbinguni.
Msifuni enyi jua na mwezi,*
msifuni enyi nyota zote zing'aazo.
Msifuni enyi mbingu za juu,*
na maji yaliyo juu ya mbingu.
Lazima kulisifu jina la Mungu,*
maana yeye aliamuru, na vyote vikawa.
Yeye aliviweka mahali pao daima;*
amri yake yadumu milele.
Msifuni Mungu kutoka duniani;*
vilindi vya bahari na majoka yake, msifuni.
Msifuni enyi moto, mvua ya mawe na theluji,*
upepo wa tufani unaotimiza amri yake.
Msifuni enyi milima na vilima,*
miti ya matunda na misitu!
Msifuni enyi wanyama wa porini na wafugwao,*
wanyama watambaao na ndege wote!
Msifuni enyi wafalme wote na mataifa*
viongozi na watawala wote duniani!
Msifuni enyi wavulana na wasichana;*
wazee wote pamoja na watoto pia!
Nyote lisifuni jina la Mungu,/
maana jina lake peke yake latukuka;*
utukufu wake wapita dunia na mbingu.
Taifa la Israeli liko karibu naye;/
yeye amelikuza na kulipatia nguvu,*
hivyo watu wake wote waaminifu wanamsifu.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. III: Jina la Bwana lasifiwa, mbinguni na duniani, aleluya.
SOMO: Mate.10:40-43
Mungu alimfufua siku ya tatu, akamfanya aonekane si kwa watu wote, ila kwa wale Mungu aliokwisha
wachagua wawe mashahidi wake, yaani sisi tuliokula na kunywa pamoja naye baada ya kufufuka kwake
katika wafu. Alituamuru kuihubiri Habari Njema kwa watu wote, na kushuhudia kwamba yeye ndiye
aliyeteuliwa na Mungu awe Mwamuzi wa Wazima na wafu. Manabii wote waliongea juu yake Kwamba kila
mtu atakayemwamini atasamehewa dhambi zake zote kwa jina lake.
KIITIKIZANO
K. Utuhurumie, Kristo, Mwana wa Mungu aliye hai, aleluya, aleluya. (W. Warudie)
K. Umefufuka kutoka wafu.
W. Aleluya, aleluya.
K. Atukuzwe Baba na Mwana na Roho Mtakatifu.
W. Utuhurumie...
Ant. Wimbo wa Zakaria
Ilimpasa Kristo ateswe, na siku ya tatu afufuke kutoka wafu, aleluya.
WIMBO WA ZAKARIA
Lk.1:68-79 Masiha na mtangulizi wake
Asifiwe Bwana Mungu wa Israeli,/
kwani amekuja kuwasaidia*
na kuwakomboa watu wake.
Ametupatia Mwokozi shujaa,*
mzao wa Daudi, mtumishi wake.
Aliahidi hapo kale*
kwa njia ya manabii wake watakatifu,
kwamba atatuokoa kutoka maadui wetu*
na kutoka mikono ya wote wanaotuchukia.
Alisema kwamba atawaonea huruma wazee wetu,*
na kukumbuka agano lake takatifu.
Kwa kiapo alichomwapia mzee wetu Abrahamu/
aliahidi kutukomboa kutoka maadui wetu*
na kutujalia tumtumikie bila hofu,
ili tuwe watakatifu na waadilifu mbele yake*
siku zote za maisha yetu.
Nawe, mwanangu, utaitwa:*
nabii wa Mungu Aliye Juu,
utamtangulia Bwana*
kumtayarishia njia yake;
kuwatangazia watu kwamba wataokolewa*
kwa kuondolewa dhambi zao.
Mungu wetu ni mpole na mwenye huruma,/
atasababisha pambazuko angavu la ukombozi*
litujie kutoka juu,
na kuwaangazia wote wanaokaa/
katika giza kuu la kifo,*
aongoze hatua zetu katika njia ya amani.
Atukuzwe Baba na Mwana*
na Roho Mtakatifu.
Kama mwanzo na sasa na siku zote*
na milele. Amina
Ant. Ilimpasa Kristo ateswe, na siku ya tatu afufuke kutoka wafu, aleluya.
MAOMBI
Tumwombe Kristo, aliye chanzo cha uzima. Mungu alimfufua kutoka wafu, na yeye mwenyewe atatufufua
sisi kwa uwezo wake mwenyewe.
W. Kristo, uzima wetu, utuokoe.
Kristo, wewe ndiwe nuru inayoondoa giza na kuwaingiza watu kwenye utakatifu;
- utuwezeshe kukusifu siku hii ya leo kwa matendo yetu. (W.)
Bwana, ulikwenda njia ya mateso hadi msalabani;
- utujalie tuweze kufa pamoja nawe, na kufufuka nawe. (W.)
Bwana wetu na ndugu yetu, umetufanya tuwe ufalme wa makasisi, tupate kumtumikia Mungu Baba yetu;
- utuwezeshe kukutolea kwa furaha sadaka ya sifa. (W.)
Mfalme wa utukufu, tunaitazamia siku ya ujio wako;
- ndipo tutakapouona uso wako, na kushiriki utukufu wako. (W.)
Sala ya Baba yetu:
K. Na sasa tusali kwa maneno yale aliyotufundisha Mwokozi wetu:
Baba Yetu...
Baba Yetu, uliye mbinguni,
jina lako litukuzwe.
Ufalme wako ufike.
Utakalo lifanyike, duniani kama mbinguni.
Utupe leo mkate wetu wa kila siku;
utusamehe makosa yetu,
kama tunavyowasamehe na sisi waliotukosea,
usitutie katika kishawishi,
lakini utuopoe maovuni. Amina.
SALA:
Bwana Mungu, uwajalie watu wako furaha ya daima Kwa kutiwa nguvu mpya rohoni mwao. Wanafurahi
kwa sababu umewarudishia utukufu wa kufanywa Watoto wako: uwafanye waungojee kwa furaha na matumaini
ufufuko ambao hakika wataupata. Tunaomba hayo kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo, Mwanao,
anayeishi na kutawala nawe na Roho Mtakatifu, Mungu, daima na milele.
W. Amina.
K. Bwana atubariki, atukinge na maovu yote, na atufikishe kwenye uzima wa milele.
(W.) Amina.