DOMINIKA YA 3 KWARESIMA MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.25:15-16
Macho yangu humwelekea Bwana daima, naye atanitoa miguu yangu katika wavu. Uniangalie na
kunifadhili, maana mimi ni mkiwa na mteswa.
AU: Eze.36:23-26
Nitakapotakaswa kati yenu nitawakusanya na kuwatoa katika nchi zote; nitawanyunyizia maji safi,
nanyi mtatakasika na uchafu wenu wote. Nami nitawapa ninyi roho mpya, asema Bwana.
KOLEKTA:
Ee Mungu, uliye asili ya rehema zote na mema yote, ulionesha kuwa dawa ya dhambi ni kufunga, kusali
na kutoa sadaka. Uwe radhi kutazama ungamo hili la unyonge wetu, ili, maadamu tunanyenyekeshwa na
dhamiri zetu, tuinuliwe daima na rehema yako. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi
na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Kut.3:1-8a 13-15
Musa alikuwa akilichunga kundi la Yethro mkwewe, kuhani wa Midiani; akaliongoza kundi nyuma ya
jangwa, akafika mpaka mlima wa Mungu, hata Horebu. Malaika wa Bwana akamtokea, katika mwali wa moto
uliotoka katikati ya kijiti; akatazama, na kumbe! kile kijiti kiliwaka moto, nacho kijiti hakikuteketea.
Musa akasema, Nitageuka sasa, niyaone maono haya makubwa, na sababu kijiti hiki hakiteketei. Bwana
alipoona ya kuwa amegeuka ili atazame, Mungu akamwita kutoka katikati ya kile kijiti, akasema, Musa!
Musa! Akasema, Mimi hapa. Naye akasema, Usikaribie hapa; vua viatu vyako miguuni mwako; maana mahali
hapo unaposimama ni nchi takatifu. Tena akasema, Mimi ni Mungu wa baba yako, Mungu wa Ibrahimu, Mungu
wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Musa akaficha uso wake; kwa maana aliogopa kumwangalia Mungu. Bwana akasema,
Hakika nimeyaona mateso ya watu wangu walioko Misri, nami nimekisikia kilio chao kwa sababu ya wasimamizi
wao; maana nayajua maumivu yao; nami nimeshuka ili niwaokoe na mikono ya Wamisri, niwapandishe kutoka
nchi ile, hata nchi njema, kisha pana; nchi ijaayo maziwa na asali. Musa akamwambia Mungu, Tazama, nitakapofika
kwa wana wa Israeli, na kuwaambia, Mungu wa baba zenu amenituma kwenu; nao wakaniuliza, jina lake ni nani?
Niwaambie nini? Mungu akamwambia Musa, Mimi niko ambaye niko; akasema, Ndivyo utakavyowaambia wana wa Israeli:
Mimi niko amenituma kwenu. Tena Mungu akamwambia Musa, Waambie wana wa Israeli maneno haya, Bwana, Mungu wa
baba zenu, Mungu wa Ibrahimu, Mungu wa Isaka, Mungu wa Yakobo, amenituma kwenu; hili ndilo jina langu hata
milele, nalo ni kumbukumbu langu hata vizazi vyote.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.103:1-4,6-8,11 (K)8
1. Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana.
Naam, vyote vilivyo ndani yangu
Vilihimnidi jina lake takatifu.
Ee nafsi yangu, umhimidi Bwana,
Wala usizisahau fadhili zake zote.
(K) Bwana amejaa huruma na neema.
2. Akusamehe maovu yako yote,
Akuponya magonjwa yako yote,
Aukomboa uhai wako na kaburi,
Akutia taji ya fadhili na rehema. (K)
3. Bwana ndiye afanyaye mambo ya haki,
Na hukumu kwa wote wanaoonewa.
Alimjulisha Musa njia zake,
Wana wa Israeli matendo yake. (K)
4. Bwana amejaa huruma na neema,
Haoni hasira upesi, ni mwingi wa fadhili.
Maana mbingu zilivyoinuka juu ya nchi,
Kadiri ileile rehema zake ni kuu kwa wamchao. (K)
SOMO 2: 1Kor.10:1-6,10-12
Ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita
kati ya bahari; wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari; wote wakala chakula
kilekile cha roho; wote wakanywa kinywaji kilekile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho
uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo. Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa
nao; maana waliangamizwa jangwani. Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu
wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani. Wala msinung'unike, kama wengine wao walivyonung'unika,
wakaharibiwa na mharabu. Basi mambo hayo yaliwapata wao kwa jinsi ya mifano, yakaandikwa ili kutuonya
sisi, tuliofikiliwa na miisho ya zamani. Kwa hiyo anayejidhania kuwa amesimama na aangalie asianguke.
SHANGILIO: Zab.95:7-8
Msifanye migumu mioyo yenu;
Lakini msikie sauti yake.
INJILI: Lk.13:1-9
Wakati ule walikuwapo watu waliompasha Yesu habari ya Wagalilaya wale ambao Pilato alichanganya
damu yao na dhabihu zao. Akawajibu akawaambia, Je, mwadhani ya kwamba Wagalilaya hao walikuwa wenye
dhambi kuliko Wagalilaya wote, hata wakapatwa na mambo hayo? Nawaambia, sivyo; lakini msipotubu,
ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Au wale kumi na wanane, walioangukiwa na mnara huko Siloamu,
ukawaua, mwadhani ya kwamba wao walikuwa wakosaji kuliko watu wote waliokaa Yerusalemu? Nawaambia,
Sivyo; lakini msipotubu, ninyi nyote mtaangamia vivyo hivyo. Akanena mfano huu; Mtu mmoja alikuwa na
mtini umepandwa katika shamba lake la mizabibu; akaenda akitafuta matunda juu yake, asipate. Akamwambia
mtunzaji wa shamba la mizabibu, Tazama, miaka mitatu hii naja nikitafuta matunda juu ya mtini huu,
nisipate kitu; uukate, mbona hata nchi unaiharibu? Akajibu akamwambia, Bwana, uuache mwaka huu nao,
hata niupalilie, niutilie samadi; nao ukizaa matunda baadaye, vema! La,usipozaa, ndipo uukate.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Ndugu zangu, Watu hufikiri kwamba shida ya ghafla au balaa ni adhabu ya Mungu mwenye nia ya kuwaadhibu kwa
sababu ya dhambi zao. Lakini Yesu alisema kwamba watu wote ni wakosefu mbele ya Mungu wanaohitaji toba na
hivyo kumwongokea Mungu.
Tuombe,
1. Ee Bwana Mungu wetu, utusaidie kusikia mwito wa kutubu na kujitahidi kujisahihisha katika makosa yetu.
2. Ujifunue kwa wote walio na shida ya kukutambua katika mahangaiko ya maisha yao.
3. Utupe neema ya kutambua kwamba tumekukosea na utujalie nguvu ya kurudi kwako na kuacha njia ya dhambi zetu.
4. Ulainishe mioyo ya watu wakaidi na wokorofi wanaodhani kwamba hawahitaji kutubu ili kuanza maisha mapya
kwa neema yako.
5. Utusaidie kwa nguvu yako kuacha njia zetu zinazopingana na amri zako.
6. Uburudishe mioyo yetu kwa neema yako ili tufurahie furaha ya kuongozwa nawe.
Ee Mungu Baba, Mwana wako alitufungulia mlango wa wokovu. Utusaidie kusikia sauti yake na kumfuata, Yeye
anayeishi na kutawala pamoja nawe na Roho Mtakatifu, daima na melele. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, ukiisha kutulizwa na dhabihu hii, utujalie ili, maadamu tunakuomba kusamehewa
dhambi zetu wenyewe, tufanye bidii kuwasamehe ndugu zetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.84:3-4
Shomoro naye ameona nyumba, na mbayuwayu amejipatia kioto, alipoweka makinda yake, kwenye
madhabahu zako, ee Bwana wa majeshi, Mfalme wangu na Mungu wangu. Heri wakaao nyumbani
mwako, wanakuhimidi daima.
SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana tumepokea amana ya siri ya kimungu na kushibishwa kwa mkate wa mbinguni tungali bado
hapa duniani. Tunakuomba kwa unyenyekevu ili yaliyotendwa ndani yetu na sakramenti hii yatimizwe
kwa matendo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
SALA YA KUWAOMBEA WAAMINI:
Ee Bwana, tunakuomba, ongoza nyoyo za waamini wako, na uwe radhi kuwajalia watumishi wako neema
hii, kwamba, kwa kudumu katika kukupenda wewe na majirani, waweze kutimiza utimilifu wa amri zako.
Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.