DOMINIKA YA 31 YA MWAKA C
MASOMO

ANTIFONA YA KUINGIA: Zab.38:21-22
Wewe, Bwana, usiniache; Mungu wangu, usijitenge nami. Ufanye haraka kunisaidia, ee Bwana, nguvu za wokovu wangu.

UTUKUFU husemwa.

KOLEKTA:
Ee Mungu mwenyezi na rahimu, kwa neema yako waamini huweza kukutumikia kwa namna inayofaa na ya kusifika. Tunakuomba utujalie tuweze kuzikimbilia ahadi zako bila kujikwaa. Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, milele na milele.

SOMO 1: Hek.11:22-12:2
Ulimwengu wote mbele zako ni kama chembe moja katika mizani, na mfano wa tone moja la umande lishukalo asubuhi juu ya ardhi. Lakini Wewe unawahurumia watu wote, kwa sababu unao uweza wa kutenda mambo yote; nawe wawaachilia wanadamu dhambi zao, ili wapate kutubu. Kwa maana Wewe wavipenda vitu vyote vilivyopo, wala hukichukii kitu chochote ulichokiumba. Kwa kuwa hungalifanya kamwe kitu chochote kama ungalikichukia; tena kitu chochote kingaliwezaje kudumu, ila kwa mapenzi yako? Au kitu kisichoumbwa nawe kingaliwezaje kuhifadhika? Lakini Wewe unaviachilia vyote, kwa kuwa ni vyako, Ee Mfalme Mkuu, mpenda roho za watu; maana roho yako isiyoharibika imo katika vyote. Kwa hiyo wawathibitishia kidogo kidogo hatia yao, wale wanaokengeuka kutoka katika njia njema; wawaonya, ukiwakumbusha kwa mambo yale yale wanayokosa, ili waokoke katika ubaya wao, na kukuamini Wewe, Bwana.

WIMBO WA KATIKATI: Zab.145:1-2,8-11,13-14(K)1
1. Ee Mungu wangu, Mfalme, nitakutukuza,
Nitalihimidi jina lako milele na milele.
Kila siku nitakuhimidi,
Nitalisifu jina lako milele na milele.

(K) Ee Mungu Mfalme wangu,
Nitalitukuza jina lako milele.

2. Bwana ana fadhili, ni mwingi wa huruma,
Si mwepesi wa hasira, ni mwingi wa rehema,
Bwana ni mwema kwa watu wote,
Na rehema zake zi juu ya viumbe vyake vyote. (K)

3. Ee Bwana, viumbe vyako vyote vitakushukuru,
Na wacha Mungu wako watakuhimidi.
Wataunena utukufu wa ufalme wako.
Na kuuhadithia uweza wako. (K)

4. Ufalme wako ni ufalme wa zamani zote,
Na mamlaka yako ni ya vizazi vyote.
Bwana huwategemeza wote waangukao,
Huwainua wote walioinamia chini. (K)

SOMO 2: 2The.1:11-2:2/a>
Wapenzi, twawaombea ninyi sikuzote, ili Mungu wetu awahesabu kuwa mmekustahili kuitwa kwenu, akatimiza kila haja ya wema na kila kazi ya imani kwa nguvu; jina la Bwana wetu Yesu litukuzwe ndani yenu, nanyi ndani yake, kwa neema ya Mungu wetu na ya Bwana Yesu Kristo. Basi, ndugu, tunakusihini, kwa habari ya kuja kwake Bwana wetu Yesu Kristo, na kukusanyika kwetu mbele zake, kwamba msifadhaishwe upesi hata kuiacha nia yenu, wala msisitushwe kwa roho, wala kwa neno, wala kwa waraka unaodhaniwa kuwa ni wetu, kana kwamba siku ya Bwana imekwisha kuwapo.

SHANGILIO: Lk.21:36
Aleluya, aleluya!
Kesheni ninyi kila wakati, mkiomba,
ili mpate kusimama mbele za Mwana wa Adamu.
Aleluya!

INJILI: Lk.19:1-10
Yesu alipoingia Yeriko alipita katikati yake. Na tazama, palikuwa na mtu, jina lake Zakayo, mkubwa mmoja katika watoza ushuru, naye ni tajiri. Huyu alikuwa akitafuta kumwona Yesu ni mtu wa namna gani, asiweze kwa sababu ya umati wa watu, maana ni mfupi wa kimo. Akatangulia mbio, akapanda juu ya mkuyu apate kumwona, kwa kuwa atakuja kuipitia njia ile. Na Yesu, alipofika mahali pale, alitazama juu, akamwambia, Zakayo, shuka upesi, kwa kuwa leo imenipasa kushinda nyumbani mwako. Akafanya haraka, akashuka, akamkaribisha kwa furaha. Hata watu walipoona, walinung'unika wote, wakisema, Ameingia kukaa kwa mtu mwenye dhambi. Zakayo akasimama, akamwambia Bwana, Tazama, Bwana, nusu ya mali yangu nawapa maskini, na ikiwa nimenyang'anya mtu kitu kwa hila namrudishia mara nne. Yesu akamwambia, Leo wokovu umefika nyumbani humu, kwa sababu huyu naye ni mwana wa Ibrahimu. Kwa kuwa Mwana wa Adamu alikuja kutafuta na kuokoa kile kilichopotea.

Nasadiki husemwa.

MAOMBI
Habari ya Zakayo inatuonyesha jinsi Yesu anavyoweza kubadili maisha yetu. Nguvu ya wokovu wake ilijulikana katika mabadiliko ya Zakayo.

Ee Bwana Mungu,
1. Zakayo alikutana na Yesu na maisha ya Zakayo yamebadilika: Ubadili maisha yetu tufanane zaidi nawe.

2. Zakayo alikuwa na hamu ya kumjua mwanao Yesu; utuamshe tuwe na hamu kukutana na Yesu mwanao katika Ndugu zetu, neno lako na Ekaristi Takatifu ili kuonja nguvu yako ya kutubadili.

3. Utupe matumaini kuwa kati ya wale waliopokelewa na kusamehewa nawe.

4. Zakayo alibadili mtindo wa maisha yake: Utujalie neema ya kushuhudia wokovu kwa ukarimu na hisani yetu.

5. Uwapokee marehemu wote waliotegemea ukarimu wa kukirimiwa nawe furaha ya milele.

Ee Baba wa huruma, unamtaka kila mmoja wetu aache njia ya ubinafsi akufuate wewe. Uyasikilize maombi yetu tupate nguvu ya kutimiza amri zako, kwa Kristo Bwana wetu. Amina.

SALA YA KUOMBEA DHABIHU:
Ee Bwana, tunaomba dhabihu hii iwe sadaka safi mbele yako, na ituletee zawadi takatifu ya huruma yako. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.

ANTIFONA YA KOMUNYO: Zab.16:11
Utanijulisha njia ya uzima; mbele za uso wako ziko furaha tele, ee Bwana

Au:
Yn.6:57

Bwana asema: Kama vile Baba, aliye hai, alivyonituma mimi, nami ni hai kwa Baba; kadhalika naye mwenye kunila atakuwa hai kwa mimi.

SALA BAADA YA KOMUNYO:
Ee Bwana, tunakuomba uweza wako uzidi kutenda kazi ndani yetu, ili, baada ya kulishwa sakramenti ya mbinguni, kwa neema yako tuandaliwe kupokea yaliyoahidiwa na sakramenti hiyo. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.