DOMINIKA YA 2 YA PASAKA MWAKA C
MASOMO
ANTIFONA YA KUINGIA: 1Pet.2:2
Kama watoto wachanga waliozaliwa sasa yatamanini maziwa ya akili yasiyoghushiwa, ili kwa
hayo mpate kuukulia wokovu, aleluya!
Au:
Ezr.2:36-37
Pokeeni furaha ya utukufu wenu, mkimshukuru Mungu aliyewaita kwa ufalme wake wa mbinguni,
aleluya!
Utukufu husemwa.
KOLEKTA
Ee Mungu wa rehema ya milele, wewe unaamsha imani ya taifa lako takatifu katika kurudia kila
mwaka kwa sikukuu ya Pasaka. Tunakuomba uongeze neema uliyolijalia, ili wote watambue kwa uelewa
sahihi thamani kuu ya Ubatizo uliowatakasa, ya Roho aliyewazaa upya na ya damu iliyowakomboa.
Kwa njia ya Bwana wetu Yesu Kristo Mwanao, anayeishi na kutawala nawe katika umoja wa Roho
Mtakatifu, Mungu, milele na milele.
SOMO 1: Mdo.5:12-16
Kwa mikono ya mitume zilifanyika ishara na maajabu mengi katika watu; nao wote walikuwako kwa nia
moja katika ukumbi wa Sulemani; na katika Wote wengine hapana hata mmoja aliyethubutu kuambatana
nao; ila watu waliwaadhimisha; walioamini wakazidi kuongezeka kwa Bwana, wengi, wanaume na wanawake;
hata ikawa katika njia kuu hutoa nje wagonjwa, na kuwaweka juu ya majamvi na magodoro, ili Petro,
akija, ngawa kivuli chake kimwangukie mmojawapo wao. Nayo makutano ya watu wa miji iliyoko kandokando
ya Yerusalemu wakakutanika, wakileta wagonjwa, nao walioudhiwa na pepo wachafu; nao wote wakaponywa.
WIMBO WA KATIKATI: Zab.117:2-4,22-27(K)1
1. Israeli na aseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
Mlango wa Haruni na waseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
Wamchao Bwana na waseme sasa,
Ya kwamba fadhili zake ni za milele.
(K) Mshukuruni Bwana kwa kuwa ni mwema,
Kwa maana fadhili zake ni za milele.
Au:
Aleluya, aleluya!
2. Ulinisukuma sana ili nianguke;
Lakini Bwana akanisaidia.
Bwana ni nguvu zangu na wimbo wangu,
Naye amekuwa wokovu wangu.
Sauti ya furaha na wokovu
Imo hemani mwao wenye haki. (K)
3. Ee Bwana, utuokoe, twakusihi;
Ee Bwana, utufanikishe, twakusihi.
Na abarikiwe yeye ajaye kwa jina la Bwana;
Tumewabarikia toka nyumbani mwa Bwana.
Bwana ndiye aliye Mungu,
Naye ndiye aliyetupa nuru. (K)
SOMO 2: Ufu.1:9-11a,12-13,17-19
Mimi Yohane, ndugu yenu na mwenye kushiriki pamoja nanyi katika mateso na ufalme na subira ya Yesu
Kristo, nalikuwa katika kisiwa kiitwacho Patmo kwa ajili ya Neno la Mungu, na ushuhuda wa Yesu.
Nalikuwa katika Roho, siku ya Bwana; nikasikia sauti kuu nyuma yangu, kama sauti ya baragumu,
ikisema, Haya uyaonayo uyaandike katika chuo, ukayapeleke kwa hayo makanisa saba. Nikageuka niione
ile sauti iliyosema nami. Na nilipogeuka, niliona vinara vya taa saba vya dhahabu; na katikati ya
vile vinara nikaona mtu mfano wa Mwanadamu, amevaa vazi lililofika miguuni, na kufungwa mshipi wa
dhahabu matitini. Nami nilipomwona, nalianguka miguuni pake kama mtu aliyekufa. Akaweka mkono wake wa
kuume juu yangu, akisema, Usiogope, Mimi ni wa kwanza na wa mwisho, na aliye hai; nami nalikuwa
nimekufa, na tazama, ni hai hata milele na milele. Nami ninazo funguo za mauti, na za kuzimu. Basi,
uyaandike mambo hayo uliyoyaona, nayo yaliyopo, na yale yatakayokuwa baada ya hayo.
SHANGILIO: Yn.20:29
Aleluya, aleluya!
Yesu alimwambia Tomaso,
Wewe, kwa kuwa umeniona, umesadiki;
Wa heri wale wasioona wakasadiki.
Aleluya!
INJILI: Yn.20:1-9
Ikawa jioni, siku ile ya kwanza ya juma, pale walipokuwapo wanafunzi, milango imefungwa kwa hofu
ya Wayahudi; akaja Yesu, akasimama katikati, akawaambia, Amani iwe kwenu. Naye akiisha kusema
hayo, akawaonesha mikono yake na ubavu wake. Basi wale wanafunzi wakafurahi walipomwona Bwana.
Basi Yesu akawaaambia tena, Amani iwe kwenu; kama Baba alivyonituma mimi, mimi nami nawapeleka
ninyi. Naye akiisha kusema hayo, akawavuvia, akawaambia, Pokeeni Roho Mtakatifu. Wowote mtakaowaondolea
dhambi, wameondolewa; na wowote mtakaowafungia dhambi, wamefungiwa. Walakini mmoja wa wale Thenashara,
Tomaso, aitwaye Pacha, hakuwako pamoja nao alipokuja Yesu. Basi wanafunzi wengine wakamwambia,
Tumemwona Bwana. Akawaambia, Mimi nisipoziona mikononi mwake kovu za misumari, na kutia kidole
changu katika mahali pa misumari, na kutia mkono wangu katika ubavu wake, mimi sisadiki hata kidogo.
Basi, baada ya siku nane, wanafunzi wake walikuwamo ndani tena, na Tomaso pamoja nao. Akaja Yesu,
na milango imefungwa, akasimama katikati, akasema, Amani iwe kwenu. Kisha akamwambia Tomaso, Lete
hapa kidole chako, uitazame mikono yangu; ulete na mkono wako uutie ubavuni mwangu; wala usiwe asiyeamini,
bali aaminiye. Tomaso akajibu, akamwambia, Bwana wangu na Mungu wangu! Yesu akamwambia, Wewe. kwa kuwa
umeniona, umesadiki; wa heri wale wasioona, wakasadiki. Basi kuna ishara nyingine nyingi alizozifanya
Yesu mbele ya wanafunzi wake, zisizoandikwa katika kitabu hiki. Lakini hizi zimeandikwa; ili mpate kuamini
ya kwamba Yesu ndiye Kristo, Mwana wa Mungu; na kwa kuamini mwe na uzima kwa jina lake.
Nasadiki husemwa.
MAOMBI
Ndugu zangu, baada ya matukio ya Ijumaa Kuu wafuasi walipoteza imani yote. Lakini imani yao hafifu
iliamshwa tena na Yesu mfufuka aliyewatokea mara kwa mara.
Ee Yesu mfufuka,
1. Imani yetu ni dhaifu sana. Uamshe imani yetu kama ulivyoamsha imani ya mitume wako.
2. Mtume Tomas hakutaka kuamini bila kuoneshwa alama zako. Utujalie kuonja nguvu yako katika maisha
yetu ili kuimarisha imani yetu.
3. Tunajua kwamba hatuwezi kukuamini bila kusaidiwa na neema yako. Utujaze neema yako ili ituimarishe
katika imani na upendo wetu kwa wenzetu.
4. Dalili chache zinatosha kuamsha imani yetu. Utujale kuona dalili chache za enzi yako katika maisha
yetu ili kutuimarisha katika maisha ya kila siku.
5. Ulisema: wenye heri wasioona na kusadiki. Uimarishe imani yetu ili kutuwezesha kukuamini kwa moyo
wote.
Ee Mungu Baba, sisi binadamu tuna shida zetu katika kuamini bila kuona kwa macho yetu ya kibinadamu.
Uangaze macho ya mioyo yetu ili tuone kwa imani yale yasiyoonekana kwa macho yetu. Tunakuomba kwa njia
ya Mwana wako Yesu Kristo anayeishi na kutawala pamoja nawe katika umoja wa Roho Mtakatifu, daima na
milele. Amina.
SALA YA KUOMBEA DHABIHU
Ee Bwana, tunakuomba uvipokee vipaji wanavyokutolea watu wako (pamoja na wanao
waliozaliwa upya), ili, wakiisha kufanywa wapya kwa kuliungama jina lako na
kwa Ubatizo, wapate kuifikia heri ya milele. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.
UTANGULIZI: Fumbo la Pasaka.
K. Bwana awe nanyi.
W. Na awe rohoni mwako.
K. Inueni mioyo.
W.Tumeiinua kwa Bwana.
K. Tumshukuru Bwana Mungu wetu.
W. Ni vema na haki.
K. Kweli ni vema na haki, tendo la kufaa na la kuleta wokovu, kukutukuza
kila wakati, ee Bwana, lakini hasa siku hii ya leo kutangaza utukufu wako, kwa kuwa Kristo, Pasaka
wetu, ametolewa sadaka.
Yeye ndiye Mwanakondoo wa kweli aliyeondoa dhambi za ulimwengu. Yeye ndiye aliyeangamiza mauti yetu
kwa kufa kwake, na alitengeneza upya uzima kwa kufufuka kwake.
Kwa sababu hiyo, katika upeo wa furaha ya kipasaka, ulimwengu mzima unashangilia. Lakini pia nguvu
za mbinguni na majeshi ya Malaika wanaimba utenzi wa utukufu wako, wakisema bila mwisho:
Mtakatifu, Mtakatifu, Mtakatifu, Bwana Mungu.
ANTIFONA YA KOMUNYO: 1Kor.5:7-8
Pasaka wetu amekwisha kutolewa kuwa sadaka, yaani Kristo, aleluya; basi na tuifanye karamu kwa
yasiyochachika, ndio weupe wa moyo na kweli, aleluya, aleluya!
SALA BAADA YA KOMUNYO
Ee Mungu, ulilinde Kanisa lako kwa wema wako wa daima, ili likiisha kufanywa upya kwa mafumbo ya
Pasaka, lipate kuufikia mwangaza wa ufufuko. Kwa njia ya Kristo Bwana wetu.