DOMINIKA YA 33 MWAKA C
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Yer.29:11,12,14
Bwana asema: Mawazo ninayowawazia ninyi ni mawazo ya amani wala si ya mabaya. Nanyi mtaniita nami nitawasikiliza, nami nitawarudisha kutoka mahali pote watu wenu waliofungwa.

Utukufu husemwa

KOLEKTA:
Ee Bwana Mungu wetu, tunakuomba utujalie tufurahi daima katika kukutumikia, maana kama tukikutumikia wewe uliye muumba wa mema yote, tunayo heri iliyo kamili siku zote. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: Mal.4:1-2
Angalieni, siku ile inakuja, inawaka kama tanuru, na watu wote wenye kiburi, nao wote watendao uovu, watakuwa makapi; na siku ile inayokuja itawateketeza, asema Bwana wa majeshi; hata haitawaachia shina wala tawi. Lakini kwenu ninyi mnaolicha jina langu, jua la haki litawazukia, lenye kuponya katika mbawa zake.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.98:5-9 (K)9
1. Mwimbieni Bwana zaburi kwa kinubi,
Kwa kinubi na sauti ya zaburi.
Kwa panda na sauti ya baragumu,
Shangilieni mbele za Mfalme, Bwana.

(K) Bwana anakuja awahukumu mataifa kwa haki.

2. Bahari na ivume na vyote viijazavyo,
Ulimwengu, nao wanaokaa ndani yake.
Mito na ipige makofi,
Milima na iimbe kwa furaha mbele za Bwana. (K)

3. Kwa maana Bwana, anakuja aihukumu nchi,
Atauhukumu ulimwengu kwa haki,
Na mataifa kwa adili. (K)

SOMO 2: 2The.3:7-12
Ndugu zangu, mwajua wenyewe jinsi iwapasavyo kutufuata; kwa sababu hatukuenda bila utaratibu kwenu; wala hatukula chakula kwa mtu yeyote bure; bali kwa taabu na masumbufu, usiku na mchana tulitenda kazi, ili tusimlemee mtu wa kwenu awaye yote. Si kwamba hatuna amri, lakini makusudi tufanye nafsi zetu kuwa kielelezo kwenu, mtufuate. Kwa kuwa hata wakati ule tulipokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula. Maana twasikia kwamba wako watu kwenu waendao bila utaratibu, hawana shughuli zao wenyewe, lakini wanajishughulisha na mambo ya wengine. Basi twawaagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivu na kula chakula chao wenyewe.

SHANGILIO: Lk.21:36
Aleluya, aleluya!
Kesheni ninyi kila wakati, mkiomba,
ili mpate kusimama mbele za Mwana wa Adamu.
Aleluya!

INJILI: Lk.21:5-19
Wakati ule, watu kadha wa kadha walipokuwa wakiongea habari za hekalu, jinsi lilivyopambwa kwa mawe mazuri na sadaka za watu, Yesu alisema, Haya mnayoyatazama, siku zitakuja ambapo halitasalia jiwe juu ya jiwe ambalo halitabomoshwa. Wakamwuliza wakisema, Mwalimu, mambo hayo yatakuwa lini? Nayo ni nini ishara ya kuwa mambo hayo ya karibu kutukia? Akasema, Angalieni, msije mkadanganyika, kwa sababu wengi watakuja kwa jina langu, wakisema, Mimi ndiye; tena, Majira yamekaribia. Basi msiwafuate hao. Nanyi mtakaposikia habari za vita na fitina, msitishwe; maana, hayo hayana budi kutukia kwanza, lakini ule mwisho hauji upesi. Kisha aliwaambia, Taifa litaondoka kupigana na taifa, na ufalme kupigana na ufalme; kutakuwa na matetemeko makubwa ya nchi; na njaa na tauni mahali mahali; na mambo ya kutisha na ishara kuu kutoka mbinguni. Lakini, kabla hayo yote hayajatokea, watawakamata na kuwaudhi; watawapeleka mbele ya masinagogi na kuwatia magerezani, mkipelekwa mbele ya wafalme na maliwali kwa ajili ya jina langu. Na hayo yatakuwa ushuhuda kwenu. Basi, kusudieni mioyoni mwenu, kutofikirifikiri kwanza mtakavyojibu; kwa sababu mimi nitawapa kinywa na hekima ambayo watesi wenu wote hawataweza kushindana nayo wala kuipinga. Nanyi mtasalitiwa na wazazi wenu, na ndugu zenu, na jamaa zenu, na rafiki zenu, nao watawafisha baadhi yenu. Nanyi mtachukiwa na watu wote kwa ajili ya jina langu. Walakini hautapotea hata unywele mmoja wa vichwa vyenu. Nanyi kwa subira yenu mtaziponya nafsi zenu.

Nasadiki husemwa.

Ndugu wapenzi, Kabla ya mwisho wa dunia na historia yake yatatokea mambo mengi ya kutisha. Mengi ni ya kutudanganya na kutushawishi tumwache Mungu na kuwasikiliza "wakombozi wa uwongo". Tumuombe Mungu atusaidie tusinaswe kwa mitego ya ahadi za uwongo. Ee Mungu Baba Muumbaji wa vyote,

1. Mwanao alileta wokovu duniani, lakini wengi hawakuujali bali walibaki katika hali ya ubaya wao: Utusaidie tusinaswe na kushindwa katika hila za shetani.

2. Utuimarishe kwa nguvu ya Roho wako Mtakatifu ili tuyashinde magumu tutakayokumbana nayo katika imani yetu.

3. Utupe moyo wa kutokubali kushindwa kwa ubaya bali tuushinde ubaya kwa wema.

4. Katika maisha yetu tunagundua na tunavumilia madhulumu na mateso: Utushike mikono yetu ili tusikate tamaa ya kupata ushindi katika wewe.

5. Utusindikize katika safari yetu ya kuja kwako tuvuke mabonde ya magumu na vikwazo kwa usalama ili kufika mbinguni.

Ee Mungu wa milele, ulitujalia imani ituimarishe katika misukosuko ya dunia. Uyasikilize maombi yetu, na utuongoze tushike kwa uthabiti maneno ya Mwana wako, Yesu Kristo, Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba utujalie ili vipaji tulivyotoa mbele ya macho yako wewe uliye mtukufu, vitupatie neema ya kukutumikia kwa uchaji na tunda la heri ya milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.73:28
Nami kumkaribia Mungu ni kwema kwangu; nimefanya kimbilio kwa Bwana Mungu.

Au:
Mk.11:23-24

Bwana asema: Amin, nawaambia, yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tumepokea mapaji ya fumbo hili takatifu. Tunakusihi kwa unyenyekevu, ili, yale ambayo Mwanao alituagiza kwa ukumbusho wake, yatufae kwa kutuongezea mapendo yetu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.