DOMINIKA YA 3 MAJILIO

MASOMO MWAKA A

ANTIFONA YA KUINGIA: Flp.4:4-5
Furahini katika Bwana sikuzote; tena nasema furahini. Bwana yu karibu.

KOLEKTA
Ee Mungu, unatuona sisi taifa lako tukiingojea Kiaminifu sherehe ya kuzaliwa kwake Bwana wetu. Tunakuomba utujalie tuweze kuzifikia furaha za wokovu huo mkubwa sana, na kuziadhimisha daima kwa ibada kuu na shangwe. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Isa.35:1-6,10
Nyika na mahali palipo ukiwa patafurahi; jangwa litashangilia na kuchanua maua kama waridi. Litachanua maua mengi, na kufurahi, naam, kwa shangwe na kuimba; litapewa uzuri wa Lebanoni, utukufu wa Karmeli na Sharoni; watauona utukufu wa Bwana, ukuu wa Mungu wetu. Itieni nguvu mikono iliyo dhaifu, yafanyeni imara magoti yaliyolegea. Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo msiogope; tazama, Mungu wenu atakuja na kisasi, na malipo ya Mungu; atakuja na kuwaokoa ninyi. Ndipo macho ya vipofu yatafumbuliwa, na masikio ya viziwi yatazibuliwa. Ndipo mtu aliye kilema atarukaruka kama kulungu, na ulimi wake aliye bubu utaimba. Na hao waliokombolewa na Bwana watarudi, watafika Sayuni wakiimba; na furaha ya milele itakuwa juu ya vichwa vyao; nao watapata kicheko na furaha, huzuni na kuugua zitakimbia.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.146:6-10 (K) Isa.35:4
1. Huishika kweli milele.
Huwafanyia hukumu walioonewa,
Huwapa wenye njaa chakula;
Bwana hufungua waliofungwa;

(K) Uje Bwana kutuokoa.
Au:
Aleluya!

2. Bwana huwafumbua macho waliopofuka;
Bwana huwainua walioinama;
Bwana huwapenda wenye haki;
Bwana huwahifadhi wageni. (K)

3. Huwategemeza yatima na mjane;
Bali njia ya wasio haki huipotosha.
Bwana atamiliki milele,
Mungu wako, Ee Sayuni, kizazi hata kizazi. (K)

SOMO 2: Yak.5:7-10
Ndugu, vumilieni, hata kuja kwake Bwana. Tazama, mkulima hungoja mazao ya nchi yaliyo ya thamani, huvumilia kwa ajili yake hata yatakapopata mvua ya kwanza na ya mwisho. Nanyi vumilieni mthibitishe mioyo yenu, kwa maana kuja kwake Bwana kunakaribia. Ndugu, msinung'unikiane, msije mkahukumiwa. Angalieni, mwamuzi amesimama mbele ya milango. Ndugu, watwaeni manabii walionena kwa jina la Bwana, wawe mfano wa kustahimili mabaya, na wa uvumilivu.

SHANGILIO: Lk.4:18
Aleluya, aleluya!
Roho wa Bwana yu juu yangu,
Amenituma kuwahubiri maskini habari njema;
Aleluya!

SOMO 3: INJILI: Mt.11:2-11
Siku ile, Yohane aliposikia huko gerezani matendo yake Kristo, alituma wanafunzi wake, kumwuliza, Wewe ndiwe yule ajaye, au tumtazamie mwingine' Yesu akajibu akawaambia, Nendeni mkamweleze Yohane mnayoyasikia na kuyaona; vipofu wanapata kuona, viwete wanakwenda, wenye ukoma wanatakaswa, viziwi wanasikia, wafu wanafufuliwa, na maskini wanahubiriwa habari njema. Naye heri awaye yote asiyechukizwa nami. Na hao walipokwenda zao, Yesu alianza kuwaambia makutano habari za Yohane, Mlitoka kwenda nyikani kutazama nini? Unyasi ukitikiswa na upepo? Lakini mlitoka kwenda kuona nini? Mtu aliyevikwa mavazi mororo? Tazama, watu wavaao mavazi mororo wamo katika nyumba za wafalme. Lakini kwa nini mlitoka? Ni kuona Nabii? Naam, nawaambia, na aliye mkuu zaidi ya Nabii. Huyo ndiye aliyeandikiwa haya, Tazama, mimi namtuma mjumbe wangu mbele ya uso wako, atakayeitengeneza njia yako mbele yako. Amin, nawaambieni, Hajaondokea mtu katika wazao wa wanawake aliye mkuu kuliko Yohane Mbatizaji; walakini aliye mdogo katika ufalme wa mbinguni ni mkuu kuliko yеyе.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Yesu alimsifu Yohane Mbatizaji kama mtu asiyepeperushwa kwa mikondo mbalimbali ya hewa, maana yake Yohane alikuwa na msimamo wa kutimiza ujumbe kwa uaminifu kabisa. Ee Baba Mwenyezi,

1. Utuimarishe tusiyumbishwe na madhehebu yanayojitokeza siku hizi kama uyoga, bali tumfuate Yesu na Enjili yake kwa msimamo thabiti.

2. Utupe nguvu ya kushika imani inayotuhakikishia njia ya wokovu, ndiye Yesu Kristo, Bwana wetu.

3. Utusaidie kuwaonesha wenzetu njia ya wokovu kwa kuwasaidia katika taabu za mwili na shida za roho.

4. Utuangaze katika mashaka kuhusu imani yetu na kuhusu mwenendo wetu wa maadili.

5. Uwaongoze raia nchini mwetu wawachague wajumbe wabunge bora watakaotunga sheria zinazozingatia haki na amani.

Ee Baba mwema, upokee maombi yetu kwa jina la Kristo Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, tunakuomba sadaka ya ibada yetu itolewe kwako daima. Nayo itimize agizo la kuadhimisha fumbo takatifu, na kutenda kwa mafanikio wokovu wako ndani yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

1. UTANGULIZI WA MAJILIO:
MAJILIO I:

K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W. Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.

K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, tukushukuru Wewe daima na popote, ee Bwana, Baba uliye mtakatifu, Mungu mwenyezi wa milele, kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
Yeye, katika ujio wake wa kwanza, alipokuja katika unyenyekevu wa mwili, aliutimiza mpango ulioandaliwa nawe tangu kale. Hivyo, akatufungulia njia ya wokovu wa milele, ili, atakapokuja tena katika utukufu wa enzi yake, hatimaye tupewe waziwazi mema yaliyoahidiwa, ambayo kwa sasa tunathubutu kuyatarajia, tukikesha.
Kwa sababu hiyo, sisi pamoja na Malaika na Malaika Wakuu, pamoja na Viti vya enzi na Milki, na majeshi yote ya Malaika wa mbinguni, twaimba utenzi wa utukufu wako, tukisema bila mwisho:

W. Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu,
Bwana Mungu wa majeshi.
Mbingu na dunia zimejaa utukufu wako.
Hosana juu mbinguni.
Mbarikiwa ajaye kwa jina la Bwana.
Hosana juu mbinguni.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Isa.35:4
Waambieni walio na moyo wa hofu, Jipeni moyo, msiogope; tazama, Mungu wetu atakuja na kutuokoa.

SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Bwana, tunakuomba utujalie huruma yako, ili misaada hii ya kimungu ituondolee dhambi zetu, na kutuweka tayari kwa sikukuu zijazo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.