DOMINIKA YA 32 YA MWAKA C
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.88:2
Maombi yangu yafike mbele zako, uutegee ukelele wangu sikio lako, ee Bwana.

UTUKUFU husemwa.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi na rahimu, utuepushe kwa radhi yako na yote yawezayo kutudhuru, ili, tukiwa huru rohoni na mwilini, tupate kuyatimiza mapenzi yako pasipo kizuio. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, Mungu, milele na milele.

SOMO 1: 2Mak.7:1-2,9-14
Ilitokea ya kuwa ndugu saba, pamoja na mama yao, walikamatwa kwa amri ya mfalme na kuteswa sana kwa mijeledi na mapigo ili kuwashurutisha kuonja nyama marufuku ya nguruwe. Mmoja akajifanya mnenaji wao, akasema, Wataka kuuliza nini na kujua nini juu yetu? Sisi tu tayari kufa kuliko kuzivunja amri za wazee wetu. Naye [wa pili] alipokuwa kufani alisema, Wewe, mdhalimu, unatufarikisha na maisha ya sasa, lakini Mungu wa ulimwengu atatufufua sisi tuliokufa kwa ajili ya amri zake, hata tupate uzima wa milele. Na baada yake alidhihakiwa yule wa tatu. Naye mara alipoagizwa, alitoa ulimi wake, akanyosha mikono yake bila hofu, akasema kwa ushujaa, Kutoka mbinguni nalipewa hivi, na kwa ajili ya amri za Mungu navihesabu kuwa si kitu, na kwake natumaini kuvipokea tena. Hata mfalme na watu wake walishangazwa kwa roho ya kijana huyu, kwa jinsi alivyoyadharau maumivu yake. Akiisha kufa huyu, walimtesa wa nne na kumtendea mabaya yaleyale. Naye alipokaribia kufa alisema hivi: Ni vema kufa kwa mikono ya wanadamu na kuzitazamia ahadi zitokazo kwa Mungu, kuwa tutafufuliwa naye. Lakini kwako wewe hakuna ufufuo.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.17:1,5-6,8,15,(K)15
1. Ee Bwana, usikie haki, usikilize kilio changu,
Utege sikio lako kwa maombi yangu,
Yasiyotoka katika midomo ya hila.

(K) Ee, Bwana niamkapo
nitashibishwa kwa sura yako.

2. Nyayo zangu zimeshikamana na njia zako,
Hatua zangu hazikuondoshwa.
Ee Mungu, nimekuita kwa maana utaitika,
Utege sikio lako ulisikie neno langu. (K)

3. Unilinde kama mboni ya jicho,
Unifiche chini ya uvuli wa mbawa zako;
Nami nikutazame uso wako katika haki,
Niamkapo nishibishwe kwa sura yako. (K)

SOMO 2: 2The.2:16-3:1-5
Ndugu zangu, Bwana wetu Yesu Kristo mwenyewe, na Mungu Baba yetu, aliyetupenda akatupa faraja ya milele na tumaini jema, katika neema, awafariji mioyo yenu, na kuwafanya imara katika kila neno na tendo jema. Hatimaye, ndugu, tuombeeni, neno la Bwana liendelee, na kutukuzwa vilevile kama ilivyo kwenu; tukaokolewe na watu wasio haki, wabaya; maana si wote walio na imani. Lakini Bwana ni mwaminifu, atakayewafanya imara na kuwalinda na yule mwovu. Nasi tumemtumaini Bwana kwa mambo yenu, kwamba mnayafanya tuliyowaagiza, tena kwamba mtayafanya. Bwana awaongoze mioyo yenu mkapate pendo la Mungu, na saburi ya Kristo.

SHANGILIO: Yn.1:12,14
Aleluya, aleluya!
Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu;
wote waliompokea
aliwapa uwezo wa kufanyika watoto wa Mungu.
Aleluya!

INJILI: Lk.20:27-38
Baadhi ya Masadukayo, wale wasemao ya kwamba hakuna ufufuo, walimwendea Yesu, wakamwuliza, wakisema, Mwalimu, Musa alituandikia ya kuwa, mtu akifiwa na ndugu yake mwenye mke, lakini hana mtoto, na amtwae huyu mke, ampatie ndugu yake mzao. Basi, kulikuwa na ndugu saba. Wa kwanza alioa mke, akafa hana mtoto; na wa pili akamtwaa yule mke, akafa hana mtoto; hata wa tatu akamwoa, na kadhalika wote saba, wakafa, wasiache watoto. Mwisho akafa yule mke naye. Basi, katika ufufuo atakuwa mke wa yupi? Maana aliolewa na wote saba. Yesu akawaambia, Wana wa ulimwengu huu huoa na kuolewa; lakini, wale wahesabiwao kuwa wamestahili kuupata ulimwengu ule, na kule kufufuka katika wafu, hawaoi wala hawaolewi, wala hawawezi kufa tena; kwa sababu huwa sawasawa na malaika, nao ni wana wa Mungu, kwa vile walivyo wana wa ufufuo. Lakini, ya kuwa wafu hufufuliwa, hata na Musa alionyesha katika sura ya Kijiti, hapo alipomtaja Bwana kuwa ni Mungu wa Ibrahimu na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo. Naye si Mungu wa wafu, bali wa walio hai; kwa kuwa wote huishi kwake.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Ndugu wapendwa, Masadukayo wasioamini habari ya ufufuko wa wafu walitaka kuhadaa habari hii ya ufufuko kwa hadithi ya wanaume saba watakaompigania mwanamke mmoja huko mbinguni. Yesu alirekebisha mawazo yao ya uwongo.

Ee Bwana Mungu,
1. Uamshe ndani yetu furaha ya kushirikishwa uzima wa milele katika ulimwengu ujao.

2. Utusaidie kufuata nyayo za mwanao Yesu Kristo zinazotuonesha njia ya kukaribishwa mbinguni.

3. Utusaidie tusisahau ahadi za mbinguni katika mapambano ya maisha yetu ya kila siku hapa duniani.

4. Kwa kufa na kufufuka mwanao ulitupatia mwanzo wa uzima wa milele; uimarishe matumaini yetu tusipoteze amana ya uzima huo.

5. Ujaze mioyo yetu furaha ya kuvikwa utukufu wa mbinguni pamoja na ndugu, jamaa na marafiki zetu marehemu waliotutangulia.

Ee Mungu wa uzima, unaishi tangu milele na uzima wako hauna mwisho. Tunatoka kwako kwa kuumbwa na kwako tutarudi. Uyasikilize maombi yetu, kwa Kristo Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunakuomba uwe radhi kuitazama dhabihu hii tunayokutolea, ili, lile tunaloadhimisha katika fumbo la mateso ya Mwanao, tulipokee kwa upendo na uchaji. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.23:1-2
Bwana ndiye mchungaji wangu, sitapungukiwa kitu. Katika malisho ya majani mabichi hunilaza, kando ya maji ya utulivu huniongoza.

Au:
Lk.24:35

Wafuasi walimtambua Bwana Yesu katika kuumega mkate.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, baada ya kulishwa kipaji kitakatifu, tunakutolea shukrani na kukuomba sana huruma yako. Na kwa kumiminiwa Roho wako Mtakatifu, wale ambao wamepokea nguvu ya mbinguni, wadumu katika neema ya uaminifu. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.